Skip to main content
HISTORIA YA MAISHA YA BAHATI BUKUKU (Sehemu ya 2)
 |
Bahati Bukuku. |
Nilipenda
kwenda shule kusoma, na hii ilikuwa njia mojawapo ya kuepuka kufanya
kazi za nyumbani, hasa kuosha vyombo kitu nilichokuwa nikikichukia mno.
Japokuwa nilikuwa mtoto mdogo lakini mama alijitahidi sana kuniweka
katika mazingira ambayo mtoto wa kike anatakiwa kuwa.
Achukia kuosha vyombo
Kila siku alikuwa akinitaka nioshe vyombo, hii ilikuwa kazi pekee
niliyokuwa nikiichukia mno. Kila nilipokuwa nikirudi nyumbani, mama
alikuwa akinipa maziwa na kiporo cha jana, nikimaliza kula, alikuwa
akiniambia nioshe vyombo nilivyovitumia.
Nilikereka mno lakini sikuwa na jinsi, nilibaki nikilalamikalalamika
lakini mwisho wa siku niliosha vyombo mbele yake huku akionekana kuwa na
furaha.
AWA KIONGOZI WA KUIMBA
Ijulikane kwamba kuimba ni kipaji nilichozaliwa nacho. Nakumbuka kipindi
hicho mimi ndiye nilikuwa kiongozi wa nyimbo mbalimbali tulizokuwa
tukiimba shuleni. Sauti yangu haikuwa nzuri, ilikuwa ni ya kukoroma sana
lakini kila nilipokuwa nikiimba walimu waliipenda na ilikuwa ni lazima
ujue kwamba ‘huyo anayeimba ni Lusako’.
AANZA DARASA LA KWANZA
Baada ya kusoma shule ya chekechea kwa miaka miwili, mwaka 1990
nilitakiwa kwenda kuanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi
Muungano ambayo haikuwa mbali kutoka tulipokuwa tukiishi.
Kama kawaida yangu, siku hiyo niliamka asubuhi sana huku nikiwa na hamu
ya kuanza darasa la kwanza. Moyo wangu haukuweza kusahau, bado
niliendelea kukumbuka miaka miwili iliyopita ambapo nilishindwa
kulishika sikio langu la upande wa kushoto kwa kutumia mkono wangu wa
kulia kwa kuupitisha kichwani.
Kwanza kabla ya yote, hapohapo nyumbani, nikajaribu kulishika sikio
langu, nikafanikiwa.
ACHEKELEA KUJIUNGA NA SHULE YA MSINGI
Naweza kusema kwamba katika mwaka huo, siku hiyo ndiyo nilikuwa na
furaha kupita kawaida. Nilipenda sana shule, kila nilipokuwa nikiwaona
wanafunzi wakipita nyumbani huku wakiwa wamevalia sare zao za shule,
niliona wivu moyoni.
Leo hii na mimi nilitakiwa kwenda kuanza darasa la kwanza! Asubuhi ya
siku hiyo, mama akaniletea sketi na shati huku chini nikivalia soksi za
pundamilia.
Sikuwa na sare za shule hivyo siku hiyo nilivalia nguo za nyumbani ila
miguuni nilikuwa na soksi hizo za pundamilia. Baada ya kutembea kwa
umbali mdogo, nikaelekea shuleni huku nikiongozana na baba, mzee Bukuku.
Watoto waliokuja kuanza shule walikuwa wengi na zoezi lilikuwa lilelile
la miaka yote, kushika sikio lako. Wapo walioshindwa ambao walilia kama
nilivyofanya miaka miwili iliyopita lakini pia walikuwepo wale
waliofaulu na kutakiwa kujiunga na shule hiyo kwa ajili ya kuanza na
elimu ya msingi huku nikiwa nimeandikishwa jina jingine na kuitwa
Bahati.
AANZA MASOMO
Niliipenda masomo, niliipenda shule kwa jinsi majengo yake yalivyokuwa.
Yalipendeza na kuvutia sana. Siku hiyohiyo ambayo baba alikuwa
amenipeleka shuleni hapo, tukaingizwa darasani na kupangwa, siku
iliyofuata, tukaanza masomo huku tukiwa watoto zaidi ya arobaini katika
darasa moja.
Kila mmoja alionekana kuwa na furaha kama nilivyokuwa. Hakukuwa na
utulivu, kila wakati wanafunzi walikuwa wakipiga kelele, nadhani kwa
walimu au kwa watu waliokuwa katika mitaa yenye watoto wengi watakuwa
wanalitambua hili, jinsi watoto wanavyopiga kelele zenye kuleta kero.
AONGOZA KWA UTUNDU
Kati ya wanafunzi wote waliokuwa darasani, mimi ndiye nilionekana kuwa
mtundu. Kwanza sikutulia sehemu moja, nilionekana kama mtu aliyekuwa
akitafuta kitu fulani, muda huu unaweza kuniona hapa na baadaye kuniona
kule.
UTUNDU WAMPA UMONITA
Kutokana na utundu wangu wa muda mfupi, hata mwalimu wa darasa hilo
aitwaye Rugemilila alipoingia darasani, akanichagua niwe ‘monita’ yaani
kiongozi wa darasa lile.
Maisha ya nyumbani yaliendelea kuwa vilevile kwamba kila nilipokuwa
nikirudi na kula chakula, mama alinitaka nioshe vyombo. Bado mama
alinifundisha mambo mengi huku akitamani sana niwe kama wasichana
wengine, nadhani mbele ya maisha yangu aliyaona kwani kwa kile
alichokuwa akikitaka ndicho kimeweza kunisaidia sana kipindi hiki.
AKAMUA NG’OMBE MAZIWA
Kazi zote za nyumbani ambazo alikuwa akizifanya mama, ilikuwa ni lazima
na mimi nizifanye. Siku ambayo sikuwa nikienda shule, ilikuwa ni lazima
nipike japo chai na kufanya usafi nyumbani hapo huku nikisaidiana naye.
Nyumbani kulikuwa na ng’ombe, kila siku, hata kabla ya kwenda shule
ilikuwa ni lazima niamke asubuhi sana, nikamue maziwa na kisha mtu
ambaye alikuwa akihusika kwa ajili ya kwenda kuwachunga akiwatoa zizini
na kwenda nao machungoni.
ACHUNGA NG’OMBE
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu ya kila siku. Siku ambazo sikuwa
nikielekea shuleni, pia nilikuwa nikichukuliwa na kupelekwa machungoni.
Nilichukia kazi nyingine lakini hii ya kuwapeleka ng’ombe machungoni
niliipenda kwa sababu ilinipa nafasi ya kuondoka nyumbani hapo kwenda
kuzurura na ng’ombe hao.
AUZA CHIPSI
Kutokana na utundu niliokuwa nao na ujanja wa hapa na pale, mwalimu
wangu wa darasa akanichagua niuze chipsi zake. Wanafunzi wengi walikuwa
wakiitamani kazi hii kwani walijua fika kwamba mara unapouza na nyingine
kubaki, walimu huwa na kawaida ya kukupa mfuko mmoja ule.
MUNGU akubariki na kama hukusoma sehemu ya kwanza ya ushuhuda huu FUNGUA HAPA

Comments
Nimefurahi kuona nami nilisoma shule ya Msingi ya Muungano ambayo ulisoma na wewe Pia, nabahati njema zaidi, nilipata kusoma na mdogo wako aitwaye Erasto Bukuku.
Mungu akubariki kwa huduma yako ya uimbaji, mana huwa nabarikiwa sana napo sikiliza nyimbo zako.
Nimefurahi kuona nami nilisoma shule ya Msingi ya Muungano ambayo ulisoma na wewe Pia, nabahati njema zaidi, nilipata kusoma na mdogo wako aitwaye Erasto Bukuku.
Mungu akubariki kwa huduma yako ya uimbaji, mana huwa nabarikiwa sana napo sikiliza nyimbo zako.