NJIA SABA ZA KUKUSAIDIA KUIACHA DHAMBI INAYOKUSUMBUA.

Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Dhambi ni kosa la kwenda kinyume na utaratibu wa MUNGU.
Dhambi ni uasi kwa MUNGU.
Dhambi ni kulikataa kusudi la MUNGU.
Dhambi ni matendo maovu yote atendayo mwanadamu mbele za MUNGU.
Warumi 6:12 '' Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;''
 
Kama kuna kitu cha kwanza ambacho mwanadamu anatakiwa kushughulika nacho basi ni kuacha dhambi ili kuishi maisha matakatifu.
Kwanini tunajifunza njia hizi saba za kukusaidia kuacha dhambi?
Ni kwa sababu hakuna siri kwa MUNGU.

Mithali 15:3 ''Macho ya BWANA yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.'' 

Kwa MUNGU matendo yetu yote yako wazi mbele zake.
Na kama mtu asipoacha dhambi na asipotubu maana yake matendo yake yataendelea kukaa, na siku ya mwisho kama matendo yake yalivyokuwa angali alipokuwa duniani ndivyo atakavyolipwa siku ya mwisho.

 Obadia 1:15 ''Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''

Waliotenda mema katika KRISTO wataupata uzima wa milele na waliotenda mabaya wote watapokelewa na ziwa la moto.
Ni muhimu sana kuacha dhambi.
Ni Muhimu sana kutafuta njia za kuiacha hiyo dhambi inayokusumbua.

1Timotheo 1:15 ''Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba KRISTO YESU alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.'' 

Kumbuka kuwa ukimpokea YESU na ukatubu kwake hakika dhambi zako zote zitafuta na MUNGU hatazikumbuka tena. Lakini usipotubu na kuokoka hakika uovu wako utadumu hadi siku unaondoka duniani maana hukutubu na kuacha uovu huo.
Kuna watu hudhani kwamba hawawezi kuacha dhambi lakini ukweli ni kwamba huo ni uongo tu wa shetani kuhakikisha mwanadamu huyo haendi uzima wa milele.
Kama kuna dhambi inakutesa na hujui jinsi ya kuiacha nakuomba jifunze ujumbe huu na uuhamishie katika matendo utashinda.

 NJIA SABA ZA KUKUSAIDIA KUIACHA DHAMBI INAYOKUSUMBUA.

1. Kumtii MUNGU kupitia Neno lake Biblia.
Yakobo 4:7-10 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza. ''

Njia muhimu za kumtii MUNGU ni kumpinga shetani.
Ni kujitenga na kila jambo la kishetani.
Kumtii MUNGU ni kumwabudu katika Roho na kweli.
Kama kuna dhambi inakutesa ni kwa sababu tu hujaamua kumtii MUNGU.
Kumtii MUNGU ni kuiacha dhambi hiyo kwa nguvu kisha kuhamishia nguvu zako kwa MUNGU.
Ndugu anza kuanzia leo kumtii MUNGU na Neno lake utashinda.
 
2. Kuishi maisha matakatifu.

1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''


Mtakatifu kinyume chake ni mtenda dhambi.
Kama unataka kushinda dhambi basi acha dhambi na kuanza kutenda mema, huo ndio utakatifu.
Anza tu kuipenda mbingu kwa kuamua kuishi maisha matakatifu.
Jitenge na kila vishawishi vilivyokufanya uingie dhambini.
Jitenge na marafiki wabaya wote.
Acha tabia zako zote ambazo ni za dhambi. Acha ulevi, uzinzi, uongo na kila dhambi.
Amua tu kumpendeza MUNGU kwa kuanza kuishi maisha matakatifu kila siku.
Kama ukiamua hakika utaona nguvu ya MUNGU ya kukusaidia kuishi maisha matakatifu.
Kumbuka huwezi kuishi maisha matakatifu kama uko mbali na MUNGU, uko mbali na Neno la MUNGU, Uko mbali na watakatifu wengine ambao watakusaidia kusonga mbele vyema, ndio maana ni muhimu sana wewe ukaokoka na kuanza kuwa mhudhuliaji wa vipindi kanisani ili ukue kiroho na ukikua kiroho itakuwa rahisi sana kwako kushinda dhambi.

3. Kuokoka.

Yohana 3:16-21 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU. ''

Kuokoka ni jambo la muhimu sana kama unataka kuzishinda dhambi.
Kuokoka ndio mwanzo wa mwanadamu kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
Kuokoka ni kumpokea BWANA YESU kama Mwokozi wako.
Hakuja jambo zuri na muhimu kwa kila mwanadamu kama kumpokea YESU na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Kama unataka kuishinda hiyo dhambi nakuomba okoka na uwe mhudhiliaji wa ibada, huko kanisani utapata maarifa sahihi ya kukusaidia kushinda dhambi na mambo ya ulimwengu.
 
4. Kujitenga na dhambi.

Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.''

Biblia iko wazi sana ikisema kwamba dhambi ina matokeo mabaya sana.
Dhambi ina mshahara na huo mshahara unaitwa mauti yaani kutengwa na MUNGU. Na mauti hiyo kama Mwanadamu huyo hatatubu maana yake mauti hiyo ya dhambi itazaa jehanamu.
Kama unataka kushinda dhambi hakikisha unajitenga na kila dhambi.
Kila kisababishi cha dhambi hakikisha unakaa mbali nacho.
Kama ni wanadamu ndio hukushawishi kuingia dhambini nakuomba leo amua kuwa karibu  na YESU mwenye uzima wako. tii Neno la MUNGU utashinda.
Kama unaweza kuacha kula chakula fulani ulichokatazwa kula na daktari, basi mimi naamini kabisa kwa njia kama hiyo hiyo unaweza kuamua kuacha dhambi zote, maana ukitenda dhambi kuna madhara kama ambavyo ukila chakula kile ulichokatazwa na daktari.
Ndugu, amua tu kutoka moyoni mwako kuacha dhambi zote na utabarikiwa rohoni na mwilini.

5. Kuutumia muda wako wote vizuri na kwa malengo mema.

Waefeso 5:15-17 ''Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya BWANA.''

Biblia inakushauri kuukomboa wakati maana nyakati hizi ni nyakati za maovu mengi.
Muda ambao unautumia disko ungeutumia kwa MUNGU ungeziepuka dhambi.
Muda ambao unautumia kuzini ungeutumia katika maombi ungeepuka dhambi.
Dhambi unaweza ukaishinda kwa kuamua tu kuutumia muda wako vizuri. Kama rafiki yako anakuita ili mkafanye mabaya hakikisha muda huo wewe utumie kwa MUNGU. Hudhuria semina za Neno la MUNGU. Hudhuria mikutano ya injili. Nenda kanisani na utumie muda wako mwingi katika mabo ya MUNGU utashinda.

6. Kufunga na kuomba.
Mathayo 17:21 ''Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.''

Kazi mojawapo ya maombi ni kuutiisha mwili ili tamaa mbaya zisiinuke.
Kazi mojawapo ya maombi ya kufunga ni kuifanya roho yako iutawale mwili na sio mwili kuitawala roho.
Kama huwa huwezi kupata muda wa kuomba ni ngumu kushinda ya dunia.
Kama huwa huwezi kupata muda wa kufunga na kuomba ni ngumu kushinda dhambi.
Nakushauri kuanzia leo uwe na muda wa kuomba na kufunga itakusaidia.
Sio yale maombi ya kuombea chakula tu na wewe unajiita muombaji, wala sio yale maombi ya kabla ya kulala unaomba dakika moja na wewe unajiita muombaji bali maombi ya kudumu na ya muda mrefu.
Sio yale maombi ya kukariri na wewe ujaiita muombaji, bali ni maombi yanayotoka katika moyo wako kwa imani sio kukariri.
Tafuta ushindi wako katika maombi.
Ita utakatifu kupitia maombi yako.
Ita nguvu za kuishinda dhambi kupitia maombi.
Utiishe mwili wako kupitia maombi na kufunga.
Hakika ukizingatia utashinda.
 
7. Kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:16 ''Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.''

Kazi mojawapo ya ROHO wa MUNGU ndani yetu ni kutusaidia kushinda mambo yote ya ulimwengu.
Changamoto ya wanadamu ni jinsi ya kumpata huyo ROHO MTAKATIFU maana yeye hachangamani na uovu, yeye ni mtakatifu na akiingia ndani yako atakusaidia kuishi maisha matakatifu ila kama tu ukimtii.
Mambo mengi yanayokuja mbele yako ni mapando ya giza ili kukufanya utende dhambi, lakini akiwapo ROHO wa MUNGU atakusaidia jinsi ya kuepuka dhambi.
Unaweza kukuta Binti unaitwa na rafiki yako, yule rafiki yako anakuwa amepanga akupe madawa ya kulevya kisha atembee na wewe, Kama una ROHO wa MUNGU ni lazima tu atakukataza kwenda maana yeye anajua jambo kabla hata halijatokea. ukimtii ROHO wa MUNGU utashinda.

Asante kama unanielewa ndugu yangu.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments