KAKOBE AWARUSHIA KOMBORA ZITO NYALANDU, MWIGULU

Stori: Gladyness Mallya 

Katika hali isiyo ya kawaida Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe amefunguka na Injili nzito kwa kuwataja baadhi ya wagombea urais kwamba waingie katika wokovu kamili badala ya kuwa na wokovu aliodai ni wa kuigiza. 
 
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe. 


Katika moja ya mahubiri yake kanisani kwake Mwenge, Sam Nujoma Road, Askofu Kakobe aliwataja wagombea urais Mwingulu Nchemba na Lazaro Nyalandu pamoja na mmoja wa mawaziri maarufu, Dk. Harisson Mwakyembe kwamba wanapaswa kuokoka ili mambo yao yawanyokee. “Leo sikwepeshi maneno. Kila mtu anajifanya ameokoka lakini huo ni wokovu ule. Nyalandu (Lazaro), ameokoka kweli? Mwigulu (Nchemba), ameokoka kweli, Mwakyembe (Dk. Harisson) ameokoka? Angalia sasa kwa viwango hivi ndiyo utajua umeokoka au namna gani. 
 
Lazaro Nyalandu. 

“Mimi hapa sitafuti mtu, waziri ukija hapa, rais ukija hapa utanisaidia nini, rais huwezi kunipa hela mimi….mimi ndiyo naweza kumpa hela…sihitaji hela ya mwanasiasa, ninachohitaji watu waingie katika wokovu wa kweli,” alisema Askofu Kakobe. Nyalandu aliwahi kuonekana katika kanisa linaloongozwa na Nabii Josephat Mwingira Kibaha ambako aliwaomba waumini kumuunga mkono katika harakati zake za urais na Dk. Mwakyembe aliwahi kuonekana katika Kanisa la Askofu Josephat Ngwajima. Hata hivyo, Mwigulu naye kwa mujibu wa Askofu Kakobe, amekuwa akijitangaza kwamba ameokoka, wokovu ambao kiongozi huyo haridhiki nao.Hakuna kiongozi yeyote kati yao aliyepatikana juzi kuzungumzia wito huo wa Askofu Kakobe

Comments