![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
➡️Maana mojawapo ya Neno "Unabii" ni kutamkwa mambo yatakayotokea Baadae.
◼️Watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU hutamka mambo ya ki MUNGU yatakayokuja kutokea Baadae.
Mfano ni huu.
Mwanzo 49:1 "Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho."
Yakobo anatoa Unabii wa mambo yatakayotokea Baadae, Yakobo katika ROHO MTAKATIFU anatoa hadi Unabii wa kuja Bwana YESU KRISTO ambaye alikuja kutokea zaidi ya miaka 1500 tangu Yakobo atoe Unabii huo.
Mwanzo 49:10 "Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii."
➡️Lakini kwa sababu kinywa kinaweza kuumba wapo pia watu wabaya wanaweza kumtamkia Mtu kipepo ili mambo fulani mabaya yampate, kama Mtu huyo hayuko thabiti katika KRISTO YESU mambo hayo humpata kweli.
➡️Wengine Wala sio watu wabaya ila ni watu wa kawaida tu ila kwa sababu siku hiyo walikuwa na hasira wanaweza kumtamkia Mtu jambo kibinadamu tu bila kumhusisha MUNGU na jambo hilo kinampata mhusika.
Mfano ni Nuhu baada ya kutoka kwenye ulevi alimtamkia Mjukuu wake kuwa mtumwa na ikawa hivyo.
Mwanzo 9:24-25 " Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema,Na alaaniwe Kaanani;Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake."
➡️Leo wapo watu walitamkiwa utumwa na Wazazi wao, wapo watu walitamkiwa kushindwa na ndugu zao na wapo watu walitamkiwa kufa na mapema na ikawa hivyo.
◼️Kuna faida ya ajabu Kuokoka na kuishi pamoja na Bwana YESU KRISTO, hata Kuna neno gani baya ulitamkiwa unaweza kulifuta kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO Kwa sekunde chache tu na halitatokea Tena jambo hilo.
Yohana 14:13-15 " Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu."
➡️Ndugu zangu katika utumishi wangu kwa KRISTO YESU, Mimi Peter Mabula nimewahi kukutana na watu wengi wanaotembea kwenye Unabii mbaya wa Maisha yao.
Kuna mmoja alitamkiwa na Baba yake wa kiroho akiwa Binti Mdogo sana, alitamkiwa hataolewa na baada ya hapo hakupata Mchumba hadi anafikisha miaka 50, alinisimulia kwa uchungu sana huku akilia akiniambia nimuombee na akasema tangu amezaliwa hajawahi kukutana kimwili na Mtu, hakujua kama alikuwa amefungwa kiroho kwa maneno Yale hadi alipokutana na somo langu mtandaoni.
➡️Kuna watu walitamkiwa mabaya na wakayazima hayo mabaya kwa Neno la MUNGU la Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
Mfano hai ni Goliath alimtamkia Daudi kwamba atamuua na mwili wake atawapa ndege na wanyama waule
1 Samweli 17:44 "Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni."
◼️Daudi baada ya kutamkiwa Unabii huo mbaya hakusubiri Ibadani ndio afute Bali aliufuta Unabii ule mbaya muda ule ule, aliufuta kwa kutamka maneno haya ya ushindi.
1 Samweli 17:45-46 " Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, MUNGU wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko MUNGU katika Israeli.
➡️Ndugu, Inawezekana unateswa na Unabii mbaya uliotamkiwa Maisha Yako, Leo unayo nafasi ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako Kisha omba au kuombewa ili Kufuta Unabii mbaya wote uliotamkiwa Maisha Yako.
Luka 11:10 "Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."
➡️Kuna watu walitamkiwa hawatafunga Ndoa, kuingia kwenye Ndoa kwao imekuwa vigumu sana.
➡️Kuna watu walitamkiwa kutokupata kazi au kutokuoa au kutokuolewa au kutokufanikiwa.
Ndugu Leo katika Jina la YESU KRISTO unaweza kuomba na Unabii mbaya wowote wa Maisha Yako ukafutika Leo Leo.
Yohana 15:7 "Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa."
➡️Kuna watu walitamkiwa kufa, Leo kwenye Maombi sema sitakufa Bali nitaishi katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Zaburi 118:17 "Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya BWANA."
➡️Ndugu, ni Unabii gani ulitamkiwa na Leo unakutesa?
Leo tumia Neno la MUNGU kwenye Maombi kufuta Kila Unabii mbaya uliotamkiwa Wewe au Watoto wako, au Ndoa Yako au watu wengine wanaokuhusu utakaotamani kuwaombea.
Zaburi 107:20-22 " Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments