UJASIRI WA MKRISTO


shalomu mpendwa
karibu katika somo hili muhimu kwa watu wa MUNGU kuhusu UJASIRI na Biblia inasema ‘’Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.’’Mithali 28:1

Watu wengi wameshindwa kufanya mambo fulani mazuri na mema  kwa kukosa ujasiri.
Kama mkristo nakuomba ufahamu kwamba hakuna ushindi bila mapambano na hauwezi kuwa jemedari bila vita.
Katika waebrania 10:35 Biblia inasema ‘’Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu.’’
Ndugu ni jambo la muhimu kutambua kuwa ujasiri wetu kama watu wa MUNGU una thamani kubwa mbele za MUNGU na MUNGU atajivunia wewe ambaye unamcha yeye na ukienenda kwa utakatifu huku ukimkriri KRISTO kwa kila hali na kila mazingira maana hatukupewa roho ya woga bali roho ya nguvu na pia hatupigani vita vya kimwili bali vita ya kiroho na vita hiyo ya kiroho inafanyika katika ulimwengu wa kiroho na kwa sababu tuna mamlaka ya KRISTO ndani yetu ushindi ni lazima. Maana  BWANA YESU ambaye ni mshindi siku zote huachilia ushindi huo kwa kila aliyempa yeye maisha yake na kukubali kuenenda katika kweli ya MUNGU ambayo ni neno la MUNGU.
Mtu mwenye ujasiri ana thawabu na hufanikiwa na kumbuka kuwa tangu mwanzo hadi ufunuo MUNGU alikua akiambatana na watu wasio waoga bali wajasiri na walioweka tumaini lao kwake na usije ukasahau kwamba tangu kitabu cha Mwanzo hadi kitabu cha ufunuo kwenye BIBLIA, MUNGU hakuambatana na watu/watumishi waoga bali wajasiri na hata waliokua waoga MUNGU aliwataka kuwa mashujaa, hodari na wajasiri mfano Yoshua katika Yoshua 1:6-7 ‘’Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.’’
Yapo mambo mengi hayatatendeka kwako mpaka utakapokua  na UJASIRI.

                   CHANZO CHA UJASIRI

1.Ujasiri wa kipepo/mapepo:
Kuna vyanzo vingi vya ujasiri na hata ujasiri wa shetani upo mfano makahaba wanaojiuza wanakuwa na ujasiri wa kuwaendea wateja wao, ni ujasiri lakini ni machukizo makuu kwa MUNGU na watu wa jinsi hiyo wanamhitaji YESU ili wapone na kufunguliwa kutoka kwenye ujasiri huo wa kishetani/majini na kuwa watu wapya waliosafishwa kwa damu ya YESU na wataupata ujasiri wa kumungu wa kuweza hata kuwasaidia watu wengine waijue kweli ili hiyo kweli iwaweke huru mbali na tabia za kishetani.
Watu wengi wameahirisha mambo yao mema  kwa kukosa ujasiri.

2.Ujasiri wa kimungu;
upo ujasiri wa kimungu au ujasiri wa wenye haki. Mithali 4:12 ‘’
Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu.’’

Ndugu  chanzo cha ujasiri cha watu wa MUNGU sio hadi uwe na elimu bali ROHO MTAKATIFU ndiye utoshelevu wetu.’’
Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA.’’- Isaya 55:8.

                   JE UNAPATAJE UJASIRI

A.  Kumjua YESU.

B.  Kuwa na ROHO MTAKATIFU.

C.  Ufahamu wa neno la MUNGU na maarifa.

D.  Kuvaa silaha zote za MUNGU.

E.  Kuwa maisha ya haki.

F.  Kuishi katika agano na MUNGU.


MUNGU akubariki sana na songa mbele na BWANA YESU hadi uzima wa milele.
Ni mimi ndugu yako Peter Michael Mabula.



Comments

Unknown said…
mungu akubaliki sana mtumishi wa mungu nimelipenda sana somo lako..mungu aendelee kukutumia kwa viwango visivyo vya kawaida..