MAONO NA NDOTO * sehemu ya tano *

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla
Bwana Yesu asifiwe...
Haleluya...

Tunasoma;
" Itakuwa siku za mwisho,asema Mungu,nitawamwagia watu wote Roho yangu,na wana wenu na binti zenu watatabiri;na vijana wenu wataona maono;na wazee wenu wataota ndoto." Matendo 2:17

Haleluya....
Jina la Bwana libarikiwe....

Andiko tulilolisoma hapo juu,ndilo andiko letu la kusimamia fundisho letu zuri. Kupitia andiko hilo,tulijifunza kuhusu KUTABIRI kwa mujibu wa maandiko matakatifu na tukaangalia mifano ya watu waliopata kutabiri,kisha tukajifunza kuhusu MAONO.
Leo ni siku ya tano tukijifunza juu ya MAONO.Tulijifunza kuhusu maono kama ishara ya picha halisi juu ya tukio lijalo lenye kuonekana katika ulimwengu wa kiroho,tukaenda kiundani sana kuangalia na aina za maono,pamoja na mifano yake( Fuatilia sehemu zilizopita)
Leo tunajifunza kuhusu maono kwa mtizamo mwingine.
Kumbuka;
Nilikuwaambia kwamba,kila mwanadamu chini ya jua ameumbwa kwa maana na kusudi maalumu la Mungu mwenyewe. Nikakuambia ya kwamba,hakuna mwanadamu aliyeumbwa kwa bahati mbaya.

Haijalishi wewe ni mkristo au si mkristo lakini ujue ya kwamba hukuumbwa kwa bahati mbaya.Mungu anakuhitaji akuokoe kwa wokovu ulio mkuu kupitia jina la Yesu Kristo wa Nazareti.
Hivyo basi kama hukuumbwa kwa bahati mbaya ,basi uliumbwa kwa bahati nzuri ya kuyafanya mapenzi ya Baba wa mbinguni.

Ikiwa ni hivyo basi,
Tafsiri nyingine ya MAONO ni ipi?

MAONO ni ufumbuzi wa kusudi la Mungu na mpango wa Mungu ndani ya maisha yako.
Haleluya...
Nasema MAONO ni ufumbuzi wa mpango na malengo ya Mungu ndani ya maisha yako,
Au,
Kwa lugha nyingine mmoja anaweza sema MAONO ni Kusudi la ki-Mungu uliloumbiwa. Yaani ni kwa nini uliumbwa mwanadamu,ile sababu iliyokufanya uumbwe hivyo ulivyo wewe mwanadamu,sababu hiyo ndio inaitwa MAONO.

Bwana Yesu asifiwe...
Kama ningekuwa nakufundisha kwa lugha ya kiingereza ningekuambia;
VISION is the discovery of divine purpose and plan in your life.

Dhumuni kubwa la kuumbwa mwanadamu ni kumuakilisha BWANA MUNGU hapa duniani. Katika kumuakilisha BWANA MUNGU hapa chini ya jua,ndio namna ya kuyafanya mapenzi yake katika DHUMUNI na LENGO fulani la Mungu mwenyewe.
Hilo dhumuni na lengo fulani lililofichika ndilo huitwa MAONO au VISION.
Mfano;
BWANA MUNGU anataburisha dhumuni la kumuumba Yeremia akisema;

" Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua,na kabla hujatoka tumboni,nalikutakasa;nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. " Yeremia 1:5
Bwana Mungu anaelezea dhumuni na lengo kamili la kuumbwa kwa Yeremia,kwamba Yeremia aliumbwa ili awe nabii wa mataifa.
Lile dhumuni la kutengwa kwa Yeremia,awe nabii ndio MAONO.
Maono hayo yalikuwa katika hali ya kufichika,kwamba hakuna mwanadamu mwenye kuyajua hayo,isipokuwa ni Mungu pekee ndiye aliyekuwa akijua MAONO ya kuumbwa kwa Yeremia.

Haleluya...
Hata wewe,kabla hujaumbwa katika tumbo la mama yako,BWANA alikujua,alikutakasa,na alikutenga kuwa mtu fulani katika kazi yake Mungu hapa chini ya jua. Hiyo " kazi fulani ya Mungu hapa chini ya jua uliyoumbiwa..." Ndio hujulikana kama MAONO.
Mungu alikujua kabla hujaumbwa tumboni,na pia alikutakasa,na zaidi ya yote ulitengwa kwa kazi ya Bwana.
Ngoja nikupe mfano mwingine hapo;
BWANA MUNGU anatambulisha pia dhumuni la kumuumba Yohana mbatizaji.

Tunasoma;
" Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana;hatakunywa divai wala kileo;naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao."Luka 1: 15-16

Bwana Mungu anazidi kutuelezea dhumuni na lengo la kumuumba Yohana mbatizaji. Anasema Yohona alikusudiwa kuwalejeza wengi katika Waisraeli,kuwalejeza kwa Bwana Mungu wao kwa njia ya toba ya ubatizo wa maji.Yohana ndiye aliyepewa kusudi la kutengeneza njia ya Bwana Yesu.
Haleluya..
Maono ni ufumbuzi wa kazi ya ki-Mungu ndani ya maisha ya mtu.
Ngoja niendelee kukupa mifano zaidi kuhusu maono katika mtazamo huu wa pili.
Bwana Mungu anazidi kutueleza kusudi la uumbaji kwa watu wake. Na hapa anatueleza kusudi na lengo maalumu la kumuumba Sauli,

Tunasoma;
" Kesho wakati kama huu,nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini,nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli,naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti;maana nimewaangalia watu wangu,kwa sababu kilio chao kimenifikilia."1 Samweli 9:16.

Maono ya kuumbwa kwa Sauli,yalikuwa ni kuwaokoa wana wa Israeli kutoka katika mikono ya Wafilisti,maana kilio chao kilimfikilia Bwana Mungu.
Sauli hakuwa na maono ya ubatizaji,Bali maono ya kuwaokoa Waisraeli kutoka kwa Wafilisti.
Alikadhalika tunaona dhumuni na kusudi la kuumbwa kwa mtume Paulo,Paulo hakuumbwa awe mbashiri wa ndoto,Bali aliumbwa ili awe mtume wa mataifa.Kuwa mtume wa mataifa ni maono ambayo yalikuwa ndani ya Paulo hata kama hapo awali alikuwa ni muuaji,lakini Bwana Mungu alikwisha mtenga awe mtume wa mataifa. (Wagalatia 1:15-16)
Haleluya,.....
Glory to God...

Pia tunaona Maono ya ujio wa Bwana Yesu Kristo chini ya mbingu.Maono ya ujio wa Bwana Yesu Kristo yalikuwa ni kuokoa kile kilichopotea.Kuwaokoa watu na dhambi zao. Pia Yesu Kristo amebeba kusudi la kurejesha ushirika wa Roho mtakatifu,ushirika ule uliopotea pale katika bustani ya Edeni.
*Sasa hayo yote yalikuwa ni MAONO...
ITAENDELEA...
*Usikose fundisho lijalo,tutakapokwenda kuangalia maono yatupasayo kuyapata.
Kwa huduma ya maombi na maombezi,basi usisite kunipigia simu kama wengine wanipigiavyo kwa namba hii;
0655-111149.

UBARIKIWE.

Comments