VIJANA KATIKA HARAKATI ZA KUPATA WACHUMBA.

 Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


VIJANA KATIKA HARAKATI ZA KUPATA WACHUMBA.

BWANA YESU atukuzwe sana.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Mithali 31:10A '' Mke mwema, ni nani awezaye kumwona?''
Mwanaume anayetarajia kuingia katika uchumba anaweza kujiuliza kwamba ''Mke mwema nitamjuaje?''
Mwanamke anayetarajia kuingia katika uchumba naye anaweza kujiuliza '' Mume mwema nitamjuaje?''

Huwa kuna maswali mengi sana katika kumjua mwanamke anayefaa kuwa mke.
Huwa kuna maswali mengi sana katika kumjua mwanaume anayefaa kuwa mume.
Leo sikuchagulii mtu anayetakiwa kuwa mchumba wako ila kazi yangu ni kukufundisha wewe unayetarajia kuingia katika uchumba au una mchumba kisha unatarajia kuingia katika ndoa.
Binti au kijana unatakiwa uwe msafi kiroho na kimwili wakati wote, hiyo itakusaidia Kuolewa au kuoa mapema na katika usahihi.
Kijana au Binti naomba ujue kwamba Uchafu unaweza kuwa ni kitu pekee kwako kuwafukuza wachumba.
Mithali 30:12 ''Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao.'' 

Dawa ya uchafu wa kimwili ni kuoga na kuamua kuwa msafi kila muda.
Dawa ya uchafu wa kiroho ni kuamua kuishi maisha matakatifu.
Mara nyingi watu husema tu shetani lakini sio mara zote shetani anakuwa kizuizi cha wewe kuolewa au kuoa.

Binti kukubali kushikwashikwa na wavulana ni kuwafukuza wachumba kutoka kwa MUNGU.
Kuna vijana hata huenda kwa waganga ili akimshika tu binti basi huyo binti amkubali yeye.
Ewe mwanamke usikubali kushikwa shikwa na wanamume, utakosa mchumba bure.
Kuna mabinti wakiwa mitaani au kazini mara washikwe makalio mara washikwe matiti n.k

 lakini wao huona kawaida tu kumbe tendo kama hilo ni la kipepo na linaweza kukupa mkosi mzito wa kutokupata mchumba kamwe.
Sijui wewe binti uliyeokoka kama umewahi kuomba maombi ya kufuta alama zote za kipepo zilizowekwa katika mwili wako.
Nimewahi kuandaa somo linaloitwa MAOMBI YA KUFUTA KILA ALAMA YA KISHETANI, unaweza ku-search kwenye blog yangu ya maisha ya ushindi au google na utaliona maana somo hilo lina maombi pia ya kukusaidia jinsi ya kuomba kufuta alama za kipepo mwilini mwako.
Ndugu yangu, kijana anaweza kutaka kuachana na wewe kwa sababu ambazo anazijua yeye kisha kabla ya kuachana anakuendea kwa mganga na kuja kukushika ili usipate mwingine ila yeye na yeye wakati huo hakutaki, ziko hila za shetani nyingi mno ila ninachokuomba binti au hata kijana kukataa kushikwa shikwa. wewe sio mpira kila mchezaji ana ugusa. wewe ni mtu wa thamani na unatakiwa ujiheshimu na ujitunze, tunza ubinti wako na MUNGU atakupa mume mwema.
Kuna mikono hukushika na kukuachia maagano ya kishetani ndio maana nakuomba uwe makini sana na usikubali mwili wako kushikwa shikwa na wanaume wakware.
Kuna mikono ikikushika inakuachia maagano ya kipepo yatakayokuzuia kuolewa na mtu sahihi kwa sababu una muhuri wa shetani mwilini mwako.

Mithali  112:1-3 '' Haleluya. Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo yake. Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele. ''
 
 Kuwa mbali na YESU KRISTO ni kuwa mbali na uzima wa milele.
Shauri yako wewe uliye mbali na YESU KRISTO, hata kuokoka hutaki. Wewe kumpata mke mwema au mume mwema ni ndoto maana utachagua tu kutoka kwenye tamaa zako na ufahamu wako.


Jambo jingine ni kwamba Wasichana wengi huchelewa kuolewa wakati mwingine kwa sababu ya kujiachia sana.
Binti unakuwa mtu wa kujiachia sana kiasi kwamba kijana akifunuliwa kuhusu wewe kwa ndoto anaweza wakati mwingine akakemea akidhani ni mapepo yamemfunulia na sio MUNGU, ila kwa sababu tu ya binti kujiachia achia sana ndio maana kijana akakemea hata penye ukweli.
Binti Kujiachia maana yake ni kuwa rahisi kwa vijana wa kiume wala wakuguse, mara waone sehemu fulani ya mwili wako. Mara uonekane jinsi unavyofakamia msosi, mara uonekane jinsi ulivyo mwepesi wa kutukana. Mara kila mtu ajue kwamba hujaoga tangu juzi, mara kila mtu ajue kwamba wewe kila siku uko busy ndani ya vyumba vya wanaume. Huko ni kujiachia.
Najua kuna mtu anaelewa sasa na akimtii KRISTO na Neno lake atapona sasa.

Jambo jingine ni kwamba Mtu mwasherati hata akioa au akiolewa ni rahisi sana kutoka nje ya ndoa yake.
Vijana wa kiume na wa kike mnaotarajia kuingia katika ndoa ni muhimu sana kuwa mbali na uasherati maana roho ya uasherati ni ya shetani na huwafuatilia watu maisha yao yote kama wasipoamua kubadilika na kuanza kumcha MUNGU.
1 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.''
 
Ni ngumu kuacha uasherati kama hakuna hofu ya MUNGU ndani yako, na hofu ya MUNGU itakuja tu ndani yako pale utakapoamua kuokoka. Hofu ya MUNGU itakuja ndani yako pale tu utakapoamua kuuchagua uzima wa milele katika KRISTO YESU.

 Ndugu Ikimbie zinaa maana kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe, na anaweza kupata magonjwa au maagano ya kishetani ayatakayokuzuia kuolewa au kuoa au yatakuzuia kutulia katika ndoa yako.

Jambo jingine ni kwamba Binti unayetaka kuolewa ni lazima ujue kwamba unatakiwa kuwa na usemi mzuri, unatakiwa uwe na kauli nzuri kwa wateule wenzako wa KRISTO.
Mithali 16:24 Biblia inasema ''Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; Ni tamu nafsini, na afya mifupani.''
Kama wewe binti maneno yako ni ya mkatao tu na dharau nyingi hakika jambo hilo linaweza kukukosesha mchumba sahihi.
Ili upate mchumba sahihi na mtakatifu unatakiwa uwe kielelezo katika usemi, mwenendo, usafi na imani pia upendo kwa watu watu.
1 Timotheo 4:12 ''Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.''

 Jambo jingine ni kwamba Wewe Mteule wa MUNGU uliye na mchumba naomba utambue kwamba Muujiza wa mchumba ulioupata kwa maombi huwa muujiza huo unatunzwa kwa maombi pia.
Ukipata Mchumba sio ndio uache kuomba bali unatakiwa uongeze maombi ili adui asipande magugu ambayo baadae yanaweza kukushinda kuyang'oa na uchumba huo ukafa kabla ya kufika katika ndoa.

 Lazima wewe  mteule wa KRISTO uwe tofauti na watu wa dunia.
Fanya mambo yako kwa utakatifu na maombi huku ukimsikiliza ROHO wa MUNGU.
Watu wa kidunia huongozwa na tamaa tu za kipepo.
Mfano ni kwamba;
Baadhi ya Mabinti wa kidunia maandalizi yao ya kuolewa ni;
1.Kujichubua.
2. Kufanya mazoezi ya kucheza nyimbo za kidunia siku ya harusi yake.
3. Kutafuta wigi zuri la kuvaa kwenye sherehe ya harusi yake.
4. Kujikondesha kwa kupunguza kula ili asinenepe hadi siku ya harusi yake.
5.Kuwatambia marafiki zake kwamba yeye anaolewa muda mfupi ujao.
7. Kujiona yuko juu kuliko wanawake wote duniani.

Wewe mteule wa KRISTO usikubali kuwa kama watu wa kidunia.
1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.'

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments