FAIDA TANO(5) ZA MAOMBI KWA MUOMBAJI

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU.
Leo nazungumzia maombi.
Maombi ni muhimu sana na ni lazima kwa kila Mkristo aliyeokoka.
Maombi unayoomba leo yanaweza kuwa jambo la kumkumbusha MUNGU katika hitaji lako la kesho.

 1 Thesalonike 5:17 ''ombeni bila kukoma;''

Ni muhimu sana kuwa muombaji na sio kutegemea tu kuombewa.

Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu''

Nakusihi ndugu kuhakikisha unakuwa mwana maombi na husika na maombi kila siku.

1 Yohana 5:14-15 ''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.''

-Tenga Muda wako katika kumtafuta MUNGU kwa maombi.
-Usikubali kukosa muda wa kuomba.
-Usikubali kuwa mtu wa kuombewa tu bali jifunze kuomba na jiunge na kundi la maombi kanisani.

Kuna faida nyingi za matokeo ya kumtafuta MUNGU kwa maombi, chache katika hizo ni;

   1.  Mabaya hayatakupata wewe.

Zaburi91:10 ''Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.''

-Mabaya ya shetani huzuiliwa kwa maombi. Kama wewe ni mwombaji hakika mabaya utayashinda lakini kama wewe sio muombaji hakika kuna makombora ya shetani yakirushwa kwako yatakupata maana huombi.
Ni muhimu sana kuwa muombaji na katika maombi yako ongeza na imani na katika imani ongeza na utakatifu pamoja na kulitii Neno la MUNGU.
 
   2.  Utashinda katika majaribu.


Zaburi 50:15 ''Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.''

-Maombi ni kumwita MUNGU.
-Kama hupendi kumwita MUNGU ujue kuna mateso ya shetani yatakutesa na hakuna msaada maana msaada pekee ni kwa BWANA YESU na wewe  huna muda wa kumwita.
-Ukimwita MUNGU kwenye hitaji lako yeye atakujibu na wewe utamtukuza, lakini kama wewe hupendi kuomba hakika hutajibiwa.
-Kumwita MUNGU kupitia maombi yako ni faida kwako maana BWANA atajibu maombi yako.

   3.  Macho yako ya kiroho yatakuwa yanaona.


Yeremia 33:3 ''Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.''

-Mambo magumu ambayo utayaona  baada ya maombi au baada ya wewe kuwa muombaji ni pamoja na kuona rohoni.
-Kuna vitu kabla havijatokea  waombaji huviona na kuomba ili kama ni kusudi la giza liondoke kupitia maombi yao.
-Kila mtu ana macho ya rohoni lakini mtu akiwa mbali na MUNGU macho yake ya rohoni huziba hata haoni, lakini ukiwa muombaji mzuri basi macho yako ya rohoni yatatiwa nuru ya KRISTO hata utakuwa unaona rohoni.
Faida mojawapo ya maombi ni kukufanya macho yako ya rohoni yaone vizuri vitu vya rohoni.

   4.  Utapokea hitaji lako.


Mathayo 7:7-8 ''Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.''

-Kila aombaye hupokea kutoka kwa MUNGU, Kama huombi maana yake kuna vitu hutapokea.
-Faida mojawapo ya maombi  ni kupokea hitaji lako.
Ni muhimu sana kuwa muombaji maana maombi ni silaha nzuri ya kumshinda adui yako hata upokee baraka yako uitakayo kutoka kwa MUNGU.

   5.  Utamuona MUNGU katika matendo makuu kwako.


Yeremia 29:13 ''Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.''

-Kumtafuta MUNGU kwa bidii ni pamoja na kuomba kwa bidii.
-Kumtafuta MUNGU kwa bidii ni kutenda yale ayatakayo yeye.
-Kumtafuta MUNGU kwa bidii ni kuishi maisha mataktifu pamoja na kuomba kwa imani ili upokee hitaji lako.
-Maombi yana faida kubwa kwa muombaji na faida mojawapo kubwa ni kutendewa matendo makuu na MUNGU.
Inawezekana mtu anaumwa sana na madaktari wameshindwa kumponya lakini kwa maombi BWANA YESU anamponya mtu huyo na kumweka huru mbali na magonjwa, hiyo ni faida mojawapo tu ya maombi katika zile faida nyingi sana.
-maombi ni mkono mrefu wa kupokea kutoka kwa MUNGU hivyo utumie mkono huo ili upokee baraka zako za rohoni na mwilini.

3 Yohana 1:2 ''Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo. ''


Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments