TUMIA SILAHA ZA MUNGU ILI USHINDE.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Kila mmoja anajua kazi ya silaha.
Kama una silaha kali ni ngumu sana adui kukushinda.
Ukiwa na silaha kali maadui zako watakuogopa sana. Hiyo ni kimwili lakini kiroho ni zaidi.
Silaha za rohoni ndizo zenye nguvu kuliko silaha zote za kimwili.
Silaha za rohoni ziko za aina 2.
Kuna silaha za giza na silaha za nuru.
Silaha za giza hutumiwa na waganga wa kienyeji, wachawi, majini na mizimu.
Silaha za nuru ndizo zenye nguvu isiyoweza kushindwa kamwe.
Silaha za Nuru ndizo silaha za MUNGU kwetu.

Waefeso 6:11-12 ''Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. '' 

Ziko Silaha nyingi za MUNGU lakini leo nakuletea silaha hizi muhimu sana ambazo kwa hizo utamshinda shetani siku zote.

Silaha za MUNGU ambazo kwa hizo utamshinda shetani;

1. NENO LA MUNGU.

Waebrania 4:12 ''Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.'' 
=Neno la MUNGU li hai na lina nguvu sana.
Litumie Neno la MUNGU kwa kulitamka ukiwa kinyume na adui zako. Litumie Neno la MUNGU katika maombi.
Kama kuna kitu shetani anakiogopa basi ni Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU ni moto ulao, kupitia maombi tumia Neno la MUNGU huku ukiwa kinyume na kila kazi ya shetani maishani mwako.
Mfano ni kama huu; inawezekana unaumwa na kuna watu wanasema utakufa muda sio mrefu. Kwa imani unaweza ukaomba ukisema '' Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya BWANA.-Zaburi 118:17''   
=hakika utapona kama umezingatia silaha hizo saba.

=Jiambatanishe na neno siku zote ukiomba kwa imani, Kumbuka kwamba BWANA YESU siku zote analiangalia Neno lake ili alitimize.
Yeremia 1:12 '' Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.''
= Ndugu, je unalo Neno la MUNGU?
Kuna baadhi ya watu wamekariri maandiko machache ya Biblia lakini wakiomba kupitia maandiko hayo hawapokei kwa sababu ya maisha yao ya dhambi au kwa sababu ya imani ndogo au kwa sababu ya tamaa za dunia ambazo sio nzuri.
Ni muhimu sana kutumia Neno lakini tumia Neno la MUNGU ukiwa katika maisha matakatifu na sio dhambi wala dhuluma.


 2. UTAKATIFU.
Waebrania 12:14 ''Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;''
=Pointi ni kwamba hakuna Mwanadamu atakayemuona MUNGU asipokuwa mtakatifu.
Kumuona MUNGU hapa ina maana mbili.
Maana ya kwanza ni kumuona MUNGU baada ya kushinda ya dunia lakini kama uliokoka na kuishi maisha matakatifu.
Kumbe sifa za kukuwezesha kuingia mbinguni ni utakatifu katika KRISTO YESU.
Maana ya pili ya kumuona MUNGU ni kumuona katika Miujiza au matendo  makuuu aliyokutendea.
Muujiza ni kupokea jambo ambalo lilikuwa nje ya uwezo wa mwanadamu wa kawaida, lakini kumbe kumuona huko Tunamuona MUNGU kama tukiwa watakatifu.
Ndio maana Biblia imesema Bila utakatifu hatuwezi kumuona MUNGU. Kumbe utakatifu ni Silaha muhimu sana na kutufanya tumshinde shetani na wapambe wake.
Warumi 13:12 '' Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.''

3. IMANI.

Mathayo  17:20 ''YESU akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.'' 
=Mkiwa na imani mtauambia mlima ''ondoka hapa'' utaondoka.
Kumbe Imani ni silaha kubwa sana maana ukiwa na imani unaweza ukayaambia magonjwa yako ''Ondoka hapa'' nayo yataondoka.
Ukiwa na imani unaweza kusema '' ondoka matatizo kwenye ndoa yangu'' nayo yataondoka.
Milima iliyosemwa na BWANA YESU ni kila kitu ambacho kwako kimegeuka milima hata huwezi tena kuikabili, lakini kwa imani kupitia maombi huku ukiambatanisha na silaha zote saba ninazoelezea leo hakika utashinda.
Marko 9:23 ''YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.''


4. ROHO MTAKATIFU.

Zakaria 4:6 '' Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la BWANA kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa ROHO yangu, asema BWANA wa majeshi.''
=ROHO MTAKATIFU ndiye muhimu zaidi kwa kila Mkristo baada ya kuokoka.
ROHO MTAKATIFU ana kazi zaidi ya 10 kwa Mkristo.
ROHO anajua yote yajayo mbele yako hivyo ukimuomba anaweza akakuepusha katika yale ambayo hukudhani kama ungepona.
Kama anaweza kukuepusha na mabaya basi huyo ni silaha kuliko silaha zote.
Si kwa uweza wa kibinadamu bali ni kwa ROHO MTAKATIFU kama tunataka kushinda tutashinda.
ROHO MTAKATIFU ni silaha tena zaidi ya silaha maana tukiwa na yeye hakuna jambo tutashindwa kulijua, hakuna mipango ya adui ambayo hatutaijua, bali kila kitu kitakuwa wazi.
Mwanzo 41:38b '' Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye ROHO ya MUNGU ndani yake?'' 
 
5. DAMU YA  YESU KRISTO.

Ufunuo 12:11 ''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.''
=Kumbe tunamshinda shetani kwa damu ya mwanakondoo YESU KRISTO aliye hai.
Damu ya YESU ina kazi saba kwa mkristo.
Damu ya YESU ni silaha kali na ambayo iko juu ya silaha zote za kibinadamu.
Ita damu ya YESU iwe ulinzi katika maisha yako, familia yako, kazi yako, ndoa yako na katika kila jambo lako.
Damu ya YESU adui hata kuiangalia tu hawezi maana ni silaha hatari sana.
Yohana 6:53-54 ''Basi YESU akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.''

6. JINA LA YESU KRISTO.

Mithali 18:10 ''Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.''
=Jina la YESU ndio mwisho wa reli naweza kusema hivyo.
Jina la YESU ni silaha inayoweza kufanya kazi maelfu.
Hakuna silaha kushinda jina la YESU.
=BWANA YESU mwenyewe anasema, 
Yohana 14:14 ''Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.'' 
Mwombaji yeyote hakuna jinsi anaweza akajitenga na jina la YESU kama anataka kujibiwa maombi yake.
Jina la YESU ni kama muhuri wa kuidhinisha maombi hata yakajibiwa.
1 Petro 4:16 '' Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze MUNGU katika jina hilo(YESU KRISTO).''
 
7. Maombi.

Mathayo 17:21 ''Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.''
=Kusali ndio kuomba kwenyewe.
Maombi ni maisha tena maombi ndio mkono mrefu zaidi wa kupokea kutoka kwa BWANA.
Kuna aina nyingi za maombi maana maombi ni muhimu sana.
Kuna maombi ya kufunga, kuna maombi ya kusihi, kuna maombi ya kuombeleza, kuna maombi ya vita, kuna maombi ya mapatano n.k.
 1 Thesalonike 5:17 ''ombeni bila kukoma;'' 
=Kuomba ni silaha ya kukufanya ushinde kila siku.
Maombi ni ufunguo wa kupokea.
 Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''
=Ndugu yangu katika BWAMA nakuomba utumie silaha hizi siku zote na utamshinda shetani siku zote.


Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments