MAOMBI YA KURUDISHA KILICHOIBIWA KIROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu nikujuze ujumbe wa Neno la MUNGU.
 Mwanzoni mwa wiki hii nikiwa katika maombi nilisikia sauti ikisema niombe juu ya kurudisha vilivyoibiwa na mawakala wa shetani kipepo na nifundishe pia somo ili watu waombe kurudisha vitu vyao vyema vilivyoibiwa kiroho, Nikapewa Andiko la Isaya 42:22.

Karibu sana.
Isaya 42:22 ''Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.''

Japokuwa mtu anaweza kujiona yuko sawa tu lakini Biblia inasema kwamba kuna watu hata kama watajiona wako sawa lakini kiroho wanaweza kuwa wameibiwa na kutekwa na mawakala wa shetani.
Kuna watu wako katika magereza ya kiroho na kuna watu wako katika mashimo waliyotegewa na mawakala wa shetani.
Ndoa inaweza kuibiwa kiroho na mawakala wa shetani ndio maana ndoa hiyo haiko hai tena, ina vita na kusalitiana tu, ina maumivu na majuto makubwa sana.
Uchumba unaweza kuibiwa na shetani ndio maana yule yule mchumba aliyesema ''Nakupenda kuliko wote''  huyo huyo anasema wakati akikuacha kwamba '' Sikupendi kuliko watu wote duniani''
Ufahamu unaweza ukaibiwa kipepo hata unakuwa huwezi kuamua vyema na huwezi kuamua vizuri katika mambo yako mema.
Kuna walioibiwa ufahamu na mawakala wa shetani na leo watu hao ni vichaa maana ufahamu wao mzuri wameondolewa.
BWANA YESU leo anataka atende jambo jipya la kurudisha kitu chako kizuri kilichoibiwa kiroho, BWANA anangoja tu useme ''Narudisha vitu vyangu vilivyokuwa vimeibiwa, navirudisha kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.''
Unaweza kuwa unaibiwa hata mshahara wako kipepo ndio maana japokuwa mshahara wako ni mkubwa sana lakini hakuna ulichofanya.

Biashara yako inaweza kuibiwa kipepo, japokuwa una juhudi sana katika Biashara yako na una mtaji mkubwa lakini hujaona faida kabisa, na wenye mitaji midogo na juhudi ndogo ndio unawaona wanafanikiwa tu huku wewe mafanikio yako yameibiwa.
Mafanikio yako yanaweza kuibiwa kipepo.
Uzao wako unaweza kuibiwa kipepo ndio maana hupati mtoto.
Biblia inasema '' wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha'' 
Inawezekana kabisa dhambi zako ndizo chanzo cha vitu vyako kuibiwa kipepo, lakini leo baada ya kutubu toba ya kweli pambana kimaombi na jina la BWANA YESU litakupa ushindi uutakao.
Huduma yako inaweza ikaibiwa ndio maana hufanikiwi.
Kuna watu japokuwa wana kazi nzuri lakini katika kazi hizo wanaishi kama watumwa, adui ameiba haki yao.
Afya yako inaweza ikaibiwa ndio maana magonjwa ni kila siku.
Uzuri wako binti unaweza ukaibiwa kipepo ndio maana japokuwa wewe ni mzuri sana na unaishi maisha matakatifu lakini  hakuna anayetaka kukuchumbia huku umri unaenda sana.
Biblia inasema '' wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha'' 

Haki yako unaweza ukairudisha kimaombi na ikarudi kwa jina la YESU KRISTO.
Uchumi wako unaweza ukaurudisha na ukarudi kwa Damu ya YESU KRISTO.
Kuna watu wakati huu lao ni kusema tu ''Nilikuwa tajiri sana zamani'' lakini hawaeelewi pesa yao ilipoteaje.
Mtu  mmoja alipata neema ya kupelekwa mbinguni na kuonyeshwa mambo mengi ambayo kanisa linatakiwa liyatendee kazi sana. Katika maagizo hayo mojawapo aliambiwa awaambie wateule kwamba kila kitu chao walichonacho, wanachotumia au wanachonunua ni lazima sana kukiombea na kukifutia maagano ya kipepo na kukifunika kwa damu ya YESU KRISTO.
Kuna watu kitendo cha kuwa tu karibu yako kinaweza kukuletea umasikini mkubwa.
Kuna watu ukifanya nao kazi tu usipokuwa muombaji utabaki hufanikiwi huku wao wakifanikiwa.
Sio watu wote uwaonao ni wema, wengine wamembeba shetani kabisa na ukizubaa watakuachia maumivu makuu katika maisha yako.
Ndugu, kama huwa unaliona kanisa kuwa adui yako nakuomba kwanzia leo anza kuliona kanisa kama rafiki yako mkuu na nenda kanisani ukaombewe.
Kama semina na mikutano ya injili kwako unaiona kuwa si kitu napenda kukuambia MUNGU anaweza kupeleka huko hitaji lako la tangu zamani unaloombea na mtumishi huyo anayeihubiri kweli ya KRISTO atakuombea na utashangaa sana kupata ushindi.

1 Kor 15:57 '' Lakini MUNGU na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu YESU KRISTO.'' 

Changamka leo katika maombi na maombezi ili kurudisha vitu vyako vilivyoibiwa na mawakala wa shetani.
Sio kila rafiki yako ni wa baraka, uwe makini sana maana shetani anao watoto wake wanaoweza kukuibia kabisa vitu vyako kiroho.
Mume anaweza kuibiwa akili zake kichawi na akawa kazi yake ni kumpiga tu mkewe wa ndoa bila hata kosa hata moja.
Mume anaweza kuibiwa akili yake njema na kuanza kutokujali familia yake na ndoa yake, mdada wa kazini anaweza kuwa chanzo kabisa cha kumwendea kwa mganga na kumuibia ufahamu.
Leo unaweza kukuta binti mdogo anayetumika kipepo amejenga nyumba nzuri kumbe kwa pesa za kuhongwa na mume wa mtu aliyeibiwa ufahamu.
Mama uliyeibiwa mume wako kiroho naomba leo ita jina la YESU na Damu ya YESU katika maombi ili kurudisha ufahamu wa mwanzo wa mume wako.
Baba ambaye unadhani kabisa mke wako kaibiwa ufahamu na vijana wadogo, urudishe ufahamu huo kwa maombi katika jina la YESU KRISTO.
Leo kuna mambo ya ajabu sana.
Unakuta kijana aliyesema jana jioni kwamba anampenda binti na anataka kumuoa lakini leo asubuhi tu anasema hamtaki binti huyo.
Mume aliyemwambia mkewe jana usiku kwamba ''i love you so much'' lakini ni huyo huyo leo asubuhi tu amempiga mkewe na kumvuja mguu au mkono, Ni hatari ndugu zangu.
Biblia inasema '' wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha''

1 Yohana 3:22-24 ''na lo lote tuombalo(MUNGU), twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake YESU KRISTO, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo ROHO aliyetupa. ''

Naamini sana umeshajua ni kitu gani ambacho umeibiwa kiroho na mawakala wa shetani.
Kama mtaa wenu umeibiwa kiroho na wakuu wa giza kiasi kwamba mtaa mzima ni maskini tu basi rudisha leo baraka yako kwa jina la YESU KRISTO.
Kama ukoo wenu umeibiwa fahamu ndio maana kazi za wana ukoo wenu ni ulevi  na uzinzi tu basi leo omba maombi ya kurudisha.
Kama sura yako imeibiwa ndio maana hakuna anayeweza kukubali aingie katika uchumba  na wewe, basi leo kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO rudisha baraka yako.
Kama afya yako imeibiwa ndio maana kila siku wewe ni kuumwa tu basi leo kwa maombi yako irudishe kwa jina la YESU KRISTO.
Kama akili yako imeibiwa ndio maana kiwango chako cha kufaulu kama zamani kimeondoka, basi leo kwa jina la YESU KRISTO rudisha ufahamu wako na jifunike kwa damu ya YESU KRISTO.
Inawezekana una kiwanja lakini kila ukipata pesa za ujenzi vinaibuka vikwazo na pesa hiyo inapotea tu.
Inawezekana kabisa hata kiwanja huna lakini pesa unayopokea inaweza kukunua viwanja viwili lakini shetani anakuibia pato lako , leo ita damu ya YESU KRISTO ya pasaka ikupe ushindi.
Biblia inasema '' wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha'' 

 Zaburi 2:8 ''Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.''
Uridhi wako unaweza kuibiwa hivyo urudishe leo kwa jina la YESU KRISTO.
Baraka yako iliyoibiwa irudishe leo kwa maombi yako na utashinda.
Furaha ya kwenye ndoa yako au familia yako iliyoibiwa irudishe leo kwa jina la YESU KRISTO.
MUNGU akubariki sana na nakuomba unichangie mchango wako wa hiari ili niweze kuchapisha vitabu kwa ajili ya kuwafikia watu wengi zaidi. Nataka kuchapisha vitabu 2000 vya masomo ya maombi kama lilivyo somo la leo na pia nataka kuchapisha vitabu vya masomo ya ujana, uchumba na ndoa. Ukipenda nichangie kwa namba yangu ambayo iko mwisho wa kila somo langu ambayo ni 0714252292 jina PETER MABULA, nichangie kutokea mtandao wowote na pesa hiyo itafika, asante pia kwa wewe uliyenichangia na unayetarajia kunichangia.
MUNGU yule ambaye mbingu ni zake(Zaburi 83:18) akubariki sana sana.
 Maombi haya naomba yamsaidie muombaji mchanga ili ajue jinsi ya kuliendea hitaji lake, na kwa muombaji mzoefu naamini kabisa baada tu ya kulisoma somo lote amejua nini cha kurudisha kwa njia ya maombi na ataomba mwenyewe bila kutegemea maombi haya.

 MAOMBI YA KURUDISHA VILIVYOIBIWA.

BABA wa mbinguni hakuna kama wewe.
Asante kwa kunilinda na kunipa nafasi hii ya kuomba mbele zako maombi utakayoyajibu wewe MUNGU Muumbaji wangu.
Katika jina la YESU KRISTO aliye hai ninarudisha mali zangu zote zilizoibiwa kipepo na majini, wachawi, washirikina, wakuu wa giza na waganga wote.
Ninairudisha afya yangu njema ya kuishi bila kuumwaumwa, Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninarudisha furaha iliyopotea katika ndoa yangu,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha uchumba wangu uliokuwa unaelekea katika ndoa takatifu,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninarudisha mipango yangu mizuri ili ianze kutekelezeka,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha mani katika ndoa yangu au uchumba wangu,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha pesa zangu ambazo huibiwa kichawi na mawakala wa shetani,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha kuelewana katika ukoo wangu au familia yangu,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha amani kwa wazazi wangu wasioelewana,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha kupendwa na kukubaliwa kazini kwangu,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha ujuzi wangu ulioibiwa na shetani,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha kila baraka yangu iliyokuwa imeibiwa,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Narudisha kila mali yangu iliyokuwa imeibiwa,Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ujasiri wangu wa KiMUNGU uliokuwa umeibiwa naurudisha leo kwa jina la YESU KRISTO.
Huduuma yangu iliyokuwa imeipiwa, Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila kilicho changu ambacho ni baraka kutoka kwa MUNGU na adui wameiba, Narudisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kwa jina la YESU KRISTO nawatuma malaika wa MUNGU ambao hufanya kituo kwa wamchao MUNGU kama inavyosema Zaburi 34:7 waende wakakusanye kila baraka yangu iliyokuwa imeibiwa na mawakala wa shetani.
Nawatuma Malaika wa MUNGU ambao ni roho watumikao kama inavyosema Waebrania 1:14, Nawatuma wakalete kila baraka yangu iliyokuwa imeibiwa.
Asanye JEHOVAH mwenye nguvu kwa kunishindia.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi,
Amen Amen.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments