TUBUNI KWA MAANA UFALME WA MBINGUNI UMEKARIBIA.


BWANA YESU asifiwe.
Ukifika mwisho wa mwaka huduma au makanisa mbalimbali huwa wanakuwa na kauli mbiu ambayo wataitendea kazi kwa mwaka unaofuata. Ni jambo jema sana na mimi kwa muda kama wiki 2 nilikuwa namuomba BWANA kwamba ''mwaka 2015 ni wa nini?'' BWANA amenijibu kwamba 2015 NI MWAKA WA KUTUBU KWA MAANA UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA(Mathayo 3:2). 

Namshukuru MUNGU kwa hili maana kwa mawazo yangu nilidhani kwamba 2015 uwe mwaka wa kuteka mateka au Mwaka wa kuinuka na kuangaza au uwe mwaka wa kisasi cha BWANA, au mwaka wa baraka na ushindi. Hakika jibu la MUNGU lilikuja tofauti na nilivyowaza. 

Namshukuru MUNGU maana 2015 ni MWAKA WA KUTUBU MAANA UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA.
-Mahubiri yangu sehemu kubwa yatahusu jambo hili aliloniambia ROHO MTAKATIFU yaani watu watubu maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
-Neno hili ndilo Neno la kwanza kutamkwa na BWANA YESU alipoanza huduma yake '' akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa MUNGU umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.-Marko 1:15'', Pia Mathayo 4:17 inasema '' Tokea wakati huo YESU alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. '' Pia neno hilo hilo ndilo lilikuwa la kwanza kusemwa na Yohana mbatizaji alipoanza huduma yake kama mtangulizi wa BWANA YESU Mathayo 3:1-2 inasema '' Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema,Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. ''
Hakika ufalme wa MUNGU umekaribia na hakika umefika maana ufalme wa MUNGU unakuwa umekaribia kwa wale tu ambao hawajampokea YESU KRISTO kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yao, hao wanakuwa wanao ufalme wa MUNGU. Na ufalme wa MUNGU unakuwa umekaribia au uko karibu na kufika kwa wale ambao hawajaokoka hivyo ndio maana injili kama hii inahubiriwa kwao ili wampokee BWANA YESU na kusajiriwa kwenye ufalme wa MUNGU.



KUNA MAMBO 2 KUHUSU UFALME WA MUNGU.


1. MFALME WA UFALME WA MUNGU.
2. JINSI YA KUWA RAIA WA UFALME WA MUNGU.


-Mfalme wa ufalme wa MUNGU ni BWANA YESU, alipewa ufalme na MUNGU BABA. Daniel 7:13-14'' Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo MZEE wa siku, wakamleta karibu naye.Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. '' Na Jambo hilo aliloliona Nabii Danieli linakuja kutimia miaka zaidi ya 400 tangu Danieli aone maono hayo. BWANA YESU aliwaambia neno hilo Mitume wake Mathayo 28:18-20 '' YESU akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU;na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.''
 
-Jinsi ya kuwa raia wa ufalme wa MUNGU ni kumpokea BWANA YESU kama BWANA na mkombozi. Warumi 10:9-11 '' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka.Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. '' Na BWANA YESU mwenywe anasema ''Kwa kuwa mapenzi yake BABA yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. -Yohana 6:40''
Ndugu yangu hakika hii ni neema ya ajabu na huu ni upendo wa ajabu sana wa BWANA YESU maana aliacha enzi yake ili tu kuja kunikomboa mimi na wewe. Mpendwa wangu mpokee BWANA YESU leo na atakuandika jina lako kwenywe kitabu cha uzima.
Nawewe ambaye umeshampokea YESU yeye anasema '' Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. -Mathayo 10:22''
Kwa leo naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292

Comments