VITA YA KIROHO ITAKUFANYA UMILIKI BARAKA ZAKO.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU asifiwe.
Mithali 18:10 ''Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. ''
Inawezekana kabisa unatamani kupigana vita ya Kiroho ili ushinde.
Vita ya kiroho hupiganwa kiroho kupitia maombi yako.

Inawezekana kabisa unajua kwamba mizimu ya mababu ndio inayokusimamisha wewe katika kuifikia baraka yako kutoka kwa MUNGU.
Inawezekana kabisa kila ukipata pesa nyingi ndio wakati huo huo magonjwa yanavamia familia yako au ukoo hivyo pesa yako yote inaishia kwenye kutibu magonjwa.

Waefeso 6:11 ''Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.''

Mara nyingine inawezekana kabisa umepigana vita ya kiroho bila kushinda. Unaweza kutokushinda kwa sababu tu kuna kitu umekosea katika maombi yako.

Muombaji yeyote ni muhimu
Mimi nataka nikusaidie katika vitu vifuatavyo.
Ili upigane vita ya kuleta ushindi kupitia maombi yako ni muhimu sana kujua yafuatayo;

 1.  Mtambue kwanza adui yako.

Waefeso 6:12 '' Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''
-Adui zetu wako katika ulimwengu wa roho wa giza na sio katika ulimwengu wa mwili.
Tuna maadui hawa;
-Falme za giza.
-Mamlaka za kishetani.
-Wakuu wa giza
-Majeshi ya pepo wabaya .
Inawezekana kabisa ndoa yako ina matatizo makubwa sana kwa sababu tu ya majeshi ya pepo wabaya yaliyomvamia mwezi wako wa ndoa. Sula muhimu ni kumjua tu adui huyo ni yupi ili uite damu ya YESU umharibu na kumshinda adui huyo kupitia maombi yako.
-Kuna watu huomba tu wakiharibu nguvu za giza lakini hata siku moja hawajawahi kuzitaja hizo nguvu za giza ni zipi.
-Kama unapambana na wachawi wataje na hakikisha unawashinda kwa jina la YESU KRISTO.
-Kama unapambana na mizimu itaje na omba kwa juhudi ili ushinde.


 2.  Tambua uwezo halisi wa adui yako.
 Yakobo 4:7 ''
Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''
Adui yetu ni shetani na ana nguvu lakini taarifa ni kwamba tukimpinga na kumharibu kwa jina la YESU anaharibika.
Katika vita yako ni muhimu kutambua uwezo wa adui yako.
Kama unapambana na falme au mamlaka kubwa inabidi uombe maombi makubwa vilevile, na maombi makubwa zaidi ni maombi ya kufunga. hivyo ni muhimu kufunga na kuomba kwa juhudi.

Kama umeombea jambo na halijatoka basi tambua kwamba hujampiga huyo adui aliye nyuma ya jambo hilo. sasa ili umshinde funga au ongeza maombi, au waone watumishi wenye nguvu ya MUNGU zaidi yako wakuombee.

 3.  Tambua mbinu za adui yako.

2 Kor 2:11 '' Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.''
-Mbinu za shetani ziko wazi sana kama wewe ni muombaji.
Kupitia maombi utanoa macho yako ya rohoni ili yaone kila hila za adui dhidi yako hivyo utaomba kwa uhakika maana utakuwa unajua unapambana na nani na yuko wapi.
-Inawezekana kabisa unazijua mbinu za adui yako kwamba hutaka kukuungiza kwenye dhambi ndipo akushinde.
Wengi leo wanaweza kuombea mambo mbalimbali lakini adui halisi wakawa hawajamgusa. adui anaweza kuwa maagano ya kwenye ardhi au adui yako anaweza kukuathiri kupitia mawazo yako hivyo ni muhimu sana kujua mbinu za adui yako ndipo utaweza kumshinda kirahisi. 

inawezekana kabisa shetani hukutesa kwa sababu ya wewe kutokmtolea MUNGU hivyo jitahidi sana kujua mbinu ya adui ili umshinde.


 4.  Fahamu unapigana vita ya namna gani.

Siku zote ni muhimu sana kila mtu kujua kwamba vita ya kiroho hupiganwa rohoni.
Kwenye vita hiyo ni lazima ujue kwamba ili ushinde vita unatakiwa uwe upange wa BWANA ndipo utashinda. Ili uwe upande wa MUNGU kwanza ni lazima uokoke na kisha ni lazima uongozwe na ROHO wa MUNGU. Ukishakubali kuongozwa na ROHO wa MUNGU basi hakika utajua Neno hili kwamba  ''.....   BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya MUNGU.2 Nyakati 20:15 ''

Kuna vita nyingine ya kiroho inabidi ubadili mfumo wa maombi ndipo utashinda.
unaweza kupambana sana na maadui unaowaona lakini kumbe wale unaowaona ni wasaidizi tu wa adui unayetakiwa kupigana naye. Unaweza ukapambana na watu kumbe unatakiwa upambane na kilicho ndani ya watu au kilicho nyuma  ya watu ndipo utashinda.

 5.  Pima silaha zako. je zinauwezo wa kukufanya uanzishe vita?
Kila Mkristo Aliyeokoka anauwezo wa kuanzisha vita ya kiroho na kushinda kama tu ataamua kuzitumia silaha za MUNGU ambazo kwa hizo huja ushindi.

Waefeso 6:13 '' Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.''
Silaha za MUNGU ni;
-Neno la MUNGU.
-Damu ya YESU.
-Jina la YESU.
-Matoleo.
-Matendo mema n.k
Lakini silaha hizo haziwezi kutumika vyema kama wewe muombaji hutaomba kwa imani. Hivyo Imani ni risasi ndani ya silaha ya MUNGU hata kukuwezesha wewe kushinda vita ya kiroho,.


 6.  Pambana vita ya ushindi na sio vita ya kushindwa.

Vita ya ushindi inaanza kwanza kwa wewe mpiganani kuwa mtoto wa MUNGU  na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU huku ukizijua  haki zako.
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
Baada ya kuwa mwana wa MUNGU huku ukiongozwa na ROHO wa MUNGU katika vita ya kiroho ya ushindi unatakiwa uongeze Utakatifu na Imani.
Waebrania 11:6 ''Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.''


 7. Tambua uwezo na Mamlaka iliyo upande wako.

Mteule wa KRISTO siku zote nyuma yake yuko KRISTO kama tu mteule huo anatembea katika utakatifu na imani thabiti.
Kama KRISTO yuko upande wako basi Mamlaka iliyo nyuma yako ni kuu sana.
Mamlaka iliyo nyuma yako ni;
-Jina la YESU KRISTO.
- Damu ya YESU KRISTO.
-ROHO MTAKATIFU.
-BWANA YESU mwenyewe.
-MUNGU BABA 
1 Yohana 5:5 ''Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba YESU ni Mwana wa MUNGU? ''

Na Biblia iko wazi sana ikisema kwamba
 '' Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.-Yohana 4:4''
-Aliye ndani ya watu waliookoka ni MUNGU BABA. MUNGU MWANA na MUNGU ROHO MTAKATIFU.
Hiyo ni mamlaka kuu kuliko zote.
Hiyo ni mamlaka isiyoweza kupinga na yeyote au chochote.
Zaburi 116:1-2 ''Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote. '' 

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.


Comments