KAA KATIKA IMANI YA USHINDI SIKU ZOTE.


Na Mtumishi Peter M Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze imani ya ushindi.
Imani ya ushindi chanzo chake ni kulisikia neno la KRISTO.

Warumi 10:17 ‘’ Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.  ‘’

Imani ya ushindi lazima ije kutokana na neno la KRISTO maana KRISTO ni mshindi na neno lake lina ushindi wa milele. Mara nyingi sana BWANA YESU alisema ‘’Amini amin nakuambia’’ maana yake alichokisema ni kweli na hakuna kweli zaidi ya ile kweli aliyoisema BWANA YESU.

Yeremia 1:8 ‘’ Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema  BWANA . ‘’

Jambo ambalo watu wengi hawajui ni kwamba imani ina macho. Ndio, imani ina macho na inaona. Stephano alipokuwa anapigwa mawe aliona mbinguni na akamuona BWANA YESU akiwa ameketi katika kiti cha uweza. Aliona kwa maono lakini maono hayo yaliambatana na imani. Isingekuwa imani ya ushindi angesema ‘’wananipiga huku macho yangu yananidanganya’’ lakini Macho ya imani yaliona na kusema ‘’Wala usijali maana ukiondoka hapa duniani utaenda paleeeeee juu alipo BWANA wako YESU maana aliahidi anakwenda kukuandalia makao, hivyo makao yako wala sio hapa ila mbinguni’’
Imani iliona.
Ayubu licha ya kuwa katika wakati mgumu sana wa majaribu makuu lakini bado alisema
 ‘’ Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.  Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona MUNGU; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu.    –Ayubu 19:25-27’
-Imani ya Ayubu aliona ushindi mkuu hata kama wakati huo ushindi haukuwepo. Macho ya kawaida ya Ayubu hayakuona kwamba kuna kumuona mtetezi alie hai lakini macho ya imani ya Ayubu yalimuona BWANA  aliye mtetezi aliye hai. Macho ya Imani ya Ayubu yalimuona BWANA akija kumsaidia, kumponya na kumbariki upya na ndivyo ilivyokuja kuwa Biblia inasema
 ‘’  Basi hivyo BWANA akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu.  Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. -  Ayubu 42:12-13 ‘
Imani ya ushindi husema hivi;

=Nitashinda na zaidi ya kushinda kwa YESU anayenishindia, BWANA atanishindia wala hatanyamaza maana ninamuomba na kumuabudu katika kweli yake.

=MUNGU BABA akiwa upande wangu, ni nani aliye juu yangu?
Warumi 8:31 ‘’  1 Basi, tuseme nini juu ya hayo? MUNGU akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?  ‘’ 
-Ni ugonjwa gani uli juu yangu?
- Ni laana gani iliyo juu yangu?
- Ni shida gani iliyo juu yangu?
-Ni mchawi nani aliye juu yangu?
- Ni mganga gani aliye juu yangu?

=Ni nani atakayenishitaki mimi mteule wa MUNGU?
Warumi 8:33  ‘’ Ni nani atakayewashitaki wateule wa MUNGU? MUNGU ndiye mwenye kuwahesabia haki.  ‘’  
-Mimi sitendi dhambi, je maneno ya watu ya uongo yanishitaki na kunishinda? 
-Sina hatia, je chuki za wafanya kazi wenzangu ndizo zinishinde na kunirudisha nyuma? 
-Haiwezekani maana hakuna atakayenishitaki na kuniweza ikiwa MUNGU ndiye aliyesihesabia kuwa sina hatia hata moja.

=Ni nani atakayenihukumia adhabu?
Warumi 8:34 ‘’ Ni nani atakayewahukumia adhabu? KRISTO YESU ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa MUNGU; tena ndiye anayetuombea.  ‘’ 
-Ni mchawi nani akayetumia tunguli zake ili nife wakati Damu ya YESU inanilinda na ninaomba kila siku? 
-Ni nani atakayenitegea jinni njiani ili jinni liniue wakati BWANA YESU ndiye anayenilinda?

=Ni nani atakayenitenga na upendo wa KRISTO?
Warumi 8:35 ‘’ Ni nani atakayetutenga na upendo wa KRISTO? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?   ’’  
-Je kaa njaa kanaweza kuonondoa kwa YESU?
- Je kukusa kazi dada  ndiko kunaweza kukuondoa kwa YESU kwa wewe kuamua kuwa kahaba?
- Je kukosa mchumba ndiko kukuondoe kwa YESU ndugu? 
Hapana, ukiwa na imani ya KRISTO ya ushindi hakuna ambacho kinaweza kukuondoa katika Wokovu wa BWANA YESU.
Ndugu yangu, Imani ya ushindi huwa haishindwi ila lazima ujue jinsi ya kuitumia.
Imani ya ushindi hushindana kiroho na sio kimwili.
-kila jambo chanzo chake ni katika ulimwengu wa roho. Hakuna jambo hata moja ambalo hutokea katika ulimwengu wa mwili bila kwanza kutokea katika ulimwengu wa roho. N ahuko katika ulimwengu war oho ssi MUNGU ametupa kumiliki na kushinda kila jambo ambalo liko upande wa adui.
Warumi 8:37-39 ‘’ Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa MUNGU ulio katika KRISTO YESU BWANA wetu.
  ‘’
-Tunashinda kwa maombi makali kupitia jina la YESU KRISTO.
-Wakati mwingine BWANA hutuonyesha yale yanayopangwa na maadui zetu katika ulimwengu wa roho, BWANA hutuonyesha kwa njia ya ndoto na maono,  hatutakiwi kudharau bali kuwadhibiti maadui zetu huko huko katika ulimwengu wa roho kabla hawajafika katika ulimwengu wa mwili.
Ndugu yangu tumia fomula hii kwa njia ya maombi ili kuharibu maadui zako uliowaona katika ulimwengu wa roho,
Yeremia 1:10‘’ angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.   ‘’
=KUNG’OA
=KUBOMOA
=KUHARIBU
=KUANGAMIZA.

Kisha unajenga ufalme wa MUNGU kwa kutamka ushindi kwako kupitia jina la YESU KRISTO. Panda uzima kama unaumwa, panda Baraka kama Baraka kwa maombi, panda ushindi kupitia jina la YESU KRISTO. Ulipomfukuza adui usipaache wazi bali panga jambo jema, Kama umemung’oa pepo mchafu ndani yako basi panda neno la MUNGU kwa kulisoma sana. Panda uzima.
-Jambo la kujua katika maombi ni kwamba sio kila adui ni wa kubomoa na sio kila adui ni wa kung’oa na sio kila adui ni wa kuharibu na sio kila adui ni wa kuangamiza. Ndio maana ROHO MTAKATIFU hutusaidia katika kuomba itupasavyo, hivyo hakikisha unajazwa nguvu za ROHO MATAKTIFU. Hakika unaishi maisha matakatifu. Na kama jambo umeliona kwenye ndoto lazima MUNGU akupe ufahamu wa kujua. Maana unaweza kumuona mtoto mdogo kwenye ndoto analia, sio ukianza kuomba unang’oa, hata sijui utang’oa nini. Ndio maana ROHO MTAKATIFU ni muhimu sana katika maisha yetu maana mtoto uliyemuona anaweza kuwa ni mtu Fulani mahali Fulani anahitaji maombi yako na msaada wako, umemuona rohoni lakini hakika atakuja katika ulimwengu wa mwili na utamuona. Unaweza kumuona jirani yako anakupiga  na ukajikuta unapambana na jirani huo kiroho na kimwili kumbe kwenye ndoto ile ilikuwa ni taarifa tu kwamba kuna roho za kipepo za kuonea zinakuja na anza kupambana na madhabahu hizo ili zisifike na kuanza kukonea kazini, nyumbani na kokote utakakokuwa. Penda kupambana na roho inayomtumikisha mtu na sio kupambana na mtu huyo, pambana na madhabahu inayomtumia mtu huyo mbaya na sio kupambana nae, pambana na kiti cha enzi alichokalia mtu huyo na sio kupambana nae lakini pia kama utatakiwa kupambana nae basi pambana ila sio kimwili bali kiroho.
Yuda 1:20-23 ‘’ Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU,   jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya BWANA  wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele. Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.   ‘’
-Kaa katika imani ya ushindi, funga na kuomba, omba katika ROHO, Vaa silaha za MUNGU ili uweze kushinda. Silaha za MUNGU ambazo unatakiwa uzivae ni
=Neno la MUNGU.
=Utakatifu.
=Dirii ya haki na n.k.
Waefeso 3:20-21 ‘’ Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;   naam, atukuzwe katika Kanisa na katika KRISTO YESU  hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.  ‘’
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments