UKIZINGATIA MAMBO YA MUNGU UTAKUA KIROHO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mwili Haujengwi Kwa Tofali Bali Kwa Chakula Bora. Hata Kukua Kwako Kiroho Kutajengwa Tu Na Neno La MUNGU, Hivyo Ukilisahau Neno La MUNGU Utakufa Kiroho Bure Ndugu. 
 Yohana  6:27 ''Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, MUNGU.''

Neno la MUNGU ndilo chakula cha uzima kidumucho milele.
YESU KRISTO hutoa chakula cha uzima ambacho ni Neno lake.
Elimu za kidunia na mambo ya kidunia ni vyakula vya kuharibika tu baada ya muda, Ndio maana Biblia inakushauri kwamba usikitendee kazi chakula chenye kuharibika bali kitendee kazi chakula cha uzima ambacho kiko kwa BWANA YESU tu, chakula hicho ni Neno la MUNGU.
Nakuomba Sana Liishi Neno La MUNGU, Jifunze Neno, Litafakari Neno Na Kubali Kuongozwa Na Neno La MUNGU.

Waefeso 5:15-18 '' Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya BWANA. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe ROHO;'' 

Wengi wanatamani kukua kiroho lakini imeshindikana kwa sababu siku zote wao wanakitendea kazi chakula chenye kuharibika.
Unakuta mtu kanisa yupo lakini anachelewa kufika na anaondoka kabla ibada haijaisha, kwenye disko yupo, kwenye mpira yupo, kwenye kucheza magemu yuko, beach yuko na bado mtu huyo ni anafanya kazi inayomwingizia kipato ili kuendesha maisha yake. Mtu kama huyo kukua kiroho ni vigumu sana.
Mtu anayependa kukua kiroho anatakiwa afanye kazi na baada ya kazi ni mambo ya MUNGU na sio kwenda bar na vijiweni.
Ni vizuri sana kuhakikisha unaugawa muda wako kwa mambo mawili tu yaani kazi yako njema ya kipato chako na kisha mambo ya MUNGU na sio vinginevyo.
Ngoja nikupe mfano; Mimi nafanya kazi  lakini baada ya kazi naenda kanisani na baada ya kanisani naandaa masomo na kuomba. Kwa wiki nzima ni alhamisi pekee ndio sina kipindi kanisani.
Najua sijafika ndio maana kila iitwapo leo natamani nikue kiroho zaidi. Hata wewe ndugu yangu weka mikakati ya kuhakikisha unakua kiroho. Kuna faida nyingi mno za wewe kukua kiroho.
Mambo yasiyo ya lazima unatakiwa uyaache ili kutoa nafasi ya kujifunza Neno la MUNGU.
Mambo yasiyo na faida kwako achana nayo na badala yake tumia muda huo kwenye semina za Neno la MUNGU au kanisani.
Disko au kilabu usiende kabisa maana huko utatoka tu na mapando ya shetani na sio vinginevyo, jifunze kwa mchungaji wako maana yeye huwezi kumkuta bar wala disko.
Beach nenda lakini sio kila siku.
Lakini pia kumbuka kwamba tuko duniani kwa muda tu hivyo ni muhimu sana kuutumia muda wako vizuri na kwa utukufu wa MUNGU.
Kuna watu unaweza kukuta 50% ya muda wao wanautumia kazini, ni sawa kabisa lakini 50% iliyobaki badala ya kuitumia kwa MUNGU wao wanaitumia vijiweni au popote ambapo ni barazani pa wenye mizaha.
Zaburi 1:1-3 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. ''

Sisi Tuliumbwa Na MUNGU Kwa Ajili Ya MUNGU; Kumwabudu Na Kumtumikia, Na Si Vinginevyo. 
Kama Humwabudu MUNGU Na Humtumikii Katika KRISTO YESU Anza Leo Maana Kusudi La MUNGU Kukuumba Wewe Ni Ili Umwabudu Na Umtumikie.
Zaburi 29:2 '' Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.''

 Ndugu inawezekana umepoteza Nguvu Zako Nyingi Sana Kwa Shetani Na Bado Jehanamu Inakungoja, maana hujaamua kutubu. Je, Kwanini Usibadilike Kwa Kuamua Kumpokea BWANA YESU Na Kuokoka Na Kuanza Kuishi Maisha Matakatifu?

Yohana 3:17-18 '' Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

 Kuna Watu Huenda Kanisani Na Umaarufu Wao Na Umaarufu Wao Huo Huwafanya Wawe Watu Wa Mwilini Tu Na Sio Watu Wa Rohoni. Ndugu, Usiende Kanisani Na Umaarufu Wako Bali Umaarufu Wako Uache Mlangoni Mwa Kanisa Na Sio Kuingia Nao Kanisani. Cheo Chako Kikubwa Serikalini Usiingie Nacho Kanisani.
 Ulianza Na BWANA YESU, Je Utamaliza Na BWANA YESU?. Ndugu, Ni Muhimu Ukianza Na BWANA YESU Maliza Na BWANA YESU kwa kumtii na utakatifu halisi.

Wakolosai 2:6-8 ''Basi kama mlivyompokea KRISTO YESU, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO.''

Ndugu kwanini usimtumkie BWANA YESU?
Kwanini usiishi maisha mataktifu?
Una Afya Nzuri Sana Lakini Cha Ajabu Afya Hiyo Unaitumia Kwa Shetani. Una Pesa Nyingi Lakini Pesa Hivyo Unazitumia Kwa Shetani. Ndugu Yangu, YESU KRISTO Anaokoa Na Ukimpokea Leo Hakika Unaokoka.
 Kile Unachokipanda Sasa Ndicho Utakachovuna Siku Ukifa. Kama Unapanda Dhambi Tarajia Kwenda Kuzimu Kisha Ziwa La Moto. Kama Unapanda Utakatifu Wa KRISTO Utavuna Kwenda Mbinguni Na Kisha Uzima Wa Milele.
1 Yohana 5:11-13 '' Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe.Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa MUNGU.''

 Wakati Mwingine Muonekano Wa Mtu Nje Huonyesha Jinsi Alivyo Ndani. Wakati Mwingine Mtu Mwenye Mapepo Ndani Yake Ni Rahisi Sana Kwa Kumjua Kwa Nje Kupita Matendo Yake.
Kataa hali ya kutumikishwa na shetani.
Kua kiroho sasa kwa kupitia kuzingatia mambo ya MUNGU.
Neno la MUNGU lipo kwa ajili yako na sio wengine, ukilijua hilo utalitii Neno la MUNGU na kupitia kulitii Neno la MUNGU utakuwa kiroho na kupendwa na MUNGU.
 Inawezekana Sana Umewaza Sana  tu Jinsi Utakavyofanikiwa Kiuchumi.
 Je, Umewahi Kuwaza Mara Ngapi Kuhusu Kuokoka Na Kuhusu Uzima Wa Milele Ambao Pekee Uko Kwa YESU KRISTO?
 Kila Mwanadamu Anajua Mema Na Mabaya. Swali Ni Kwamba, Je Unayaishi Mema Au Mabaya?
Zaburi 24:14-15 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. ''

 Jambo jingine ni hili, Sio Kila Mtu Amejazwa Nguvu Za ROHO MTAKATIFU Lakini Kila Mtu Anaweza Kujazwa Akiamua. Kwenye Kuamua Sasa Ndipo Kwenye Kasheshe Kwa Baadhi Ya Watu, Maana Kuamua Lazima Kuambatane Na Utakatifu, Kumtii KRISTO Na Kukaa Katika Kusudi La MUNGU.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments