JE UMEITIKA WITO WA MUNGU KWAKO?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
'' .... ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.(Matendo 13:2)


Je wewe ndugu umeitwa na MUNGU kwaajili ya kazi gani?
Kama wewe hujatengwa kwa kazi maalumu jiulize sana?
Inawezekana umeitwa ili umwimbie MUNGU kanisani lakini hutaki.
Kuna wengine wameitwa na MUNGU ili waimbe nyimbo za injili lakini wao wamehamia kumwimbia shetani kupitia nyimbo za kidunia.
MUNGU hajakuondolea karama yako hiyo ambayo unaitumia kumwimbia shetani na sio yeye MUNGU, Lakini kuna hukumu mbeleni kwa watemnda mabaya wote. MUNGU amekuacha na karama yako hiyo kwa sababu;
'' Kwa sababu karama za MUNGU hazina majuto, wala mwito wake.-Warumi 11:29''


Umeitwa kuhubiri lakini uko busy na mambo yako tu.
Mbinguni wanakujua kwamba wewe ni mhubiri mkubwa sana duniani lakini cha ajabu hujawahi kumhubiri mtu hata mmoja. Karama yako umeikalia tu.
Umeitwa kuwategemeza wachungaji au kanisa lakini wewe unategemeza harusi tu na bar kwa ulevi wako, unategemeza gesti kwa sababu ya uzinzi wako na mwingine anategemeza waganga wa kienyeji kwa kuwapelekea kuku na pesa ili wamdanganye vizuri.

Umeitwa ili uishi maisha matakatifu lakini wewe unaishi maisha ya dhambi.
1 Petro 1:15-19 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO .''


Umeitwa ili uwe nabii wa MUNGU lakini wala hata kuokoka bado hujaokoka ndio maana MUNGU hajaanza kukutumia katika kile alichokuitia. Wewe umeitwa kuwa nabii lakini kwa sababu hujitambui ndio maana manabii wa shetani wao wanazitumia nafasi zao vizuri ili wewe uliyetakiwa kuwanyamazisha hata hujaokoka ndio maana wanaendelea kushika chati. Manabii wa shetani ni wale wanaomkataa YESU na wokovu wake na hao ulitakiwa wewe ndio uwanyamazishe kwa kuhubiri wokovu wa BWANA YESU lakini kwa sababu hujitambui ndio maana MUNGU hajaanza kukutumia.
Umeitwa kulihudumia kanisa la MUNGU lakini wewe uko busy kwa shetani ndio maana ROHO MTAKATIFU hasemi na wewe.
Wengine wameacha wokovu kabisa.
Ndugu, itakusaidia nini kuacha wokovu wa KRISTO kisha kuanza kung'ang'ania vitu vya kidunia?
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake.
Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA , bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''


Wengine wamedharau vyeo vyao alivyowapa MUNGU katika kanisa.
Ndugu usidharau cheo chako alichokupa MUNGU bali mtumikie MUNGU kwa upendo katika nafasi yako hiyo na utabarikiwa.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments