HAKIKISHA UNAONGOZWA NA NENO LA MUNGU MAANA YA DUNIA YOTE YATAPITA.

Na Mtumishi Peter Mabula
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

1 Yohana 2: 15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''

Dunia itapita na mambo yake yote.
Falsafa Ya Dunia Hii Mwisho Wake Ni Mauti. Hata Kama Mtu Angejijengea Jina Kiasi Gani Duniani Lakini Mwisho Wake Ni Mauti. Hata Kama Mtu Angeitumikia Jamii Sana Na Watu Wote Kumshangilia Mwisho Wake Bado Unabaki Kuwa Ni Kifo. Hakuna Wa Kudumu Duniani. Hata Akina Adamu Walioishi Miaka Zaidi Ya 900 Bado Hawakuwa Wa Kudumu Duniani. 

Mhubiri 3:1-2A '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa ..........''

 Hakikisha unaongozwa na Neno la MUNGU maana Dunia itapita na mambo yake yote.
Ajabu Leo Mwanadamu Japokuwa Anajua Kabisa Kwamba Hawezi Kuishi Miaka 120 Duniani Lakini Walio Wengi Wanaishi Kana Kwamba Hakuna Kuondoka Duniani. 
Kwa Upendo Wa Ajabu Sana MUNGU Muumbaji Wetu Alituletea Biblia Kama Mwongozo Na Kweli Isiyobadilika Ili Wanadamu Waishi Salama Duniani Maana Yake Hata Wakiondoka Wataenda Kuishi Sehemu Salama. 
MUNGU kwa upendo wake mkuu sana akawaletea wanadamu Wokovu ili kila mwanadamu atakayechagua Wokovu  huo asipotee bali aende uzimani.
Wokovu ni mpango wa MUNGU wa kumtafuta mwanadamu ili huyo mwanadamu awe chini yake MUNGU.
Wokovu ni BWANA YESU KRISTO tu, na wokovu huo wanadamu wanaupokea kwa kumpokea BWANA YESU kama BWANA na MWOKOZI wao, kisha wanaanza kuishi maisha matakatifu siku zote.
 
 Warumi 6:23 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA  wetu.''


Watu Walio Wengi Hawapendi Kuongozwa Na Neno La MUNGU Lakini Ukweli Ni Kwamba Kwa Mtu Anayewaza Maisha Ya Milele Ni Lazima Kuitii Biblia. 

 Hakikisha unaongozwa na Neno la MUNGU maana Dunia itapita na mambo yake yote.

 Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''

Biblia Ina Mambo Matatu Tu Makubwa;

  1.  Ukombozi Wa YESU KRISTO.
Zaburi 111:9 ''Amewapelekea watu wake ukombozi, Ameamuru agano lake liwe la milele, Jina lake ni takatifu la kuogopwa.''

-MUNGU ametuletea Ukombozi ambao uko pekee katika Mwanawe YESU KRISTO.
-Ndani ya damu ya YESU KRISTO kuna agano la milele la uzima kwa wanadamu watii.

Waefeso 1:5-7 ''Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya YESU KRISTO, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.  Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. '' 

Jambo kuu kabisa ambalo Biblia inazungumzia ni ukombozi.
Shabaha namba moja ya Biblia Biblia ni ukombozi.
Ukombozi unatokana na MUNGU wenyewe na umeletwa na MUNGU mwenyewe kwa njia ya YESU KRISTO mwanaye wa pekee.

1 Kor 2:5-6 ''Kwa sababu MUNGU ni mmoja, na mpatanishi kati ya MUNGU na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu KRISTO YESU; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.'' 

    2.  Kuishi Maisha Matakatifu Ya Kumcha MUNGU.
1 Petro 1:15 -16 ''bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''

-Maisha matakatifu  ni maisha mema ambayo MUNGU aliyaumba ili kila mwanadamu ayaishi.
Ni uamuzi wa kila mwanadamu kuishi maisha mataktifu lakini haiwezekani kuingia uzima wa milele bila kuwa watakatifu.

1 Petro 2:12 ''Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa.''
 
  3.  Kuishi Kwa Kuenenda na Kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.'

-ROHO MTAKATIFU ni halisi katika maisha ya wateule wanaomhitaji.
Bila ROHO MTAKATIFU hauwezi kushinda dhambi.

Mithali 1:23 ''Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.''

-Hakuna mwenda uzima wa milele hata mmoja asiyemhitaji ROHO MTAKATIFU.
-ROHO MTAKATIFU hutujulisha Neno la MUNGU.
-Ukipenda kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU hakika ROHO atakusaidia katika maisha yako ya Wokovu.
ROHO atakukumbusha, kukuonya, kukusaidia, kukufariji, kukuepusha na mabaya na kukuombea.
Wanaoongozwa na ROHO MTAKATIFU hao ndio wana wa  MUNGU.

Yohana 4:24 ''MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.   ''

=Ni Muhimu Kumpokea YESU KRISTO.
=Ishi Maisha Matakatifu 
=Enenda Kwa ROHO MTAKATIFU.

 Hakikisha unaongozwa na Neno la MUNGU maana Dunia itapita na mambo yake yote.
Kuna watu pia hupotoshwa na watumishi  wanaojiita wa MUNGU kumbe sio. Mtumishi wa MUNGU halisi ni yule anayemtii BWANA YESU na Neno la MUNGU.
Akili za kuambiwa changanya na za kwako.
Sasa watu wengi wameshikilia tu akili za kuambiwa hata kama ni mbaya.
Kuna watu baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari mtumishi akisema " ili upone njoo kanisani kwangu"
Wameacha na wokovu, wameacha na maombi wakitafuta nauli ili wakapewe chumvi ya upako.
Watu wana imani kwa chumvi kuliko MUNGU anayeponya.
Unakuta mtu ameweka tumaini lake kwenye vitu badala ya MUNGU, je MUNGU Na vitu nani ya muhimu?
Ndio maana nasema akili ya kuambiwa changanya na ya kwako.
MTU yuko tayari kutafuta nauli kwa miaka 2 ili aende kuchukua mafuta ya upako Nigeria.
Mafunuo yapo na karama zipo lakini BWANA YESU ni mkuu na muhimu mafunuo yote.



Waebrania 13:8-9 '' YESU KRISTO  ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.   ''


 Hakikisha unaongozwa na Neno la MUNGU maana Dunia itapita na mambo yake yote.

BWANA YESU ni muhumu kuliko chumvi na maji na vitambaa hivyo tumwamini yeye na sio chumvi na maji.
Naamini kwa somo La Leo kuna watu wanapona hakika.



Kuna watu pia  siku hizi huisingizia sana Biblia. 
Hebu ona uongo huu ambao watu hupayuka mbele za watu wengine wakisema eti Biblia inasema.
''MUNGU anasema jisaidie nami nitakusaidia''
''Kunywa kidogo ila usilewe''
''MUNGU ni wa Neema hivyo hawezi kuwaangamiza wanadamu''
''Mariamu hata sasa ni mama wa MUNGU na eti yuko katika kiti cha enzi''
''Eti Mariamu ni mwombezi wetu''
Huo ni uongo tu ambao watu waliojikinai huisingizia kwamba Biblia inasema.

BWANA anasema ''Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.-Mathayo 24:35'' 

Neno la BWANA liko katika Biblia na sio kwenye midomo ya watu waliojikinai.
Ndugu, Hakikisha unaongozwa na Neno la MUNGU maana Dunia itapita na mambo yake yote.
Ndugu zangu naomba tuwe makini na tulitii Neno la MUNGU na sio maneno ya watu wanaoongea kwa kulisingizia neno la MUNGU.
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments