SIRI YA TAIFA LA ISRAELI.




BWANA YESU asifiwe rafiki popote ulipo.

Nakukaribisha sana katika ujumbe huu mhimu wa kujua na kufahamu  juu ya taifa la Israel. Ndugu rafiki wa Maisha ya ushindi hakika utabarikiwa na kujifunza kitu muhimu sana .

Karibu.

"Magen David" au nyota ya Daudi ni ishara ya Uyahudi,
Israel ni taifu la MUNGU, nikisema ni taifa la MUNGU ni kwa sababu MUNGU mwenyewe alilichagua taifa hili. Tunaona mataifa mengi mfano ya kiafrika yalitokana na Berlin conference au mkutano wa Berlin wa mwaka 1984 chini ya uenyekiti wa mkuu wa taifa la ujerumani Bismark ambapo wakuu wa mataifa ya ulaya waliligawa bara zima katika nchi ndogondogo kwa leo lao la kutawala katika makoloni hayo, hata Tanzania, Kenya, Uganda,Burundi, Rwanda, Zambia,Msumbiji, Kongo na hata Malawi ndipo yalipoanzia katika mkutano huo, vivyo hivyo mataifa mengine kama marekani au Brazil yalianza kutokana na mipango ya wanadamu fulani katika dunia hii lakini tukiizungumzia Israel tunazungumzia taifa ambalo halikutokana na vikao wala mikutano yeyote ya kibinadamu bali MUNGU mwenyewe ndie alipanga huko mbinguni, Hivyo Israel ndilo taifa pekee ambalo kuwepo kwake kuwa taifa ni mipango ya mbinguni.  Na chanzo cha taifa hili ni kuitwa na MUNGU kwa Ibrahimu (Mwanzo 12 :1-3, BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuambia. Nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka. Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa).

BWANA YESU asifiwe! Huo ndio ukawa mwanzo wa taifa hili la MUNGU, Kumbe ukiwalaani Israel utalaaniwa na ukiwabariki utabarikiwa, aliyesema ni MUNGU wala sio mwanadamu. Kumbe mimi Peter Michael Mabula natakiwa kuwabariki Israel kama neno la MUNGU linavyosema na wewe ndugu yangu hakikisha unalibariki taifa hili na kuliombea pia.

Tunafahamu Ibrahimu alimzaa Isaka ambaye ndiye aliyebeba kusudi hili la MUNGU baada ya Ibrahimu na Isaka akamzaa Yakobo ambaye alilibeba kusudi hili la MUNGU. Na Yakobo akazaa watoto 12 ambao baadae walikuwa makabila 12 ya Israel.

-Jina ISRAELI linatokana  na jina la pili alilopewa Yakobo na Malaika baada ya mashindano yake na Malaika wa MUNGU huko Penuel. Israeli maana yake ni ‘’aliyeshindana na MUNGU  Mwanzo 32:28). Hilo jina ISRAEL alilitoa MUNGU kwa kwa baba mkuu wa taifa hili la Israel.

-Waisrael huitwa wayahudi, MYAHUDI ni jina linalotokana  na jina la YUDA  mwana wa 4 wa Yakobo(Mwanzo 29:35, Maana ya Yuda ni sifa kuu) na kwa jina la kitaifa yaani wayahudi mwanzo lilihisu watu wa kabila hilo tu yaani kabila la Yuda au Wayuda au wayahudi. Baada ya kugawanyika kwa ufalme (950 K.K) lilikuwa na ufalme wote wa kusini yaani  Benjamini na Yuda (2 Wafalme 16:6, Yeremia 32:12), na baada ya kurudi kutoka kifungo cha Babeli(538 K.K) Lilikuwa ni jina la makabila yote 12 (Mathayo 27:29,37)

Picha:Flag of Israel.svg
Bendera ya Israeli
-Pia waisraeli wanaitwa waebrania, Jina WAEBRANIA linatokana na jina la Eberi(Maana yake ‘’mtu wa ng’ambo’’ Mwanzo 10:21,24, Mwanzo 11:14-15), na inaonekana kama jina hili linahusiana na uhamiaji wa ukoo wa Ibrahimu tusioujua  uliotoka ng’ambo ya mto yordani, Eberi alikuwa alikuwa wa saba kabla ya Ibrahimu, pia alikuwa babu mkuu wa washemi wengine kama vile Ofiri na Havila(Mwanzo 10:25-30), kwa hiyo neno waebrania  hapo mwanzo lilihusu ukoo mkubwa kabla ya Ibrahimu Tazama Mwanzo 14:13, Mwanzo 39:14,17, Mwanzo 43:32. Katika unabii wa Balaamu (Hesabu 24:24), Eberi anatajwa pamoja na Ashuru, Baada ya muda mrefu jina hilo liakawa la taifa moja la agano la kale, likitofautiana na makabila mengine ya ukoo huo mkubwa( Kutoka 5:3, 1 Samweli 4:6, Yoha 1:9)

Israel ni muhimu sana kwa kanisa na waenda mbinguni wote ambao wanampa BWANA YESU maisha yao.

   ISRAELI NI KATIKATI YA DUNIA.

-Israeli inasemwa kuwa ipo katikati  ya dunia(Ezekieli 38:12c-wakaao katikati ya dunia. ) yaani Israeli ni kama daraja la kati ya mataifa makuu katika ulimwengu wa kale, ni mahali ambapo bara kuu 3 za duniani zinakaribiana sana yaani Afrika, Ulaya na Asia. Ndio maana mataifa ya Misri, Uashuru na Babeli yalipigana vita ili kulipata daraja hilo.

-Israeli ilifaa zaidi ili kutoka huko injili  ipelekwa duniani maana Yerusalemu iko kati ya mataifa (Ezekieli 5:5 BWANA MUNGU asema hivi; Huu ndio Yerusalemu; nimeuweka kati ya mataifa, na nchi zauzunguka pande zote. -)

                                        KAZI YA ISRAELI

1.  Israeli ilikuwa mpokeaji wa ufunuo wa MUNGU na makao makuu ya Mwokozi YESU KRISTO wetu alipokua duniani.

2. Israeli ilikuwa  chanzo cha kanisa la KRISTO(Yohana 4:22-Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. ) pia Warumi 11:16-24

3. Ilitakiwa kuandaa njia ili injili iyafikie mataifa yote yaani iwe mfereji wa ufunuo wa wokovu duniani kote.

4. Israeli lilikuwa taifa lililotengwa na mataifa mengine, yaani lilikuwa taifa la tofauti kabisa na mataifa ya kipagani.

5. Israeli ni  taifa la ufunuo, linalomjua MUNGU wa pekee aliye hai.(Zaburi 83:18 -Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote. ).

6. Israeli ni taifa ambalo MUNGU aliwajulisha mapenzi yake  kupitia Manabii na watumishi wake mbalimbali.

7. Israeli  ni mzaliwa wa kwanza wa mataifa yote, ni lango kwa mataifa mengine yote.





Hakuna aliye kama MUNGU wa israeli, na ni watu walio na ukipekee mwingi na unaweza kuona hata kipindi Hitler kiongozi wa ujerumani akiwatesa waisraeli katika vita kuu ya pili ya dunia ni kwa sababu ya vipaji vya kipekee walivyonavyo waisraeli maana kwa miaka michache madaktari wataalam walikua wao, na watalaamu wa mambo mengine mengi walikua ni wao hivyo kiongozi huyo akaana kuwa kuwaacha hawa waishi watachukua idara nyeti za taifa huku wakiwa watumwa. Na hata leo Marekani kuna waisraeli ambao ni wataalam wa hali ya juu katika sekta nyeti kwenye taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani na ukiibariki Israeli hakika unabarikiwa na wewe kama ilivyo kwa marekani.

Naamini kwa sehemu umejifunza kitu cha muhimu sana kuhusu Israeli, na hakika hawa ni wa kipekee na ndio maana MUNGU hakuwahi kuita MUNGU wa taifa lolote ila ni MUNGU wa Israeli.

Kanisa pia ni uzao wa Ibarahimu wa jinsi ya rohoni na warithi sawa sawa na ahadi (Wagalatia3:7-14.Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. KRISTO alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika YESU KRISTO, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.)

MUNGU wa Israeli awabariki sana na kama hujaokoka ndugu fanya hivyo leo maana hakuna uzima wa milele kwingine nje na BWANA YESU (Yohana 14:6-YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. , PIA Matendo 4:12-Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ), BWANA YESU anakuhitaji ndugu ambae hujampokea maana alikufa mara moja ili wewe uwe hai milele katika yeye. Mpe maisha yako leo.

                                    MUNGU akubariki sana

                   Ni mimi ndugu yako Peter Michael Mabula

                            Maisha ya ushindi Ministry.

                                           0714252292

             HAKUNA ALIYE KAMA MUNGU WA ISRAELI.

                                        Amen.

 
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments