SIRI SABA ZA KUKUSAIDIA KUJIWEKA HURU KUPITIA MAOMBI YAKO.

Na mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe.
Ngoja leo nitoe siri 7 ili zikusaidie katika maombi yako ya kujiweka huru mbali na kuonewa na shetani.

Siri ya kwanza;
 
(A)Ndoto za kufanya mapenzi mara nyingine ni taarifa kwako kwamba hutaolewa au hutaoa. Ukimilikiwa na jini kwenye ulimwengu wa roho hakika ni ngumu mwanadamu kuwa mwenzi wako wa ndoa.
Kama huwa unachekelea ukiota ndoto unafanya mapenzi basi nakuomba amka kuanzia leo kwenye huo usingizi wa dhambi na vifungo. Omba na hata kufunga funga maana jina la YESU KRISTO ndilo pekee litakuwa msaada kwako.
Utakuwa huru kama tu BWANA YESU akikuweka huru.


Yohana 8:36 ''Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. ''
 
BWANA YESU atakuweka huru siku ukiamua kutubu na kuokoka na kuomba au kuombewa na watumishi wake.


(B) Mwanandoa kuota unafanya mapenzi ni taarifa kwako kwamba usipoharibu nguvu za majini kwenye ndoa yako kutaleta kutengana au vipigo kila mara, au kukosana au kutakuwa na ugumba na hata kuachana kunaweza kutokea.
Utakuwa huru kama ukimtii MUNGU huku ukimpinga shetani.


Yakobo 4:7-8 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.  Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. ''


Siri ya pili.

Kuna wakati ndoto mbaya utaziona kupitia vitu vizuri hivi 2 vifuatavyo.
Unaweza ukaota unatembea kando kando ya bahari, hiyo ni ndoto ya kimapepo au majini mara nyingine. 

Haribu hila za majini katika maisha yako, dalili mojawapo ya mtu kuvamiwa na mapepo ni pale mara kwa mara ataota anatembea kando kando ya bahari au anaogelea baharini.
Kuota unatembea ndani ya majumba mazuri sana nalo sio jambo la kufurahia sana maana wakati mwingine shetani hukupumbaza kwa vitu vizuri hasa nyumba nzuri na kando kando ya habari kwenye ndoa.
Sio ndoto zote za majumba mazuri zinafaa bali siku zote jitenge na mashetani na mbinu zao.
Mwite BWANA YESU akushindie kupitia maombi yako ya vita.


1 Yohana 3:22 '' Na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.''


Siri ya tatu.

Kama kuna kitu shetani huanza nacho katika kukukamata basi ni ufahamu wako. Watu wengi waliokamatwa kwenye ufahamu na shetani tangu utotoni ni vigumu sana kuelezwa kweli wakaikubali.
Kama mtu alirithi kuabudu sanamu au kuabudu shetani kupitia wapingakristo ni ngumu sana kumbadilisha.
Ingawa anajua kabisa kwamba hakuna uzima wa milele nje ya Wokovu wa BWANA YESU lakini ndugu huyo akikumbuka tu maneno ya baba yake aliyekuwa mfuga majini basi anaaimini hayo hata kama aliyaelezwa zamani sana na ni ya uongo.
shetani anaweza kukamata ufahamu wa baba katika ndoa na hiyo ikapelekea familia nzima kuacha Wokovu wa BWANA YESU hata kama wanajua kabisa walikoelekezwa na baba wa familia ni kwa shetani.


1 Kor 10:14 ''Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.''

Siri ya nne.

Mtu anayeteswa sana na roho ya mizimu na uganga wa kienyeji huwa katika hali ya uchafu wa mwili na kutokujijali, kuvaa nguo chafu na kupenda kuwa kwenye mazingira machafu.
shetani humfanya mtu huyo kuamini kwamba mizimu ni ulinzi wake kumbe ukweli ni kwamba mizimu ni wakala wa shetani.
Kuisaidia mizimu katika jambo lolote ni kumwabudu shetani.
Kuitolea mizimu sadaka ni kujiunganisha na shetani.
Kwenda kwa waganga wa kienyeji ni uovu mkuu.
Kama unaishi katika mashariti ya mizimu hakika wewe ni mtoto wa shetani na sio wa MUNGU, Jitenge na mizimu kwa kumkimbilia BWANA YESU aliye kweli ya MUNGU.
Kama wewe unaishi kwa kufuata masharti uliyopewa na mganga hakika wewe bado ni mtoto wa shetani, badilika kwa kukimbilia maombezi kanisani.

  Walawi 19:26-28 '' Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu. Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA.''

 Siri ya tano.
 
Chanzo kimojawapo cha mtu kuwa na roho ya kukataliwa ni mama yake kutunga mimba yake bila kutaka.
Kama mama yako alitunga mimba yako bila kutaka na akakuzaa wewe, ujue hiyo mimba kwa kuwa hakuitaka na wewe pia utakuwa na roho ya kukataliwa.
inawezekana unakataliwa na kila mchumba unayempata kumbe unateswa na roho ya kukataliwa.
Inawezekana kila ukipata kazi baada ya muda mfupi tu unafukuzwa kumbe tatizo ni roho ya kukataliwa.
Kuna watu wamezaliwa kwa bahati mbaya maana yake wazazi wake hawakupenda azaliwe, wazazi wake walimkataa tangu tumboni ndio maana sasa anateswa na roho ya kukataliwa.
Ndugu Yangu kama unateswa na roho ya kukataliwa, nakuomba tena nakuomba sana okoka au fuata maombezi kanisani ili iondoke hiyo roho ya kukataliwa inayokutesa sasa.
Sitaki useme kwamba ''labda MUNGU hanioni'' kumbe umekubali kuishi na roho ya shetani iitwayo roho ya kukataliwa.
BWANA YESU anaokoa na kuponya kwa kila anayemwendea. changamka ndugu ili baraka yako ije kwako katika jina la YESU KRISTO.


Mathato 18:18 ''Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. ''


siri ya sita.

shetani ukimruhusu akutawale basi atapanda ndani yako vitu vifuatavyo ambavyo vitakufanya uwe mbali na MUNGU wa mbinguni.
shetani ukimpa moyo wako atakuwekea ndani yako kiburi, hasira , uchungu, kukataliwa, uasi, uvivu, chuki, mashaka, kuchanganyikiwa, kujidharau, kutokuamini ya MUNGU, anasa, ukaidi, mashindano, mateso, ukosefu wa usingizi, roho ya mauti, woga, uongo, kutokusamehe, uasherati na uzinzi, uchafu, kujipamba kupita kiasi, kutokutii, wivu, kutoa mimba, fitina, kujihisi hisi pasipo sababu, kutokusoma Neno la MUNGU na udhaifu wa kuomba.

Ndugu hizo ni baadhi tu ya silaha za shetani lakini Biblia inasema


 ''wala msimpe Ibilisi nafasi.-Waefeso 4:27 '' 

Kama umeathiriwa na silaha hata moja katika hizo omba kwa jina la YESU KRISTO ukikataa hila hizo za shetani.
BWANA YESU anaokoka na kuponya kabisa na kila mitego ya giza.


 Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''

Siri ya saba.

Ziko dalili nyingi za mtu kuvamiwa au kuwa tayari amevamiwa na nguvu za giza.
baadhi katika hizo dalili za mtu kuvamiwa na nguvu za giza ni.
Mara kwa mara kupiga miayo bila hata kufanya kazi ya kuchosha ni dalili ya mtu kusumbuliwa na mapepo au mizimu.
Kama unapenda sana madaraka na hufurahia sana kusifiwa kuhusu madaraka uliyonayo, hiyo inaweza kuwa ngome kabisa ya shetani kwako ili ngome hiyo ikuletee uangamivu baadae.
Kuwadharau wengine na kujiona wewe unafaa kuliko wengine hilo ni pando la giza.


1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.'' 

MUNGU akubariki sana kwa kusoma hizo siri 7 ambazo nimekuandalia leo.
Nakutakia ushindi katika maombi yako baada ya kuzijua siri hizo sasa.
naomba mambo niliyoyaandika yakusaidie katika maombi na kubadilika kimtazamo ili umpendeze BWANA YESU siku zote.


 Mathayo 7:7 ''Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;''
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments