NAMNA PASAKA ILIVYO * Sehemu ya mwisho *



Mtumishi Gasper Madumla

SOMO : NAMNA PASAKA ILIVYO * Sehemu ya mwisho *

Haleluya….
Jina la Bwana Yesu lisifiwe…

Ninakukaribisha mpendwa tujifunze pamoja kwa habari ya PASAKA ili tunaposherekea sikukuu hii tujue ni nini tunasherekea.

PASAKA ni kufa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo ndani yetu,na sio katikati yetu,wala pembeni yetu Bali ndani yetu.Ndani yetu ni katika kilindi cha mioyo yetu,kwamba tuanze kukumbuka kifo chake na kufufuka kwake kuanzia huko ndani,

Maana hakuna Yule aliyekufa kisha akafufuka siku ya tatu,
ISIPOKUWA NI MMOJA TU AMBAYE NI YESU KRISTO PEKEE.
PASAKA sio ile ya kutamkwa tu,
PASAKA ndio ukristo wenyewe.
Tunapozungumzia KIFO CHA BWANA YESU tunazungumzia MSAMAHA wa dhambi ulioachiliwa kwetu bure.

Sikia;
Yesu alikuwa sawa sawa na Baba ,pale ilipohitajika wa kumtuma Duniani ili ifanyike upatanisho baina ya Mungu na wanadamu waliokuwa na dhambi,
Tunaona Bwana Yesu akajitoa,akaja Duniani na kuzaliwa chini ya sheria kama mwanadamu wa kawaida ili atukomboe sisi tuliokuwa watu wa dhambi.

Ikiwa ndio hivyo basi ,tutakubaliana kuwa Ipo Neema na Rehema za Mungu ndani ya kifo cha Bwana Yesu,kwa maana Yeye alijitoa kwa wengi waliopotea,ili wapate UKOMBOZI.Tunasoma Luka 19 : 10 “ Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. “

Sikia;
Kilichopotea hapo ni USHIRIKA ( SPIRITUAL CONNECTION/BOND) baina ya Mungu na watu wake baada ya anguko la dhambi ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa.
Na ndio maana baada ya dhambi Mungu anashindwa kumuona Adamu mahali anapotakiwa awe,

Tunasoma ;
Mwanzo 3 :9 :

“ Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? ”
Hapo haimaanishi kwamba Mungu alikuwa hamuoni kabisa,bali alikuwa hamuoni katika Nafasi/position yake anayopaswa kuwa siku zote.

Okey ;
Leo inasikitisha sana kwa viongozi wa dini kuwasisitiza Waamini wao kwamba kuingia katika mfungo na maombi kwa mwezi mmoja tu eti kwamba ni mwezi wa TOBA,!
Je miezi mingine vipi ?
Sio miezi ya TOBA ?
Je inakuwaje basi mtu aishi kidunia miezi hiyo yote,kisha amgeukie Mungu kwa mwezi mmoja tu,?
Je kama akifa kabla ya mwezi huo ,inakuaje ?
.,Mbingu ataiona?
Labda ujiulize maswali hayo.

Hii ni makosa kwa kanisa,Kanisa lazima lifahamu kuwa Hakuna mwezi wa toba bali miezi yote ni miezi ya TOBA,Na ndio maana tunatakiwa KUKUMBUKA MSAMAHA WA DHAMBI ZETU KILA SIKU.
Wayahudi walikuwa na sikukuu ambazo hazikuendelea katika agano jipya,lakini SIKUU YA PASAKA yenyewe yaendelea maana waliambiwa waikumbuke siku ile walipotolewa Misri kwa mkono wa Bwana,

Tunasoma Hesabu 9:2 ;
“ Tena, wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa. ”
Pia Soma Kutoka 12: 14

.Katika agano jipya hatukumbuki utumwa wa Misri bali twakumbuka wokovu tuliopata kupitia BWANA YESU.( 1 Petro 1 : 18-19 )

Haleluya…
Ninampenda huyu Yesu wa Msalaba…
Jina la Bwana liinuliwe…

Wakristo wa leo wameichukua PASAKA kama sikukuu ya kula pilau na kufanya mambo yasiyokuwa hata na maana,
Bali mimi ninakuambia kuwa kwa habari ya PASAKA,kama ukiitafakari vizuri waweza kulia machozi ukikumbuka namna ulivyokuwa Mzinzi/Mwizi/Muabudu sanamu/Mtu wa mapokeo ya dini/Mlevi/Tapeli N.K.

Lakini sasa eti wewe ni mpendwa wa Bwana au wengine ni watumishi.Katika kiwango hicho tu yafaa umpe MUNGU Utukufu.

KUFA NA KUKUFUFUKA KWA BWANA YESU.

Wewe mpendwa ni lazima utambue kuwa BWANA MUNGU anakupenda sana kuliko unavyompenda .Na ndio maana akakubali kufanywa laana pale msalabani kwa ajili yangu na yako.

Tunasoma Galatia 3 : 13 :
“ Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa ALIFANYWA LAANA KWA AJILI YETU; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;”

Ili Yesu amwage damu yake alihitaji mwili,hivyo akauacha Uungu wake akawa sawa na mwanadamu ila hakutenda dhambi.
“ bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;
tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ”Wafilipi 2 :7-9

Biblia inasema tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, “alijinyenyekeza akawa mtii ”
Tazama hapo ndipo akakirimiwa jina la Yesu,kwa maana nyingine ni kwamba jina la Yesu latokana na UTII.

Hivyo ikiwa Bwana Yesu atafufuka ndani yako siku ya leo ,kitachofufuka ndani yako ni UTII,maana Yeye ni MTII.

Okey ;
Nilikuambia kuwa :
Waisraeli ,kilichowafanya wasipatwe na madhara ya kufiwa kwa wazaliwa wao wa kwanza ilikuwa ni DAMU iliyopakwa kwenye nyumba zao,Hivyo DAMU ilikuwa kielelezo cha utetezi wao kutopatwa na pigo lolote.Kwa maana hiyo DAMU isingelikuwapo labda katika moja ya nyumba ya muisraeli,Basi ni dhahili angelipata na pigo.

Tazama sasa katika PASAKA wetu KRISTO,ameachilia DAMU yake iwe ULINZI wa kutopigwa na pigo lolote lile kutoka kwa adui.Yeye aliyekuwa ndani ya Kristo hawezi kupatwa na pigo lolote lile lijapokuja,

Tunasoma Hesabu 23 : 23:

“ Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! ”

Hivyo PASAKA namna ilivyo sasa ni tofauti na jinsi anavyotakiwa iwe,Mungu anatutizamia kwamba tukumbuke wema na fadhili zake pamoja na upendo wake wa kututoa sehemu chafu ya dhambi na kutuleta katika msamaha wa pendo lake

.Wakolosai 1 : 13-14 :
“ Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; ”

Ili Bwana Yesu afufuke ndani yako ni lazima umkubari awe Bwana na Mwokozi wako kwa kinywa chako mwenyewe.Sasa na ukiwa kama bado hujampokea Bwana Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wa maisha yako ,basi wakati ndio huu ili Bwana Yesu afufuke na wewe siku ya leo,waweza kufuatisha sala hii;

Sema,
Bwana Yesu Kristo,mimi ni mwenye dhambi ninakiri kwa kinywa changu ,ninaomba unisamehe makosa yangu yote,ninayoyakumbuka na nisiyoyakumbuka,ninayoyajua na nisiyoyajua,unifute jina langu katika kitabu cha hukumu,na uandike jina langu katika kitabu cha uzima.
Ongera kwa kuokoka,na Bwana Yesu sasa atafufuka na wewe mpendwa.

MWISHO.
UBARIKIWE.

Comments