KILA ANDIKO LENYE PUMZI YA MUNGU LINA KAZI NNE(4) KWA MWANADAMU.

Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

''Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo-Mithali 30:5-6.''
U Hali Gani Mpendwa Wa KRISTO! 
Nakutakia Nuru Njema Ya KRISTO YESU Mfalme Wa Uzima.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

2 Timotheo 3:16-17 '' Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.''

KAZI NNE ZA NENO HAI LA MUNGU KWA MWANADAMU.

 1. Kufundisha wanadamu.
Kazi ya kwanza ya Neno la MUNGU ni kuwafundisha wanadamu.
Neno la MUNGU lipo kwa ajili ya kutufudisha wanadamu ili tujue jinsi ya kumpendeza MUNGU.
Neno la MUNGU hutupa ufahamu wa kujua mema na mabaya.

Wakolosai 3:16 ''Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu.'' 

Neno la MUNGU hutufundisha kujua kazi yetu duniani na tutakuwa wapi milele ijayo.
Neno la MUNGU ni mwalimu kamili wa maisha yetu.
Ndani ya Neno la MUNGU kuna nguvu za MUNGU.
Kila andiko lenye pumzi ya MUNGU linafaa kwa mafundisho.
Litii Neno la MUNGU maana lina kufundisha.
Katika maisha yako ukikataa kufundishwa na neno la MUNGU jua tu utafundishwa neno la shetani. Kuna Neno la MUNGU ambalo ni Biblia na kuna Neno la shetani. Mwanadamu akilikataa Neno la MUNGU lazima tu atakutana na neno la shetani na hilo litamfundisha kukaa mbali na MUNGU wake.
Mafundisho ya Neno la MUNGU leo yapo mengi tu na yakiwataka wanadamu kumpokea YESU na kuishi maisha matakatifu lakini sio wote hulipokea Neno la MUNGU.
Walioshinda dhambi ni wale waliodumu katika kufundishwa neno la MUNGU.
Waliozishinda nguvu za giza ni wale waliojifunza Neno la MUNGU na wakalitendea kazi.
Waliobarikiwa ni wale waliojifunza Neno la MUNGU kisha neno  hilo wakawa wakiliishi katika maisha yao.
Kuna viwango vya kulijua Neno la MUNGU ndio maana tunatakiwa kujifunza sana Neno la MUNGU ili tukue kiroho.

Waebraria 5:12 '' Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya MUNGU; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.''
 
Kwa sababu ya upungufu wa Neno la MUNGU ndani ya mtu, wakati mwingine mtu huyo anahitaji maziwa na sio Nyama. Yaani anatakiwa afundishwe vitu vya awali na sio mambo mazito. mfano anatakiwa afundishwe kuombea chakula, kuimba, kutulia mbele za MUNGU na jinsi ya kuwa mbele za MUNGU. Mtu kama huyo anakuwa bado  hajahimili kufundishwa kwamba katika imani huwa wakati hata kuna kufa kwa ajili ya KRISTO bila kumkana, wakati mwingine kuna kupitia majaribu mazito na mristo ni lazima awe ni mtoaji wa fungu la kumi na sadaka nzuri.
Mtu wa hivyo ukimfundisha kwamba anatakiwa atoe mali zake kuwapa maskini atakimbia fundisho la MUNGU(Marko 10:16-23).

Waliokua kiroho ni wale waliojifunza Neno la MUNGU na kulizingatia.
Kila andiko lenye pumzi ya MUNGU linafaa kwa mafundisho. 

2. Kuonya watu makosa yao.
Kila andiko lenye pumzi ya MUNGU linafaa kwa kuwaonya watu makosa yao.

2 Timotheo 2:14 '' Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.'' 

Zile zote unazoona ni dhambi ni kwa sababu Biblia ndio iliyosema hivyo, hivyo ni jukumu lako siku zote kuitii Biblia.
Ukiiepuka Biblia au fundisho la Biblia linaloletwa  kupitia watumishi wa MUNGU hakika hutajua kosa lako na utafanya mambo ukijua uko sawa tu kumbe ni dhambi hivyo unahitaji Neno la MUNGU likuweke sawa. Neno huonya na Neno hukutaka uache dhambi zote na sio Nusu. 

Mithali 5:22-23 ''Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake. Atakufa huyo kwa kukosa maonyo, Naye atapotea kwa wingi wa ujinga wake.''
Maonyo sahihi ni Neno la MUNGU.

Mtu akilikwepa Neno la MUNGU wakati mwingine anaweza akafa bila kutubu maana hakupata maonyo ya MUNGU ambayo ni Neno la MUNGU.
 Kila andiko lenye pumzi ya MUNGU linafaa kwa kuwaonya watu makosa yao ili wayaache na kutubu na kuokoka. 
Andiko lenye pumzi ya MUNGU maana yake limetoka kwa MUNGU. Sio maandiko yote yana pumzi ya MUNGU mengine yana pumzi ya shetani au pumzi za wanadamu ila sio  pumzi ya MUNGU. Ndio maana leo kuna vitabu vingi vya zamani na vya sasa, kuna magazeti na kuna hadithi; hayo yote ni maandiko yaliyoandikwa lakini hayana pumzi ya MUNGU kwa sababu hayajatoka kwa MUNGU. Ila kila andiko lenye pumzi ya MUNGU linafaa kuwaonya watu makosa yao.

 Zaburi 19:12-14 ''Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri. Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa. Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.''

Kila andiko lililotoka kwa MUNGU lina pumzi ya MUNGU, Andiko lililotoka kwa MUNGU ni Biblia pekee na hiyo Biblia ina mkusanyiko wa maandiko mengi ambayo yametoka kwa MUNGU na yana pumzi ya MUNGU.
Kama kuna kitabu ambacho wanadamu hata wafanyeje hawawezi kukibadili au kukigeuza basi ni Biblia maana hiyo original yake iko mbinguni pia ROHO MTAKATIFU ambaye ndiye mwandishi wa Biblia hutufafanulia sisi ili tuielewe sawa sawa Biblia, Wanaofundisha uongo hao wanajiweka katika hukumu ya MUNGU.
Wanaobadili maandiko hao hubadili maandishi lakini Neno bado liko hai na lina ROHO wa MUNGU, na hao kwa kubadili huko huitafuta hukumu ya MUNGU.
  Kila andiko lenye pumzi ya MUNGU linafaa kwa kuwaonya watu makosa yao ili wayaache na kutubu na kuokoka.


. 3. Kuwaongoza watu.
Kazi mojawapo ya neno la MUNGU ni kuwaongoza watu wa MUNGU.
Kila andiko lenye pumzi ya MUNGU linafaa kwa kuwaongoza watu wa MUNGU.
Zaburi 139:23-24 ''Ee MUNGU, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.'

Kuongozwa na MUNGU ndio kuongozwa na Neno la MUNGU maana MUNGU hulitumia Neno lake katika kuwaongoza watu wake. 
Ukitaka uwe katika njia sahihi ya maisha yako basi litii Neno la MUNGU ambalo ni Biblia.

Zaburi 119:105 ''Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.'' 
 
Kazi ya kiongozi ni kuongoza.
Neno la MUNGU ni kiongozi wetu wa kutuongoza ili tutende mema na sio mabaya. Ndani ya Neno la MUNGU kuna injili ya KRISTO ambayo ni ya milele kwa ajili ya kuwaokoa wanadamu.
Ndani ya Neno la MUNGU kuna MUNGU.
Ndani ya Neno la MUNGU kuna YESU KRISTO na ndani ya Neno la MUNGU kuna ROHO MTAKATIFU, Tena huyo ndiye aliyeiandika Biblia akiwatumia wanadamu aliowapenda.
Ukikataa kuongozwa na Neno la MUNGU hakika utaongozwa na neno la shetani.
Neno la MUNGU hukufanya umpendeze MUNGU lakini neno la shetani hukufanya umpendeze shetani na wanadamu watenda dhambi. jitahidi sana katika maisha yako kuongozwa na Neno la MUNGU.
YESU KRISTO ni Neno katika Neno la MUNGU, Kwake kuna uzima sasa na uzima wa milele.
Ndani ya Neno la MUNGU kuna ROHO MTAKATIFU ambaye hutufundisha utakatifu halisi.
Ndugu, katika maisha yako kubali kuongozwa na Neno la MUNGU.
Usilikwepe Neno la MUNGU wala usilionee aibu neno la MUNGU bali lishike na liishi na litumie katika maisha yako.
Neno la MUNGU ni kiongozi mwenye macho halisi.
Ukilitii Neno la MUNGU utamuona MUNGU katika maisha yako.

4. Kuwaadabisha katika haki wanadamu.


Neno adabisha linatokana na neno adabu.
Adabu maana yake tabia njema.
Sasa Neno la MUNGU kazi yake nyingine ni kumfanya mtu awe na tabia njema kama akilitii.

Warumi 13:13 ''Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.'' 
 
Adabu njema ni kuishi kwa kumtii MUNGU kupitia Neno lake.
Neno la MUNGU huadabisha katika haki.
Huwezi kuwa mwenye adabu mbele za MUNGU kama hujakubali kwanza kuadabishwa na Neno la MUNGU.
Ni vizuri sana kila mtu akawa na adabu kwa MUNGU aliyemuumba.
Neno linaweza kukufanya kiwango chako cha adabu mbele za MUNGU kiongezeke.
Watu wengi hawana hofu ya MUNGU kwa sababu hawana Neno la MUNGU. Likiwepo Neno la MUNGU na Mwanadamu akalitii litamsaidia katika kukaa sawa mbele za MUNGU.
Mfano mmojawapo hai ni kwamba Biblia inasema kwamba pasipokumpokea YESU KRISTO mwanadamu hawezi kuingia uzima wa milele(Yohana 3:16-21, Warumi 10:17,Matendo 4:12,Warumi 6:23, 2 Kor 5:17,Yohana 14:6 na Warumi 10:9-10 N.k)
Mwanadamu anayeutaka uzima wa milele ni lazima kwanza awe na adabu kwa MUNGU kwa kulitii Neno lake na mpango wake.
Kama huna adabu huwezi kukubali kuokoka.
Kumbuka kwamba kuna adabu na kuna adhabu, ukikosa adabu kuna adhabu.
Kama hupendi kuadabishwa na Neno la MUNGU huwezi Kuokoka.
Kama hutaki kuongozwa na Neno la MUNGU ni ngumu kuifikia toba na kumpokea YESU.

Mithali 1:7 '' Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. '' 
 
Kunahitajika sana kila mwanadamu akubali kufundishwa na Biblia.
Kunahitajika sana kila mwanadamu akubali kuongozwa na Neno la MUNGU.
Kunahitajika sana kila mwanadamu akubali kuonywa na Neno la MUNGU.
Kunahitajika sana kila mwanadamu akubali kuadabishwa na Neno la MUNGU.
 

Kuna watu hudharau Neno la MUNGU na hiyo ni hatari mbaya sana maana nje ya Neno la MUNGU kuna neno la shetani ambalo mwanadamu akilifuata ataikosa mbingu.
Nakuomba ndugu lishike Neno la MUNGU wala usiliache.
 Pia nakuomba kwamba Katika Mahubiri Yeyote Ya Neno La MUNGU Katika KRISTO YESU Ni Muhimu Uwe Unajiuliza; Je, Anayesema Nami Ni Huyu Mtumishi, Au Hapa MUNGU Anasema Nami Kupitia Mtumishi Huyu?. Ukigundua Kwamba Ni MUNGU Anasema Na Wewe Kupitia Mahubiri Yalee Tii Hilo, Maana La MUNGU Ni La MUNGU Tu Na La MUNGU Linatakiwa Kila Mwanadamu Mwenye Akili Alitii Daima. Ni Hasara Kwako Usipolitii Jambo Au Neno Lililotoka Kwa MUNGU Kuja Kwako.

Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''
  Wako watu wamechaguliwa na MUNGU ili wawafundishe watu wa MUNGU kuhusu Neno la MUNGU,Naamini na wewe ni mmoja wao lakini naomba niseme kwamba  Ulipopakwa Mafuta Kwa Ajili Ya Kazi Fulani Ya MUNGU Ni Muhimu Ujue Kwamba Unatakiwa Uitimize Kazi Hiyo. Kumbuka Pia Kwamba Amelaani Aifanyaye Kazi Ya MUNGU Kwa Ulegevu(Yeremia 48:10) Ndivyo Biblia Isemavyo. 
Dhoruba Isikukimbize Kwenye Wito Wako Wa Kazi Ya MUNGU. Dharau Za Watenda Dhambi Zisikuondoe Kwenye Jukumu Lako Ulilopewa Na MUNGU. 
Kuna Makanisa Leo Hayana Wachungaji Kwa Sababu Wachungaji Husika Wamekimbilia Ajira Serikalini Au Pengine. Kuna Waimbaji Wa Viwango Vikubwa Leo Wameacha Wito Wao Kwa Sababu Ya Biashara. Mpendwa, Timiza Kazi Yako Uliyoitwa Kwayo Na Mfalme Wa Uzima YESU KRISTO.

 Neno la MUNGU siku zote linawataka wanadamu kumgeukia MUNGU ili wapone(Mathayo 11:28).
BWANA YESU Hajawahi Kuchoka Kukualika Wewe Kwenda Uzima Wa Milele, Hata Muda Huu Kupitia Ujumbe Huu Anakualika Kwenye Sherehe Za Uzima Milele. YESU Leo Anasema " Njooni Kwangu Ninyi Nyote Msumbukao Na Wenye Kulemewa Na Mizigo, Nami Nitawapumzisha- Mathayo 11:28" 

 Ndugu Peleka Kwa YESU Hiyo Mizigo Ya Magonjwa Inayokusumbua, Peleka Kwa YESU Hizo Roho Za Uzinzi Na Uongo Zinazokusumbua, Ataziondoa Na Kuzitupa Kuzimu.
 Ndugu Usione Fashion Kutoa Mimba Na Wala Usione Ujanja Kuitwa Changudoa. Dhambi Ni Mbaya Na BWANA YESU Hataki Dhambi Hizo Zikupeleke Motoni, Mkimbilie Leo Na Utakaa Salama. Tumtafute BWANA YESU Maadamu Anapatikana, Tumwite Yeye Maadamu Yu Karibu, Mtu Mbaya Na Aache Njia Zake Mbaya, Na Arejee Kwa MUNGU Wetu Naye Atamrehemu, Na Arejee Kwa MUNGU Wetu Naye Atamsamehe Kabisa. Ndugu. Acha Kutangatanga Kwa Shetani, Mara Leo Kwa Mganga Wa Kienyeji, Kesho Kwenye Uzinzi, Kesho Kutwa Uko Bar Kwenye Pombe. Kataa Leo Na kimbilia Kwa BWANA YESU Anayeokoa. MUNGU Akubariki,Na Ukikubali Na Kutii, Utakula Mema Ya Nchi.
Isaya 55:6-7 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. '' 
 

Asante kama unanielewa ndugu yangu.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments