KURUDISHA KILICHOIBIWA


Resident Pastor ADRIANO MAKAZI, Ufufuo na uzima


Kuna vitu vimeibiwa vingi sana, ni muhimu ugundue shetani anaweza kuiba. Na unapogundua lazma ujiulize aliibajeibaje na wakati wewe upo, ukishagundua unatakiwa uanze mikakati ya kurudisha na sio kulalamika tu. Unachotakiwa ni kujitia nguvu katika Bwana na kuanza kufatilia.

Isaya 42:22‘Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.’ Kwa hiyo kilichokosekana ni wa kusema rudisha, kwa hiyo kurudisha inawezekana ila ni hadi atokee wa kusema rudisha.

Isaya 22:18-19, 18 Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona. 19 Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? Au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani? Naam, kipofu kama mtumishi wa Bwana? 

Hapa wanaongelewa wote waliookoka, si lazma uwe mchungaji ili kuwa mtumishi wa Bwana, hapana kuna majukumu tofauti tofauti. Mfano imeandikwa aliwaita wengine kuwa manabii, mitume nk. hivyo kila mtu ameitwa katika eneo lake. Wengine wameitwa kuwa kinywa cha Bwana, kwamba kila anachotamka kinakuwa! Wengine ni mkono wa BWANA duniani akigusa kimeeleweka. Na hakuna huduma kubwa kuliko nyingine, kama wewe umeitwa kwenye maombi, kazana hapohapo na BWANA atakutokelezea hapohapo. Kila mtu ana enzi yake(wito), kumbuka malaika walioshindwa kuilinda enzi yao waliadhibiwa, Kwa hiyo jitahidi kulinda enzi yako. Kuna wengine watasema mimi mbona sina enzi, ndugu unayo ila umeibiwa na leo tunakwenda kurudisha. Kutokujifahamu kwako hakubadilishi chochote.

Kuna watu leo hii ni vyombo vya BWANA, lakini hawajijui na shetani amewateka na kuwatumia kwa kazi zake, mfano wachawi. Shetani hashughuliki na watu wasio na kitu, anawachukua watu walioandaliwa na Mungu kwa jambo la maana kwa ajili ya ufalme wake (Mungu) na kuwatumia katika kujenga ufalme wake(shetani). Lakini tazama hekima ya Mungu ilivyo kubwa, anamruhusu shetani awatumie watu atakavyo halafu baadae anawaokoa na shetani anageukwa. Kupitia hao watu mbinu za shetani zinafahamika. Na vita inakuwa rahisi mana majeshi ya BWANA yanakuwa yanajua mbinu zake ibilisi.

Mfano Paulo kwa asili alikuwa mtumishi wa Mungu, lakini shetani alimteka akawa anamtumia kuwaua watakatifu wa BWANA, hadi BWANA alipomtokea na kumbadilisha Matendo 9:1-6 ‘1 Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, 
2 akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia … awafunge na kuwaleta Yerusalemu. 
3 Hata alipokuwa akisafiri, ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.
 4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? 
5 Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.
 6 Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda….’

Sauli alivyokutana na BWANA, Yesu akamrudisha kwenye kusudi lake. Na leo kila mmoja atakwenda kurudisha kusudi la BWANA katika maisha yake katika jina la Yesu. Lakini linarudi kwa kupigana, yaani kupigana ni lazma. Ni kwamba hujapigana hujamiliki!

Isaya 42:18, tutoke kwenye upofu, tumebaki kuridhika na hali mbaya tuliyonayo tukiona amani tu! Kumbe tuko vipofu! Hatuoni uhalisia.

Luka 19:41,‘ Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, 42 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. 43 Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; 44 watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.’ Mambo yanaweza kufichwa machoni pako usiyaone, na inakuwa hasara kubwa sana lakini kama ungeona, ungetengeneza. Tunatakiwa tutambue majira ya kujiliwa kwetu. Haya ndio yale majira Yesu anataka kurudisha heshima ya jina lake, majira ambayo Yesu anataka kufanya falme za dunia ziwe zake. Isaya anasema unaona mambo mengi lakini huyatii moyoni, kwanini inakuwa hivyo ndo linapokuja swala la Isaya 42:22 kwamba huyu mtu anakuwa ameibiwa moyo, macho ndo mana anaona lakini hatii moyoni nk.

Kumbuka Samson, alikuwa na nguvu sana za rohoni na mwilini, ndo mana wafilisti walivyomkamata cha kwanza walimtoboa macho kabla ya kumfunga na kumtesa. Hivyo cha kwanza shetani anapokuteka anakutia upofu ili anapokushughulikia wewe unaona amani tu mwisho unadumbukia shimoni.

Akina Daudi walivyorudi na kukuta mji wao umechomwa moto na kila kitu kimeibiwa hadi wakeze. Wanaume wakaanza kulia hadi wakaishiwa nguvu lakini haikuwa suluhisho! Daudi akaona hili jambo suluhisho si kulia bali ni kuingia mbele za BWANA, kutafuta suluhisho, hata wewe ndugu yangu haijalishi una tatizo kiasi gani, wazazi , ndugu , marafiki , bunge na vyote hapa duniani haviwezi kukusaidia, muige Daudi kwa kumwangalia Yesu maana yeye ndiye mwenye funguo za mauti na kuzimu. Daudi akaruhusiwa na BWANA aende na atarudisha vyote ndipo Daudi alipowaongoza wenzie na kwenda na hakika walirudisha vyote.

1Sam 30:1 ‘Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka. ………………. Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka……… Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote. Basi Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye……. Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hata jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia. 18 Daudi akawapokonya wote waliokuwa wamechukuliwa na Waamaleki; naye Daudi akawaokoa wakeze wawili. 19 Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala cho chote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote. ….’ 

Leo tunaenda kulifuatilia jeshi la shetani na kurudisha vyote, kwa msaada wa BWANA itawezekana.2 Samw 22:30 ‘Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. 31 Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia..’.
Yoh 5:28 ‘..msistaajabie maneno haya kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. 29 Nao watatoka; ..’ yaani haijalishi shetani aliwapataje pataje, iwe kiuhalali au vinginevyo, mimi najua neno moja tu ‘NAO WATATOKA’

Isaya 49:24 ‘ Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka? 25 Naam, Bwana asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka;……’

Isaya 14:17 ‘ Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? 17 Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? ’

Efeso 6:10 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 

unapoenda kupigana lazima uvae silaha. Si kila silaha unaweza kuitumia kwa adui yako, lazima ujue yeye ana nini! Sio unaenda na kisu wakati mwenzio ana machine gun, atakushinda tu! Lakini kumbuka vita yetu ni katika ulimwengu wa roho.

Comments