KUMWABUDU MARIAMU NA KUABUDU SANAMU NI MACHUKIZO KWA MUNGU.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze ujumbe huu mfupi ila muhimu sana.

Inawezekana huu ukawa ujumbe ambao wengine hawaupendi lakini naomba niseme kwamba, Hata mimi napenda sana kumfurahisha kila rafiki yangu kupitia masomo yangu na posts zangu mbalimbali lakini MUNGU amenipa ujumbe wa maonyo nifanyeje? 

Je niwatii wanadamu ili waendelee kumwabudu mariam na sanamu au niwaambie ili hata akipona mmoja tu kati yao mimi nitakuwa salama? 

=Mtu kusema anaiheshimu tu sanamu wala haiabudu huo ni uongo wa shetani wa hadharani, Heri heshimu wazazi wako, serikali na watu wote kuliko kuheshimu sanamu.

=Mtu kusema anaiheshimu tu sanamu wala haiabudu hiyo ni lugha laini ya shetani kuwateka watu wa MUNGU.


Ndugu mmoja akaniambia kwamba tangu aanze kwenda kanisani zaidi ya miaka 20 iliyopita hajawahi kusikia viongozi wake wakiyataja maandiko ambayo mimi nimeyataja ya kukataza kumwabudu Mariamu wala sanamu, aliniona mimi nafundisha mambo mageni hadi nilipomtumia maandiko hayo ili ayasome katika Biblia yake hiyo hiyo ndipo alipokubaliana na mimi na kuokoka.

Biblia iko wazi ikisema;

Matendo 17:29 "Basi, Kwa Kuwa Sisi Tu Wazao Wa MUNGU, Haipasi Kudhani Ya Kuwa Uungu Ni Mfano Wa Dhahabu Au Fedha Au Jiwe, Vitu Vyote Vilivyochongwa Kwa Ustadi Na Akili Za Wanadamu."

Mapema kabisa Biblia tena inasema;
Kumb 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. ''

Biblia iko wazi kabisa ikisema kwamba Ibada ya sanamu hukimbiwa na sio kusifiwa.
1 Kor 10:14-15 '' Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. ''

Biblia iko wazi tena akisema wenye akili za rohoni wahakikishe wanavunja sanamu na wala hawaziabudu tena.
Kutoka 23:24 '' Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande. ''

Kwanini kuleta ujumbe huu leo?
Yeremia 47:7 Biblia inasema ''Utawezaje kutulia, Ikiwa BWANA amekupa agizo? '' 

mimi Peter sijatulia wala kulikwepa agizo la BWANA.
Kila siku napenda kuandaa masomo yanayowajenga watu na kuwasaidia katika hatua zao za maisha ya kiroho. Lakini wakati mwingine MUNGU anaweza akakupa ujumbe wa maonyo hivyo inakupasa kumtii MUNGU na sio wanadamu.

Nabii Yona aliambiwa aende kuwaonya Ninawi, Yona alikwepa agizo la MUNGU na kukimbilia mji mwingine lakini MUNGU kwa kuonyesha Nguvu zake alimfanya Yona kumezwa na Samaki kwa siku tatu kisha Yona akakubali sasa kwenda Ninawi, Pointi yangu ni hii ingekuwaje kama Yona asingeenda Ninawi? Je kwa sababu adhabu kali ilikuwa inaifuata Ninawi, je ni nani angeihubiri ninawi hata watu wa ninawi wakaokoka na sio kuangamia? Jibu ni Yona aliyetakiwa kufanya hivyo.
Habari ya Yona ni hizi;
Yona 1:1-4 ''Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA. Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.''

MUNGU alileta tufani baharini hadi ikapelekea Yona kutupwa Baharini na Samaki kumumeza kwa siku 3 kisha MUNGU akamwambia samaki yule amtapike Yona pwani na Yona akawa salama, Yona akajitambua ndipo akaenda kuwaonya Ninawi.

Yona 3:3-10 '' Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama BWANA alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu.  Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.  Basi watu wa Ninawi wakamsadiki MUNGU; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie MUNGU kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba MUNGU hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende. ''





 Kuitii sauti ya MUNGU kwa Yona kuliwaokoa Mji wa Ninawi ili wasiangamizwe.

Leo ujumbe wa MUNGU unalenga kuwasaidia watu ili waache kutumainia sanamu wala wanadamu waliokufa bali wategemee MUNGU tu.
Leo ujumbe wa MUNGU unawataka watu waache kuabudu sanamu wala Mariamu bali wamwabudu JEHOVAH MUNGU tu.
BWANA YESU anawahitaji watu hao ndio maana ametuma maonyo kwao ili mwenye sikio la kusikia asikie na ampokee BWANA YESU kwa upya na kuashana na sanamu zote.

'' Haleluya. Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo yake. -Zaburi 112:1'' 

MUNGU hajaanza leo kuagiza watumishi wake kwa ajili ya watu anaowapenda ili wabadilike.
'' Sauti ya BWANA inaulilia mji, na mtu mwenye akili ataliona jina lako; isikieni hiyo fimbo na yeye aliyeiagiza.-Mika 6:9''

Mara nyingine mimi huwa nawaza hivi '' akisoma mtu mmoja tu na kubadilika nakuwa nimetimiza kusudi la MUNGU.''

Mwenye siko la kusikia na asikie Neno la MUNGU na sio Neno la watu ambao ni viongozi wa kanisa walioamua kujipotosha wenyewe.
Tii Neno la MUNGU na sio neno wa watu.
BWANA YESU yu karibu.

BWANA YESU anasema
'' Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa MUNGU wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.-Ufunuo 21:7-8 ''

MUNGU wa mbinguni akubariki kwa kunisikiliza kwa njia ya maandishi.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments