ANAYEZINI HANA AKILI KABISA.

Na Peter Mabula, Mtenda kazi katika shamba la BWANA.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
ANAYEZINI HANA AKILI KABISA, ndio hana akili kabisa maana ndivyo linavyosema Neno la MUNGU na sio mimi Peter.

Mithali 6:32-33 ''Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika.'' 


Kuzini ni machukizo kwa MUNGU.
Kuzini inawezekana likawa ni jambo linaloongoza katika kuwaangusha watu wengi.
uasherati ni kuzini.
Uzinzi ni kuzini.
=Uzinzi ni kitendo cha mtu aliyeoa au kuolewa akifanya mapenzi na mtu yeyote nje ya mkewe/mmewe mmoja tu.
=Uasherati ni mtu yeyote asiyeolewa au kuoa anapofanya mapenzi na mtu yeyote yule.


Kama asiyeoa au kuolewa akifanya mapenzi na mtu aliye katika ndoa huyu atakuwa anafanya uasherati na yule wa kwenye ndoa atakuwa anafanya uzinzi.



Waebrania 13:4 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu.''

Uzinzi na uasherati ni dhambi mbaya na imewakosesha wengi.
Biblia inaita dhambi hiyo kuwa ni fedheha ambao haifutiki kirahisi maana kuna maagano mabaya huambatana na tendo hilo chafu.
Kitendo wanachokifanya wazinzi na waasherati kinaitwa kuzini.

Biblia iko wazi sana ikisema '' Usizini.-Kutoka 20:14''

 Kuna watu pia hukosea katika eneo hili;
Walikuwa wanandoa lakini baadae wanaachana na kila mmoja kuolewa na mtu mwingine, huko ni kwenda kuzini ndivyo Biblia inavyosema 

Mathayo 5:32 '' lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.''

 Je umeachana na mumeo au mkeo wa ndoa na umempata mwingine wa kuzini naye?
Je mwanandoa alikusaliti ndio maana umeachana naye?
Je mwanandoa mwenzako alitembea na rafiki yako wa karibu ndio maana umeachana naye?
Ndugu, Ni kweli mwanandoa mwenzako alikosea sana na kwa uovu wake huo itampasa hukumu kwa MUNGU kama hatatubu, lakini hata wewe usidhani kama uko salama kama utazini na mtu yeyote.
Usidhani utasamehewa kwa MUNGU kama wewe hujawasamehe wengine.

Uasherati sio sababu ya wanandoa kuachana maana umeambiwa samehe 7 Mara 70 tena kama hutasamehe na wewe sahau kusamehewa na MUNGU hiyo iko mathayo 6:14-15.

Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.'' 

Lakini pia kuna angalizo hapa kuhusu ninyi wanandoa.
Ni muhimu kuwa waombaji ili dhambi ya usaliti isitokee.
Ni muhimu kuwa wacha MUNGU ili shetani usaliti asiivamie ndoa yenu.
 mwanamke ameambiwa amlinde mmewe kwa maombi hiyo iko Yeremia 31:22 '' ......... Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.''
Hivyo wakati mwingine kama Huyo mama anayesalitiwa kama hata mwaka mzima hajawahi kufunga kwa ajili ya ndoa yake basi anapolaumu kusalitiwa pia akumbuke kujilaumu mwenyewe maana hakusimama katika zamu yake.

Mwanaume nae kaambiwa ampende mkewe kama nafsi yake(waefeso 5:28, Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. ) sasa kama amemgeuza mkewe ngoma akisalitiwa amlaumu nani?
Sina maana kwamba mwanamke ukipigwa na mumeo basi umsaliti, na tena sina maana kwamba mama ambaye hamuombei mumewe basi mume huyo ana haki ya kumsaliti mwenziwe, hapana,  kila mmoja anawajibika kwa MUNGU lakini Neno la MUNGU linatupa ufahamu wa jinsi ya kujua faida mojawapo ya maombi na jinsi ya mwanaume kumpenda na kuthamini mkewe.

Lakini  kwanini uzini?
Kwanini uisaliti ndoa yako?
Siku mnafunga ndoa ulikuwa na furaha naye sana tena ukathibitisha mbele ya mashahidi wengi wakiwemo watumishi wa MUNGU, sasa kwanini unataka kumsaliti?
Ndugu, Kumbuka neno kwamba  imeandikwa aziniye na mwanamke/mwanaume hana akili kabisa.
  sasa kwanini wewe mwanandoa unataka kuzidiwa akili na mtoto mchanga kwa kwenda kuzini?
Maana anayezini hana akili hata moja ndivyo biblia imesema lakini angalau mtoto mchanga ana akili ya kumtambua mama yake ndio maana nasema mzinifu anazidiwa akili hata na mtoto mchanga. tena mzinzi anazidiwa akili hata na kuku anayejua dalili za uwepo Wa mwewe kwenye eneo hilo alilopo.

Ndugu usikubali kutenda dhambi ya usaliti wa ndoa kwa kutoka nje.
Kijana jilinde ujana wako, usikubali kufanya ngono na mtu yeyote.

Mithali 6:25-26 ''Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani '' 

Ndugu, Heshimu ndoa yako, kumbuka agano la ndoa siku ile kanisani, kumbuka kuna jehanamu kwa wazinzi na waasherati, kumbuka kuna magonjwa mabaya unaweza kuyapata kwa sababu ya mpango wako wa kuisaliti ndoa yako.
Hata kama una elimu kubwa kiasi gani tambua kwamba ukizini basi wewe huna akili hata moja.
Mtii MUNGU anayekataza dhambi, iogope dhambi hii mbaya na usikubali kuitenda.
Kaa mbali na watu wenye mipango hiyo.
Jitenge na rafiki anayetaka kukuangusha katika dhambi ya uzinifu.
Usiangalie picha wala video za ngono maana hayo ni matunda ya shetani ili kukunasa katika dhambi.
Heshima yako inaweza kupotea kwa siku moja tu kama ukikubali kufanya ujinga huu wa kuzini. Mche MUNGU utaishi na kumbuka hakuna mbingu ya wazinzi wala waasherati.
Unaweza ukamchukua mke au mume wa mtu kwa lengo la kutaka kuzini naye lakini huko huko kukawa ndio kifo chako.
acha uzinzi na uasherati.

Mithali 6:27-29 '' Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia.'' 

 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments