Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu
na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi
kumtumikia Mungu na mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie
maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha
je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa
angani ya kwamba hawapandi wala hawavuni wala hawakusanyi ghalani; na
Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni
yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono
mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba jinsi
yameavyo; hayafanyi kazi wala hayasokoti, nami nawaambia ya kwamba hata
Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.
Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni yaliyopo leo na kesho
hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?
Msisumbuke basi mkisema, Tule nini? Au tunywe nini? Au tuvae nini? Kwa
maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni
anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake na
haki yake; na hayo yote mtazidishiwa (Mathayo 6:24-33).
Comments