![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Rafiki mmoja katika KRISTO ambaye ni Mchungaji wa Kanisa aliniandikia
"AM SORRY NIMEKUA NA CHANGAMOTO KUBWA MNO YA KIHUDUMA NAOMBA UNISAIDIE.
NIMEFUNGA NA KUOMBA NA KUFANYA SEMINA LAKINI SIONI MATOKEO.
NA MIMI NILIHITAJI KUONA WAZALIWA WAPYA NDANI YA KANISA NILIPOPANDWA NA BWANA.
NIMEONA HAMNA MAONGEZEKO NA NIMEFANYA KILA NJIA
HIVYO NAOMBA USHAURI MY TEACHER TAFADHALI NIELEKEZE NAMNA GANI NIFANYE ILI KUONA UPENYO WA KIMAONGEZEKO NDANI YA KANISA"
➡️Baada ya ujumbe huo, nilitoa majibu ambayo ROHO MTAKATIFU alinipa kumpa na katika ujumbe huu nauweka kama somo yamkini majibu haya yakamsaidia na Mtu Mwingine anayemtumikia Bwana YESU KRISTO au ana Ufunuo wa Utumishi ndani yake.
◼️Umechagua Fungu jema sana kumtumikia Bwana YESU KRISTO.
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana."
◾Vitu vinachoweza kuwaleta watu wengi Kanisani ni
1. Kufundisha fundisho sahihi la KRISTO.
2 Yohana 1:9 "Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia."
➡️Hatuna fundisho jipya la Wokovu wa KRISTO bali fundisho ni lile lile walilofundisha Mitume wa KRISTO ambapo fundisho hilo linawataka watu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao, kuishi maisha matakatifu katika Wokovu, kufanya kazi zao njema na huko kwenye Maisha yao wakimtegemea MUNGU.
➡️Baki ukiwafundisha watu umuhimu wa Kuokoka, umuhimu wa kuishi maisha matakatifu na umuhimu wa kufanya kazi njema huku wakimtegemea MUNGU.
2. Kushuhudia watu mitaani ili waje kwa YESU na kuwaalika kwa kuhusu watu wengi ili waje Kanisani.
Marko 16:15-16 " Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa."
◼️Hakikisha Kanisa Lina muda Mwingi wa kushuhudia Injili nyumba kwa nyumba na mitaani, kualika watu wengi Ibadani, mkifanya hivyo ndani ya miaka 2 Kanisa litakuwa mbali sana.
➡️Kumbuka tu kushuhudia watu ambao hawajaokoka, usijaribu kuhamisha watu kutoka Makanisa mengine ya kiroho ambao unajua kabisa wameokoka na wanaishi Maisha Matakatifu, Wewe wafuate zaidi watu ambao hawajaokoka ili wakiokoka watakuwa baraka inayodumu Kanisani.
3. Wanaokuja Kanisani Hakikisha wamefunguliwa na kuwa huru.
Mathayo 10:8 "Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure."
◼️Injili ya KRISTO inaambatana na watu kuwekwa huru dhidi ya dhambi na dhidi ya vifungo vya giza vyote.
Marko 16:17-18 " Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya."
◼️Ili watu wafunguliwe Kanisa lazima liwe na vipindi vingi vya Maombi ya kina, mikesha na wahudumu wote kuwa waombaji wanaoutafuta uso wa MUNGU ili Udhihirisho wa Nguvu za ROHO MTAKATIFU uwe mkubwa na hapo ndipo watu wataiona tofauti ya hapo na kule walikokuwa kabla hawajaokoka.
Isaya 55:6-7 " Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa."
4. Wewe na Viongozi wa Kanisa lenu Hakikisheni daima mna ushuhuda mzuri wa tabia njema na mwenendo mzuri ndani ya Wokovu wa KRISTO YESU
Tito 2:7-8 " katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu."
◼️Wewe na Viongozi wenzako wa Kanisa Hakikisheni mnakuwa Mfano Bora kwa tabia njema, lugha ya staha, Matendo mema na ucha MUNGU wa kweli.
5. Fanya kile MUNGU amekuitia.
Wafilipi 2:13-14 " Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,"
◼️Katika hili msikilize sana ROHO MTAKATIFU au muulize amekuita kufanya Nini.
Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."
◼️Ukifanya alichokuitia ROHO MTAKATIFU watu wengi sana watakuja Kanisani.
Yohana 15:16 "Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni."
Mfano Mimi nilikuwa napenda sana kuwa mwinjilisti, nikitamani kufundisha style ya uinjilisti na nihubiri na sio kufundisha lakini ROHO MTAKATIFU tarehe 20 April 2017 alisema na Mimi kwamba ameniita kuwa Mwalimu wa kufundisha Neno la MUNGU, hivyo alinisahihisha mawazo yangu yaliyokuwa kinyume na wito wangu.
Lakini pia hata ualimu alioniitia ni ualimu wa aina gani?
Alisema na Mimi kwa Mfano mingi hadi nikaelewa, Kuna wakati kwa Maono hadi alinionyesha Maono ya miaka zaidi ya elfu kabla ya KRISTO akiniambia nifanye kwa namna ya Sasa katika KRISTO YESU, siwezi kusema ni Maono gani ila nilijua kwa usahihi kabisa.
Na wakati bado nayashangaa yale Maono ya wazi watu 2 mmoja kutoka Congo na Mwingine Mchungaji kutoka Kenya walinitafuta kwa njia ya Whatsapp wakiniambia Maono waliyoyaona kuhusu huduma yangu, na yote yana maana Moja na yale niliyoyaona Mimi hivyo nikaelewa nimeitwa kwenye ualimu kwenye sekta gani.
Nasema haya ili ufanye juhudi kujua umeitiwa Nini.
Kuna wakati kulikuwa na Nafasi ya kuchunga Kanisa sehemu 3, sehemu ya kwanza ni Kanisa la mahali ambapo Mchungaji alilikimbia Kanisa hivyo wazee wa Kanisa wakaniomba nikawa Mchungaji, sehemu ya pili ni Wamishionari walihubiri sehemu kusini mwa Tanzania watu wengi wakaokoka Wahubiri wakarudi Ulaya, watu wakawa wanafanyia Ibada kwa mwenyekiti wa Kijiji na ni Wengi, mwenyekiti kwa sababu alikuwa anatumia masomo yangu akanitaka niende nikawa Mchungaji na sehemu ya tatu Mchungaji aliondoka Duniani na Nafasi ya Uchungaji ikawa wazi kwa muda hivyo walihitajika Wachungaji angalau wawili wanaojua mazingira hayo ili kwa muda wahudumie huduma ile.
Kitu Cha Ajabu ni hiki katika mazingira hayo Moyo wangu wangu Mwanzo ulikataa lakini kwa sababu ya ushawishi kutoka kwa watu nikawa natamani kuwa Mchungaji wa mahali lakini Bwana YESU KRISTO akanitokea mwenyewe na kuniambia hajaniita kuchunga Kanisa kwa wakati huo, ila akanionyesha kazi aliyoniitia.
Hapo nikajifunza kumbe ni Muhimu sana kufanya tu kile MUNGU amekuitia katika Mwili wa KRISTO hata kama kazi zingine zinakuvutia kuliko hiyo, Baki katika kile Bwana YESU KRISTO amekuitia kwenye kazi yake ndipo utaona matunda mengi sana.
Kuna Mtumishi mmoja Mtanzania Yuko Marekani alitaka sana niende huko, alikuwa tayari kutuma nauli na akawa ananisisitiza sana nikamilishe mambo ya hati ya kusafiria, hata nilipopata hati ya kusafiria rohoni nilikatazwa hivyo kumtii MUNGU ni Bora zaidi kuliko kuwasikiliza Wanadamu.
Mtumishi wa MUNGU alikuwa na nia nzuri sana kwangu ila wito ulikataa kwa wakati huo, MUNGU ndio ajuaye hivyo ni Muhimu sana kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na kumtii.
◼️Ukifanya alichokuitia MUNGU watu watakuja wengi hata bila kutumia Nguvu nyingi.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments