MAOMBI YA KUING'OA NA KUIZIMA MISHALE YOTE YA SHETANI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe.
Leo tunaomba kuing'oa na kuizima mishale yote  ya shetani katika maisha yetu, kazi zetu, biashara zetu, ndoa zetu, uchumba N.k.

Zaburi 11:2 ''Maana, tazama, wasio haki wanaupinda uta, Wanaitia mishale yao katika upote, Ili kuwapiga gizani wanyofu wa moyo. ''

Kazini kwako, wanakurushia mishale gani wafanyakazi wenzako hadi unataka kufukuzwa kazi?
Kwenye uchumba wako, wabaya wako unakurushia mishale gani hadi unataka kuachwa?
Kwenye ufahamu wako umerushiwa mshale gani hata siku hizi huamui vyema?
Kwenye ndoa yako mumerushiwa mshale gani na wachawi hata migogoro badala ya kupungua na kuishi kwenu ndio imeongezeka?
Kuna mishale mingi ya maadui zako ambayo hurushwa katika ulimwengu wa roho ili kukudhuru, kukuharibia au kukuachia maumivu mabaya.
Biblia hapo juu inaonyesha kwamba watu wabaya huwapiga mishale watu wenye haki.
Wakati mwingine MUNGU hujulisha yanayopangwa na maadui zako kwa njia ya ndoto.
Ndugu mmoja alisema kwamba aliota anafukuzwa na mbwa aliyekonda, yule mbwa akamuuma  sehemu kidogo ya kisigino cha mguu.
Akaambiwa  kwamba hiyo ni roho ya ukahaba inamwandama na roho hiyo amerushiwa ikiwa na magonjwa mabaya. Aliambiwa ahakikishe anaomba kuharibu biashara hiyo ya shetani kwenye maisha yake, aliambiwa pia awe makini sana na ajitenge na marafiki wabaya lakini hakufanya hivyo na miezi michache baadae alijulisha kwamba  ameambukizwa ukimwi katika mazingira ya kutatanisha maana alizini mara moja tu, alijikuta anaomba msamaha wakati bure.
Mtu mmoja akaota mbuzi anakula nyasi nje ya  duka lake, kumbe ni roho ya chuma ulete imetumwa katika biasahara yake, na baada ya miezi kadhaa akafilisika na kufunga lile duka.
roho za shetani ambazo hutumwa kama mishale katika maisha ya wanadamu ni nyingi sana. Najua kwenye ndoto wakati mwingine huwa unajulishwa kabisa kinachoondelea lakini huwa unapuuzia hadi baada ya majanga kukupata ndio unaikumbuka hiyo ndoto.

Marafiki zako unaowaamini sana wanaweza kukuendea kwa waganga ili tu  urushiwe mshale wa kukataliwa na mumeo ili wampate wao. Unaweza tu kushangaa kwamba siku hizi mumeo kabadilika. Unaweza ukajihukumu kwamba labda siku hizi wewe hupiki chakula vizuri, unaweza ukajihukumu kwamba siku hizi umekuwa mchafu sana ndio maana mumeo hana habari na wewe. 
cha ajabu unaweza ukajitahidi sana kupika vizuri na kuwa msafi muda wote lakini tatizo ndilo linaongezeka. Kumbe tatizo halikuwa uchafu wala upishi bali kuna mishale ya waovu imerushiwa ndio maana hutakiwi tena na mumeo.
Maneno ya uchonganishi ya watu juu yako yanaweza kuwa ni mshale wa shetani kukudhuru.Wakati mwingine maadui zako wanaweza tu kukuendea kwa wachawi au waganga na ndoa yako ikarushiwa mishale ya kukuharibia.
Mimi Peter nimekulia kijijini  huko tulijifunza kutengeneza mishale na upinde katika ulimwengu wa kimwili. Kila familia kijijini silaha kuu ya baba mwenye nyumba ni upinde na mishale, panga pamoja na rungu kubwa au fimbo. Hiyo ni mishale katika ulimwengu wa mwili lakini ipo mishale katika ulimwengu wa roho ambayo ni mishale hatari sana kuliko mishale katika ulimwengu wa mwili.
Mishale ni hatari sana maana ikishaingia kuitoa ni vigumu sana.
Lakini mishale yote katika ulimwengu wa roho ni rahisi sana kuing'oa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Lakini pia mishale mingine hata kama ukiitoa huwa unaacha madhara.
Mfano mtu anaweza kurushiwa mshale ya kumfanya aisaliti ndoa yake lakini katika usaliti huo hata akipona dhambi hiyo lakini inaweza kumwachia magonjwa au kupigwa au kilema.
Mawakala wa shetani hutuma mishale kwako ili kukudhuru.
shetani kupitia mawakala wake hutuma mishale kwako ili tu kukudhuru au kukuangamiza au kukuharibia.
Ipo mishale mingi sana ya shetani inayoweza kutumwa katika maisha yako.
Unaweza ukarushiwa mshale wa magonjwa, ukikupata mshale huo hakika utakuwa unasumbuliwa sana na magonjwa.
Wachawi wanaweza kukurushia mishale ya ya mikosi na balaa.
Waganga wanaweza kukurushia mshale wa kukataliwa.
washirikina wanaweza kukurushia mishale ya kuachika tu kwenye kila uchumba wako kila ukipata uchumba.
Ipo mishale mingi sana hutumwa katika ulimwengu wa roho ili kukudhuru.
Unaweza kurushiwa na wachawi mshale wa kukufanya uwe tasa au mgumba.
Unaweza kurushiwa mshale wa kukufanya nguvu za kiume zisifanye kazi katika ndoa yako.
Hata mtu kutoa rushwa ili akukandamize kwenye haki yako huyo ni mshale wa shetani kwako, upangue kwa maombi.
Leo omba kuing'oa na kuizima mishale yote ya shetani katika maisha yako.
Waefeso 6:16 '' zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.''.

Biblia inaonyesha kwamba huwa kuna mishale yenye moto ya shetani.
Mshale ni hatari sana.
Mishale kurushwa ni rahisi sana lakini kuing'oa michale iliyoingia katika mwili ni ngumu sana.
Unatakiwa sana kuwa muombaji mzuri kila mara ili kuizima mishale yote ya shetani.

roho ya mafarakano katika ndoa inaweza kuwa ni mshale uliotumwa katika ndoa hiyo ili isiwe na amani hata siku moja.
Unaweza ukarushiwa mshale na wabaya wako wachawi ili uugue wakati wa mitihani yako ya mwisho au wakati wako wa kufunga ndoa.
Unaweza kwenda kwenye usaili wa kupata kazi lakini siku hiyo ukashangaa midomo yako imeshikwa na hata ukiulizwa swali hujibu vizuri, kumbe kuna mtu anaitaka ajira hiyo unayoitaka wewe, amekuendea kwa waganga na umerushiwa mshale wa kukufelisha katika kila usaili, leo umeijua siri liite jina la YESU KRISTO na iite damu ya YESU KRISTO ya uzima.
Usiwe mtu wa kulalamika bali uwe mtu wa kuomba kwa MUNGU.
Kuna ahadi ya MUNGU kwa wanaoomba maombi na wanaishi maisha matakatifu katika KRISTO.
MUNGU anasema; 

 '' Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri,  Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe.  Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. -Zaburi 91:5-8 ''

Kama wewe ni muombaji hakika hutaogopa mishale ya wachawi ya usiku hata mishale ya mchana.
Ugonjwa wako unaokutesa unaweza kuwa ni mshale uliorushiwa na mashetani.
Ugonjwa ni mshale, kuonewa ni mshale, kunyanyasika ni mshale, uharibifu katika maisha yako ni mshale.
Leo ng'oa mishale yote ya maadui zako kwa jina la YESU KRISTO.
Leo zima mishale yote ya shetani katika afya yako, kazi yako, uchumi wako, izime kwa jina la YESU KRISTO.
Ita mishale ya BWANA ili uwapige wewe wachawi wanaokusumbua.
Ita mshale wa BWANA YESU ili kuwaharibu wakuu wa giza wanaofuatilia maisha yako.
Ita mshale wa MUNGU ili kuvipiga vikao vya wote wanaokujadili kwa siri kwa mabaya.
Mfalme Yehoashi wa Israeli alijulishwa na nabii Elisha  juu ya mshale wa MUNGU unavyoweza kumshindia katika vita na akashinda vita dhidi ya washami.

2 Wafalme 13:15-17 '' Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza.''

Leo ng'oa mishale yote iliyowahi kutumwa katika maisha yako, ing'oe kwa jina la YESU KRISTO.
Jifunike kwa damu ya YESU KRISTO pande zote na katika vitu vyako vyote kisha wawekee mipaka maadui zako ili wakirusha mishale yao haitakupata maana mishale ya shetani haiwezi kupenya katika damu ya YESU KRISTO. Kisha warudishie mishale yao ili kwa kiwango kile kile cha ubaya walichokikusudia kwako basi kiwapate wao. Ita mshale wa MUNGU ulio katika jina la YESU na katika damu ya YESU kisha utume mshale huo kwa maadui zako katika ulimwengu wa roho ili kuwavunja, kuwaharibu, Kuong'oa mishale yao na kuwaangamiza. Baada ya hapo panda ufalme wa MUNGU katika ukoo wako na familia yako.
Jenga utakatifu katika maisha yako na mwite BWANA YESU kila siku ili akupe ushindi.

'' angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.-Yeremia 1:10 '' 

Leo mishale yote ya shetani iliyotumwa katika maisha yako itang'oka kwa imani kwa maombi yako kwa jina la YESU KRISTO aliye hai milele.

 MUNGU akubariki sana kama unanielewa pia naomba mimi Peter Mabula nikushirikishe jambo moja hili ambalo limekuwa ndani yangu kwa muda mrefu. Nataka niwe nachapisha vitabu vitatu kila mwaka, nimeandaa masomo mengi sana na namshukuru ROHO MTAKATIFU ambaye hunipa masomo kila leo, niliyowahi kuandika mitandaoni ni sehemu tu ndogo ya masomo hayo japokuwa hadi kufika leo nimeshaandika masomo 502 ambayo nimeyaandaa kwa miaka 4.Naomba ndugu yangu unichangie mchango wa hiari wa kiwango chochote ili kufanikisha kuchapisha vitabu 2000 tu vya kuanzia ambapo nitaandaa kitabu cha maombi yenye nguvu na kitabu kingine cha ujana, uchumba na harakati za kuelekea ndoa na ndoa. Maelfu ya watu watasaidiwa na vitabu hivyo na kwa tendo hilo utakuwa umehubiri injili ya BWANA YESU pamoja na mimi na kwa MUNGU kuna thawabu kwa ajili yako maana umeipeleka injili. Ukiweza kunichangia hakika MUNGU wa mbinguni akubariki sana. Namba ya kunichangia ni hiyo moja ya tigo ambayo ni 0714252292 jina PETER MABULA, tuma kutokea mtandao wowote nitaipata pesa hiyo, namba hiyo pia huwa mwisho wa kila somo langu na ukiangalia kwenye blog yangu ya maisha ya ushindi unaweza ukafungua label juu mwanzo eneo lenye rangi ya njano na utaona masomo yangu yote zaidi ya 500 na kila somo mwisho wake ipo hiyo namba. Kama uko nje ya nchi unaweza kutafuta inbox au kwa email ili tuelekezane jinsi utakavyotuma, na kama utapenda kunitumia kwa Bank nitafute pia inbox nitakutumia account namba na utanitumia. Pia ukitaka maelezo zaidi kabla ya kutuma unaweza kunipigia kwanza kwa namba hiyo hiyo na MUNGU akubariki sana.
Baada ya maombi ya kutubu omba maombi haya.

MAOMBI YA KUIZIMA MISHALE YOTE YENYE MOTO YA SHETANI.

JEHOVAH MUNGU uliye hai pokea sifa heshima na utukuzwe milele MUNGU wa pekee..
Ninakushukuru MUNGU wangu kwa uzima wa ajabu ulionipa, ninakushukuru BWANA kwa upendeleo na ulinzi ulionipa.
Niko mbele zako Mfalme wa mbinguni ali nipokee mahitaji yangu yote.
Nashukuru kwa Neema ya KRISTO YESU inayonifunika kila iitwapo leo.
Katika jina la YESU KRISTO ninaiong'oa mishale yote ya shetani iliyowahi kuelekezwa katika maisha yangu na haijawahi kutoka,
Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninang'oa mishale yote ya magonjwa na mishale ya kuabishwa, Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninaiong'oa mishale yote ya kukataliwa na mishale yote ya mikosi,Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Mishale yote iliyotumwa ili nifeli masomo yangu,
Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Mishale yote iliyotumwa ili nisifunge ndoa takatifu, 
Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Mishale yote inayotumwa ili nifukuzwe kazi, au nishushwe cheo kazini, 
Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Mishale yote  ya kuleta umasikini na balaa, 
Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Nimekuwa mtu wa majanga sana lakini leo mshale wa majanga naung'oa  Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila aina ya mshale wa shetani unaowinda maisha yangu naung'oa na kuuteketeza kwa jina la YESU KRISTO.
Kila mshale wa shetani unaiofuata biashara yangu, kazi yangu au pesa yangu, Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila mshale unaolekezwa katika familia yangu na ukoo wangu,  Ninaing'oa kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila mshale wenye moto wa yule shetani nauzima katika jina la YESU KRISTO kama Neno la MUNGU linavyosema katika Waefeso 6:16.
Hautasalia mshale hata mmoja wa shetani uliotumwa katika maisha yangu.
Sasa nautumia Mshale wa MUNGU kuwapiga wabaya wangu wote katika ulimwengu wa roho wa giza, Niwapiga  kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Nawaponda  wachawi wote wanaonijadili usiku,
Nawapiga  kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Naharibu kila rushwa inayotolewa ili niabikie, naharibu kwa jina la YESU KRISTO. Namharibu mtoa rushwa na mpokee rushwa waliopanga nihukumiwe isivyo haki katika mahakama au katika kazi yangu, Nawapiga  kwa Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO aliye hai.
Sasa niwawashuhudia waganga wakiteswa na mishale waliyoituma wenyewe ili ije kwangu.
Sasa nitawaona wachawi wakiteseka kwa kuumizwa na mishale ile ile waliyoielekeza kwangu.
Sana kila mshirikina aliyekuwa amezoea kunirushia mshale hataweza tena kunirushia mshale wowote.
Kama wachawi na washirikina hawajawahi kunuiogopa, wakati huu wataniogopa na kunikimbia kila wanionapo.
Nakushukuru BWANA YESU maana wakuu wa giza na mishale yao wameangamia.
Asante MUNGU BABA maana umenipa ushindi wangu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Amaen Amen.


Ndugu uliyesoma ujumbe huu ubarikiwe sana.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments