NGUVU ZAKO HAZIKO KWENYE KUPIGANA

Na Frank Philip


"Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali" (Isaya 30:15).

"Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya" (Kutoka 14:13,14).

Mara nyingi tumekutana na mambo ya kutuchukiza, tumefanyiwa mambo ya hiana na watu wetu wa karibu, tumeumizwa, kuonewa na kunyanyaswa. Hasira zetu zimewaka kama moto wa gesi, na tumetamani KUPIGANA kwa jinsi ya mwilini. Mara nyingine tumetenda kwa kulipiza kisasi, huku tukijifariji kama tumeweza KUWAADHIBU watesi wetu.

Jua neno hili, KISASI ni juu ya Bwana. Mungu anajua kumlipa kila mtu kwa kadri ya matendo yake. Nguvu zako haziko katika KUPIGANA ila "katika kutulia na kutumaini". Unapotumaini, na kumwacha Mungu ashughulike na hali yako, utaona Akitengeneza NJIA PASIPO na NJIA, nawe utapita pa kavu wakati Mungu anashughulika na adui zako nyuma yako, wewe ukisonga mbele.

Laiti tungejua neno hili "akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu" (2 Nyakati 20:15).

Musa akasema " BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya"

Frank Philip.

Comments