AMRI MPYA TUMEPEWA, TUPENDANE.

Na Mtumishi Peter Mabula
BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

'' Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.-Yahana 13:34-35 '' 

 Amri Mpya Tumepewa na BWANA YESU kwamba  "TUPENDANE"
Tumepewa amri mpya wateule kwa KRISTO kwamba tupendane.
Upendo ni silaha nzuri ya kumshinda shetani na hila zake.
Siri mojawapo ya watu kututambua kwamba sisi ni wanafunzi wa kweli wa YESU KRISTO ni pale tutakapokuwa na upendo sisi kwa sisi.
Kama kanisani hakuna upendo hakika mgeni kuja itakuwa ngumu, hata akija ataondoka na kupeleka habari mbaya kuhusu kanisa alilotoka, kwa sababu yeye mwenyewe hana upendo halisi na kanisa alilotoka pia halina upendo.
 Najua kabisa kwamba hizi ni nyakati za mwisho na biblia katika kuzungumzia matukio ya siku za mwisho inasema kwamba Upendo wa wengi utapoa.
Upendo linatakiwa liwe vazi la kudumu la mkristo kama ulivyo wokovu.
MUNGU alitupenda kwanza na kutuamuru na sisi tuwe na upendo sisi kwa sisi.

''Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa MUNGU, na kila apendaye amezaliwa na MUNGU, naye anamjua MUNGU. Yeye asiyependa, hakumjua MUNGU, kwa maana MUNGU ni upendo.-1 Yohana 4:7-8''

-Upendo kwa wateule utarahisisha injili kusonga mbele.
-Upendo kwa wateule utatufanya tuombeane na kuwa salama siku zote. 
-Upendo wa wateule utatufanya tupendwe na MUNGU na tupendwe pia na wanadamu.
Tumepewa amri mpya  kwamba tupendane.
Vikundi vingi kanisani vinadumaa kihuduma kwa sababu kuu mbili ambazo ni dhambi pamoja na kukosa moyo wa upendo.
 Upendo ni wa muhimu sana katika kanisa na katika jumuia yote ya waaminio waliookolewa na BWANA YESU.


Tumepewa amri mpya  kwamba tupendane.
Sio Upendo Wa Kingono, Maana Upendo Wa Kingono Ni Wa shetani
Mithali 22:14 '' Kinywa cha malaya ni shimo refu; Anayechukiwa na BWANA atatumbukia ndani yake.''

Upendo wa kingono huo sio upendo ila ni tamaa tu ya kipepo isiyohitajika kwa watoto wa MUNGU.
Kuna baadhi ya watu ukimwambia tu ''Nakupenda'' mawazo yake yote na akili zake zote zitawaza tu upendo wa kingono kumbe sio.
Wengine pia kwa kutekwa na shetani wamejifanya kuwa na upendo wa kuwatamkia watu wa MUNGU ili wawanase kimahusiano, huo ni ushetani na haufai.
 
 Biblia inakataza upendo wa kingono ikisema 
''Nami nimeona lililo na uchungu kupita mauti; yaani, mwanamke ambaye moyo wake ni mitego na tanzi, na mikono yake ni kama vifungo; yeye ampendezaye MUNGU atamponyoka, bali mwenye dhambi atanaswa na yeye.- Mhubiri 7:26 ''

 Bali Tunatakiwa Tuwe Na Upendo Kama Watoto Wa MUNGU Tuliopendwa.
=Kwanini Wateule tupendane?
-Kwa sababu tunatarajia mbingu moja.
-Kwa sababu MUNGU wetu ni mmoja na alitupenda kwanza sisi kabla sisi hatujampenda yeye.
-Kwa sababu Mwokozi wetu ni mmoja ambaye ni BWANA YESU, Naye alitupenda sisi na kutuchagua kabla sisi hatujampenda.

Yohana 3:16 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.''  

Tunatakiwa Tuwe Na Upendo Kama Warithi Pamoja Katika Ufalme Wa MUNGU Maana Tumeokoka.
Injili inashindwa kupenya katika baadhi ya maeneo kwa sababu  hatuna upendo.

 Warumi 12:9 ''Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.'' 

 Mimi Peter Naamini hivi; Kama Askofu mmoja akimsema vibaya Askofu mwingine basi hapo ni lazima kuna watu zaidi ya 7 watashindwa kuokoka au wataamua kuwa wapagani kwa sababu tu ya maneno ya aaskofu hao.
Kama mchungaji mmoja akijitangaza redioni kwamba pengine pote hakuna MUNGU isipokuwa kanisani kwake basi huyo mchungaji, mimi Peter Naamini kwamba atasababisha zaidi ya watu 100 washindwe kuokoka kwa wakati kwa sababu ya maneno yake. maana kama mtu yuko mkoa mwingine kisha amesikia mchungaji wa mkoa mwingine akisema kwamba MUNGU wa kweli yuko kanisani kwake tu basi hakika shetani atamhubiri huyo ndugu kwamba hakuna haja ya kuokoka maana hatakama akitaka kuokoka basi inabidi ahamie mkoa wa yule mchungaji ndipo ataokoka maana ameaminishwa kwamba kwingine hakuna MUNGU wa kweli isipokuwa kanisani kwa mchungaji huyo tu.

Tumepewa amri mpya  kwamba tupendane.
Ni Upendo Wa Kuziepuka Tamaa Za Mwili

1 Petro 2:11 ''Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.'' 

Hatutakiwi Kuwa Na Upendo Wa Kujipendelea, Wala Hatutakiwi Tuwe Na Upendo Wa Kuwaona Wengine Wakitenda Dhambi Harafu Sisi Tunacheka.
Hatutakiwi Kuwa Na Upendo Kwa Watu Wakiwepo Lakini Wakiondoka Tunawaseng'enya.

 1 Kor 16:14 ''Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo.''

BWANA YESU Alitupenda Na Anatutaka Tupendane Sisi Kwa Sisi

Yohana 15:12-17 '' Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa BABA yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo BABA kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.'' 

Upendo Ni Kuzifuata Amri Za MUNGU na kuzitii.
Amri za MUNGU ni maagizo yote ya MUNGU katika Biblia ambayo kimsingi ni zaidi ya maagizo  Elfu.
Ni rahisi sana kuyashika maagizo yote ya MUNGU kama tu tutaokoka na kuanza kuongozwa na kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.

1 Yohana 1:6-7 ''Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.''

Upendo wa kiMUNGU hutusukuma sisi kufanya kazi ya MUNGU kwa usahihi.
Hata mimi kukuletea Neno la MUNGU kila siku ni matokeo ya kuwapenda watu wote na kuwapenda watu ni kuwahurumia ili wasipotee bali wampokee BWANA YESU KRISTO na kuokoka.

 Wakolosai 3:13-14 '' Mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.''

Sifa Saba(7) za Kanisa lenye upendo ni hizi;

  1.  Kushuhudia watu wasiookoka ili waokoke.
  2.  Viongozi wa kanisa kukemea dhambi hadharani kupitia mahubiri yao.
 3.   Kanisa zima  kumtii KRISTO na Neno lake.
 4.   Kila mmoja kumhesabu mwenzake kuwa ni bora kuliko yeye.
 5.   Kusaidiana kiroho.
 6.   Kuwaombea walio nje ya KRISTO ili waingie ndani ya Wokovu.
 7.  Kumjali mchungaji wao na kumuombea sana.


1 Yohana 4:11 ''Wapenzi ikiwa MUNGU alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.'' 
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments