| Na Mwl Peter Mabula Mtenda Kazi katika Shamba la MUNGU Mwenyezi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
Sasa kwa sababu ya umbali na wanafunzi tulikuwa wengi tulikuwa na taratibu za kucheza michezo mbalimbali na mingine ni michezo yenye uhalisia ndani yake, yaani kama ni mapigano ya watu wa njia hii na njia hii yalikuwa ni mapigano kweli.
Ila mchezo mmoja Maarufu nimeukumbuka, tulikuwa na utaratibu wa kuchora mstari kati ya Kundi A na Kundi B Kisha Kila Mtu wa Kundi Moja alitakiwa kuhakikisha Mtu wa Kundi jingine havuki mstari ili kuja upande wao.
Ilikuwa ni vita kubwa ila wababe tu ndio waliofanikiwa kuvuka, na waliovuka ndio washindi na wao ndio walipewa sifa ya kuwa watu wababe na wanaoogopeka.
➡️Kwanini ushuhuda huu au Mfano huu nautumia Leo?
Huo ni mfano wa kimwili wa kuwekewa mpaka ili usivuke.
➡️Ni kwamba leo wapi watu wengi wamewekewa mistari na Wachawi ili wasivuke kuingia mafanikio fulani.
➡️Leo wapo watu wamewekewa mipaka ya mistari ili wasivuke kuingia hatua fulani nzuri ya Maisha.
Mfano hai ni Farao aliyewawekea Waisraeli mipaka ya kutoondoka Misri akitaka waendelee kumtumikia, hadi MUNGU alipoingilia kati kwa mapigo mazito ndio akawaachia.
Kutoka 9:2-3 " Kwani ukikataa kuwapa ruhusa waende, NA KUZIDI KUWAZUIA, tazama, mkono wa BWANA u juu ya wanyama wako wa mifugo walioko kondeni, juu ya farasi, na juu ya punda, na juu ya ngamia, na juu ya ng'ombe, na juu ya kondoo; kutakuwa na tauni nzito sana."
➡️Biblia inasema Farao hakutaka Waisraeli waende kwenye mafanikio yao hivyo aliwazuia yaani aliwawekea mipaka ya mafanikio.
➡️Farao alizidi kuwazuia Waisraeli ili wasiende kwenye baraka zao hadi MUNGU alipoingilia kati.
➡️Hata Leo Kuna Mtu anaweza kuzuiliwa kiroho kwenye jambo Fulani la baraka.
Hata Leo Kuna Mtu anaweza akawekewa mipaka ya kufanikiwa ambayo hadi Maombi katika jina la YESU KRISTO ndio hatazuilika.
➡️Hujawahi kuona Mtu akipata pesa nyingi kidogo tu ndio matatizo na majanga yanakuja ghafla ili kuondoa hizo pesa?
Huyo amewekewa mipaka ya mafanikio ya kiuchumi.
◼️Ndugu, katika KRISTO YESU unaweza kuvuka mistari yote uliyowekewa na maadui zako katika ulimwengu wa roho.
Wafilipi 4:13 " Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."
◼️Ndugu, kama umeokoka na YESU KRISTO ni Bwana na Mwokozi wako unaweza kuvuka mistari yote ya washirikina na wanaotumika kishetani dhidi Yako wote.
Yaani kama walikulaani au kukushikilia kiroho kwa Maombi Yako katika Jina la YESU KRISTO wao ndio watashikiliwa na laana waliyokutamkia Wewe itawapata wao.
Zaburi 109:17 "Naye alipenda kulaani, nako kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye,"
➡️Je umewekewa mipaka ya kukuzuia kufanya Nini?
➡️Je umewekewa mipaka ili usizae kwenye Ndoa Yako au ili usipate kazi au ili usipone ugonjwa?
MUNGU wa Mbinguni anaweza kufuta mipaka hiyo Ukiomba katika Jina la YESU KRISTO.
Ukiwa ndani ya Wokovu wa KRISTO Kwa uaminifu MUNGU anaweza kutokusikiliza laana zote na maapizo yanayoelekezwa kwako.
Alifanya hivyo kwa kugeuza maapizo mabaya juu ya Waisraeli, maapizo hayo yakageuka kuwa baraka.
Kumbu 23:5" Lakini BWANA, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; BWANA, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda BWANA, Mungu wako."
◼️Ndugu, Leo omba kuondoa mipaka ya kichawi yote uliyowekewa katika ulimwengu wa roho.
Omba ukiamini utaona Maajabu ya MUNGU wa Mbinguni.
Marko 9:23 "YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye."
◼️Kwa Jina la YESU KRISTO unaweza kuvuka mistari ya Wachawi wote na waganga wote, waliyokuzia kuzaa au kuingia katika Ndoa au kupata kazi au kufaulu au kufanikiwa katika biashara Yako, omba Leo katika Jina la YESU KRISTO Kila mistari uliyowekewa itaondoka na hutazuilika Tena.
Mathayo 17:20 "YESU akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu."
◼️Mtu aliyeokoka hazuiliwi na Wachawi Wala waganga wa kienyeji Wala mawakala wengine wote wa shetani, maana anaomba katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.
Comments