MAMBO 7 ALIYOYAFANYA BWANA YESU BAADA YA KUFUFUKA.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Tunafahamu kwamba Bwana YESU alikufa na baada ya siku 3 alifufuka, baada ya kufufuka alikaa siku 40 kabla ya kupaa Kwenda Mbinguni.

Matendo  1:2-3 " hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa ROHO MTAKATIFU wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa MUNGU."

◾Katika siku hizi 40 tunaangalia yale aliyoyafanya, Inawezekana yapo zaidi ya 7 ili Mimi nimepewa Neema kwa sasa ya kujua haya 7.

◾Mambo 7 aliyoyafanya Bwana YESU baada ya kufufuka.

1. Kukutana na wanafunzi wake 11 na kuwathibitishia kuwa ni yeye amefufuka.

Yohana 20:19-20 " Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja YESU, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana."

➡️Hapa hata wale Wanafunzi waliokuwa na mashaka alijidhihilisha kwao ili mashaka yao yaondoke.

◼️Mfano hai ni Tomaso ambaye  alitaka kuamini kama YESU amefufuka kwa kumuona live ndipo aamini.

Yohana 20:27-29 " Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na MUNGU wangu! YESU akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.

  ◼️Kwa sababu Mitume hawa walitakiwa kuhubiri Injili yake alijidhihilisha kwao ili wasiwe Tena na Mashaka, na hata wakiulizwa na watu  "YESU alikufa je ulimuona alipofufuka hata tumwamini" wangesema kwa ujasiri wote kwamba "hakika nilimuona hivyo mpokeeni haraka kama Mwokozi wenu"
 
◼️Bwana YESU baada ya kufufuka alihakikisha wanafunzi wake wote isipokuwa yuda ambaye alikuwa ameshajinyonga, Bwana YESU alihakikisha wake wanafunzi wake 11 wanagundua ni yeye.

Marko 16:14 "Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu."

◼️Bwana YESU KRISTO alihakikisha Mitume wote wanamuona na kumtambua, hiyo ndio ilikuwa kazi yake kubwa kuifanya baada ya kufufuka kwake.

Yohana 21:9-12 " Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. YESU akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka. YESU akawaambia, Njoni mfungue kinywa. WALA HAKUNA MTU KATIKA WALE WANAFUNZI ALIYETHUBUTU  KUMWULIZA, U NANI WEWE? WAKIJUA YA KUWA NI BWANA."

2. Kuwatangazia wanafunzi wake majira ya  ujio wa ROHO MTAKATIFU, hivyo wamsubiri ROHO MTAKATIFU kabla ya kuanza Kuhubiri Injili ya Wokovu wake.

Matendo  1:4-5 " Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya BABA, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika ROHO MTAKATIFU baada ya siku hizi chache."

◼️Ujio wa ROHO MTAKATIFU ndio tukio kubwa zaidi ili Kanisa la MUNGU Duniani liwe hai.
Bwana YESU KRISTO aliwaambia Wahubiri wa Mwanzo wa Injili kwamba wasianze kuhubiri Injili kabla ya ROHO MTAKATIFU hajaja kwao, hivyo wakae sehemu Moja wasubiri.

◼️Pia Kuwajulisha Nguvu ya ROHO MTAKATIFU watakayoipokea maana walikuwa bado hawajawahi kuipokea Nguvu ya ROHO MTAKATIFU.
                                             
Matendo  1:8-9 " Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao."

➡️Ni kweli siku kumi baada ya Bwana YESU KRISTO kupaa Mbinguni ROHO MTAKATIFU alikuja na ndipo Mwanzo wa Ajabu wa Injili ya KRISTO ulianza na hata Leo Mamilioni ya Watumishi wa MUNGU wa ROHO MTAKATIFU hivyo wanahubiri Injili ya KRISTO Duniani kote kwa ujasiri mkubwa.

Matendo  2:1-4 " Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
 Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka."

3. Kukutana na Watu wengine nje na wanafunzi wake 11 ili kuwathibitishia kuhusu yeye akawaambia unabii kumhusu yeye wanaoufahamu.

➡️Mfano hapa alikutana na watu ambao sio Wanafunzi wake.

Luka 24:13-16 " Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, YESU mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue."

 ➡️Bwana YESU hadi aliwauliza Maswali juu ya mambo yanayoendelea hapo mjini Yerusalemu Wakamwambia habari kubwa ni kuhusu YESU KRISTO na kwamba Kuna watu hawajauona mwili wake Kaburini.

Luka 24:22-24 " tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona."

◼️Baadae alienda hadi nyumbani kwao akala na Chakula Kisha  yalifumbuliwa macho yao wakamfahamu ndipo akaondoka kwao.

Luka 24:31 "Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao."

◼️Hii ilikuwa Muhimu sana Ili hata makuhani ambayo wangekataa kuwaamini Mitume wangeshangaa kuona Waumini wao wenyewe wanashuhudia Wamemuona YESU baada ya kufufuka.

◼️Lakini pia Labda hii ilikuwa ili kufuta uongo wa makuhani waliomsulubisha ambao hadi waliwahonga Askari ili waseme uongo.

Mathayo 28:11-15 " Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo."

◼️Hata Leo kama Kuna Mtu anakataa kwamba Bwana YESU hakufufuka huyo Yuko Kundi la Waliodanganywa kwa uongo wa makuhani wapinga KRISTO.

4. Kuwafunulia akili Wanafunzi wake ili wawe na uwezo wa kuelewa Maandiko.

Luka 24:44-45 " Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko."

◼️Mtu aliyefunuliwa na Bwana YESU kuelewa Maandiko huwezi kumtoa kamwe kwa YESU KRISTO, ndio maana Mitume baada ya hapa hata walipotishiwa kufa hawakumkana Tena Bwana YESU KRISTO maana walimfahamu YESU na walielewa maandiko.

5. Kuwafundisha wanafunzi wake nini wafanye yeye akiondoka.

Mathayo 28:18-20 " YESU akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari."

◼️Aliwaambia wanahubiri Injili kwa watu wote ili kuwafanya Watu wote kuwa Wanafunzi wake.

◼️ Aliwaambia katika kuwahubiria watu Wawabatize wale wanaompokea.

◼️ Aliwaambia wawafundishe watu wote kuyashika aliyofundisha yeye Bwana YESU KRISTO.

➡️Hii ilikuwa kazi nyingine Muhimu sana, kwamba Nini wafanye Mitume baada ya Bwana YESU KRISTO kuondoka.

 Yohana 20:21-23 " Basi YESU akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama BABA alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni ROHO MTAKATIFU. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa."

6. Kuwajulisha Wanafunzi wake nini kitaambatana nao wakati watakapohubiri Injili yake maeneo mbalimbali.

Marko 16:15-18 " Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.

◼️Bwana YESU KRISTO hakuwaficha ili muda ukifika wasishangae kile kitakachokuwa kinatokea ambacho huambatana na Injili ya KRISTO Mwokozi.
Mambo ambayo yangeambatana nao wakiwa katika kuhubiri ni pamoja na haya; Watu Kuokoka, kutoa mapepo, kunena kwa lugha katika ROHO MTAKATIFU,  kuombea Wagonjwa wanapona n.k

7. Kumtakasa Petro aliyemkana na Kisha  kumpa majukumu.

➡️Kumbuka Petro alikuwa ni Kiongozi wa mitume wote ila akafanya kosa baya la kumkana Bwana YESU.
Katika yale aliyoyafanya Bwana YESU KRISTO baada ya kufufuka tukio Moja wapo ni kumtakasa Petro ndio maana baada ya kumtakasa akampa kazi kuu.

Yohana 21:14-17 " Hiyo ndiyo mara ya tatu ya YESU kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu. Basi walipokwisha kula, YESU akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. YESU akamwambia, Lisha kondoo zangu."

➡️Labda pia Petro alikuwa na mawazo baada ya kumkana, YESU alionyesha amemsamehe hivyo amempa nafasi ya Utumishi na uongtozi  kwa wenzake.

◼️Baada ya mambo hayo 7 na mengine mengi aliyoyafanya Bwana YESU baada ya kufufuka alipaa Kwenda mbinguni.

◼️Siku moja atarudi na Wanadamu wote wa dini zote watakusanyika mbele zake na yeye atatoa hukumu.

Mathayo 25:46 "Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele."

◼️Ndugu jiandae kwa ujio wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu.

  Ufunuo  22:20 "Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana YESU."

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe. 

Comments