![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Wokovu ndio Kuokoka kwenyewe.
◼️Wokovu sio dini mpya, Wokovu ni kumleta YESU KRISTO ndani ya Mwanadamu na ndio kazi ya Injili wakati Kanisa Duniani likianza.
Matendo 4:12 "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo."
◼️Injili ya Wokovu ndio walihubiri Mitume wote kabla dhehebu lolote la leo halijaanzishwa, hivyo kama Kuna Kanisa wanahubiri Wokovu wa KRISTO hilo sio Kanisa jipya bali ndio Kanisa lenye msingi wa Mitume wa Bwana YESU KRISTO ndani ya Biblia.
◼️Kanisa ambao hawahubiri Wokovu wa KRISTO hao ndio Kanisa jipya na lisilo na maana hata kama kibinadamu linaonekana ni dhehebu kubwa.
Kuna Maeneo tukienda kuhubiri watu wampokee YESU KRISTO na kuokoka watu wa eneo hilo wanatuona kama tunaleta dini mpya wakati sisi ndio tunawaletea dini ya kwanza na ya MUNGU kwamba ulimwengu mzima uhubiriwe Injili ya KRISTO.
Luka 24:47 "na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu."
➡️Kuna tofauti ya dini na Wokovu, kitu Muhimu zaidi kwa Mwanadamu sio Dini bali ni Wokovu.
Kumbuka Wokovu ndio Kuokoka kwenyewe.
Matendo 16:30-32 " kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la BWANA, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake."
➡️Watu wengi zaidi wamekimbilia zaidi Dini na sio Wokovu.
Yakobo 1:26 "Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai."
◼️Kumbuka Dini haiwezi kumpeleka Mtu yeyote Mbinguni ila Wokovu unampeleka Mtu uzima wa Milele.
Yuda 1:3 "Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu."
◼️Ndio maana unaitwa Wokovu wa Milele ila hakuna neno "Dini ya Milele"
Waebrania 5:9 "naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;"
◼️Narudia Tena hakuna andiko linalosema Kuna dini ya Milele ila andiko linalosema kwamba Wokovu ni wa milele lipo, hivyo fuata kitu Cha Milele na sio kitu Cha muda tu, dini au dhehebu ni vya muda tu ila Wokovu ni wa milele.
➡️Watu wengi zaidi wanapenda Dini na sio Wokovu hiyo imepelekea watu wengi kudhani Wokovu ni dini mpya kumbe Wokovu ndio ulianza.
Mitume wote hawakuhubiri Dini ila walihubiri Wokovu.
Ndugu, nakushauri kaa ndani ya Wokovu wa Bwana YESU, Jifunze Neno la MUNGU ndani wa Wokovu na Hakikisha unakua Kiroho ndani ya Wokovu wa KRISTO YESU.
1 Petro 2:2-3 " Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili."
◼️Wokovu unaanza na kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako Kisha ukaanza kuishi maisha matakatifu katika yeye ulifuata Neno la Injili yake Takatifu.
Yohana 1:12-13 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments