MAMBO YANAYOAMBATANA NA MTU AMCHAYE MUNGU.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU Mwenyezi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.


◼️Leo tunaangalia Mambo yanayoambatana na Mtu amchaye MUNGU.


◼️Mcha MUNGU ni Mtu anayemwogopa na kumpenda MUNGU.


➡️Mfano hai wa Mtu aliyekuwa anamcha MUNGU ni Ayubu.


Ayubu 1:8 "Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha MUNGU na kuepukana na uovu."


◼️Mcha MUNGU ni mtu anayependezwa na maagizo ya MUNGU hivyo huyafuata siku zote katika KRISTO YESU. 


➡️Mfano hai wa Mtu alikuwa anamcha MUNGU ni Obadia.


1 Wafalme 18:3 "Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha BWANA sana;"


➡️Wacha MUNGU ni watu Muhimu sana  kuna wakati walipungua sana Duniani.


Mika 7:2 "Mtu amchaye MUNGU ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu."


◼️Hivyo Watu wanaomcha MUNGU ni wachache kulinganisha na watu wasiomcha.


◼️ Ndugu Jitahidi sana Wewe uwe ni mmoja wa watu waliookoka wanaomcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.


◾Mambo gani basi ambayo yanaweza yakaambatana na Mtu amchaye MUNGU katika KRISTO YESU.

 

1. Mtu anayemcha MUNGU hukubaliwa na MUNGU.


Matendo  10:35 "bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye."


◼️Ukitaka uwe Mtu wa kukubaliwa na MUNGU daima basi mche yeye daima katika KRISTO YESU.


◼️Kumcha MUNGU katika KRISTO YESU kutaambatana na kukubaliwa na Yeye, ni baraka sana kukubaliwa na MUNGU.


2. Mtu anayemcha MUNGU , MUNGU atamfundisha kwa njia yake aliyoichagua.


Zaburi 25:12 "Ni nani amchaye BWANA? Atamfundisha katika njia anayoichagua."


◼️ Kumbe ukimcha MUNGU atakuchagulia njia nzuri ya kupita ili ufanikiwe, na ili uwe salama, na ili ubaki katika utakatifu na katika KRISTO  YESU.


3. Mtu amchaye MUNGU atapata sifa njema inayoweza kumfanya kuchaguliwa kwa ajili ya Ndoa safi.


Mithali 31:30 "Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa."


◼️Ukitaka Ndoa njema ambatana na ucha MUNGU maana watu watakuona na utapata sifa njema na kupata Mtu sahihi kwa ajili ya Ndoa.

Kumbuka hakuna Mtu anayetaka kuoana na mchawi au mzinzi, Kila Mtu anataka Mtu mwema na Mtu mwema sahihi ni yule anayemcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.


4. Mtu anayemcha MUNGU hupata familia bora na familia yake aliyoanzisha hubarikiwa.


Zaburi 128:1-4 " Heri kila mtu amchaye BWANA, Aendaye katika njia yake. Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye BWANA."


◼️Hii ni Ahadi njema ya MUNGU Kwa wamchao na hutimia kwao, hivyo chagua Ndugu kumcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.


5. Mtu anayemcha MUNGU hutii  sauti ya Watumishi wa kweli wa KRISTO.


Isaya 50:10 "Ni nani miongoni mwenu amchaye BWANA, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la BWANA, na kumtegemea MUNGU wake."


◼️ Mcha MUNGU huwa ana ROHO MTAKATIFU hivyo sauti ya MUNGU kupitia watumishi wake wa kweli Mtu huyo huitii na kuifuata.


6. Kumcha MUNGU ndio mwanzo wa akili njema kwa Mtu.


Zaburi 111:10 "Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele."


◼️Ukitaka uwe na akili njema zingatia sana kumcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.


Mithali 1:7 "Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu."


7. Mtu anayemcha MUNGU hupendezwa na maagizo ya MUNGU.


Zaburi 112:1 "Haleluya. Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo yake."


➡️Hakuna Mcha MUNGU wa kweli anayeweza kuchukizwa na maagizo ya MUNGU wa Mbinguni.


➡️Hakuna Mcha MUNGU halisi ambaye anaweza kuchukizwa na maelekezo ya ROHO MTAKATIFU.


◼️Mcha MUNGU hupendezwa na maelekezo yote ya Bwana YESU KRISTO.


◼️Mcha MUNGU huishi na kufuata yote ambayo ROHO MTAKATIFU anakuambia.


Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments