MAOMBI YA KUFUTA VIAPO VIBAYA VILIVYOFANYIKA KWA AJILI YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la maombi ya ushindi mkuu kutoka kwa Bwana YESU.
Kiapo ni jambo la kuwa nalo makini sana.
Kuapa ni nini?
Kuapa ni kutamka jina la MUNGU katika kuthibitisha kitu.
Kuapa ni kunena maneno mbele ya watu kwamba utayafanya na kuyazingatia.
Lakini watu wengi wamenaswa katika viapo vyao.
Biblia inakataza kuapa maana wanadamu wengi hunaswa katika viapo vyao hivyo.
Yakobo 5:12 ''Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.''

Inawezekana wewe umezoea kuapa bila kutimiza kiapo chako, ni makosa makubwa sana.
Inawezekana wewe umewahi kuapa na kulitaja jina la MUNGU katika kiapo hicho kumbe unataka tu kupitia kiapo hicho udanganye watu wa MUNGU, hiyo inaweza kukuletea madhara makubwa baade maana unaweza kuwaficha wanadamu lakini sio MUNGU.
Dada mmoja wa kanisani alikuwa na tabia ya uasherati na kuwa kero kubwa kwa kanisa.
Mchungaji wake alimuonya sana lakini yule dada alikuwa anawadharau watumishi wa MUNGU kwa kuendeleza uasherati wake. Siku moja alitoka kuzini na taarifa zikamfikia mchungaji wake na mchungaji kumwita ofisini dada huyo. Alipofika ofisini yule dada akaulizwa na Mchungaji ''Je umefanya uasherati tena?'' Yule binti akasema ''Wala sijafanya uasherati wowote, watu wananisingizia'' Mchungaji akamuuliza tena hebu nihakikishie kama kweli hujafanya dhambi hiyo mbaya na inayolitafuna kanisa'' Yule Binti akajibu ''Haki ya MUNGU sijafanya uasherati''. Mchungaji akamwambia basi nenda maana umeapa kabisa hivyo huna hatia maana umetuhakikishia kwamba hujafanya uasherati. Miaka ikapita na yule dada ikafika kipindi anataka kuolewa. Wakati huu sasa laana aliyoivuna kutoka kwenye kuapa kwa uongo ndipo ilianza kufanya kazi. Binti alikuwa mzuri sana wa sura lakini wakati alipotaka kuolewa vijana wote walimkataa na kumuona hafai. Binti yule alijaribu sana kufunga na kuomba na kuombewa sana lakini laana ile haikutoka hadi alipotambua kosa lake ndipo aliporudi katika madhabahu ile ile na kumweleza ukweli mchungaji kwa habari ya dhambi ile na kiapo chake cha hila. Mchungaji alimuombea kwa MUNGU na ndipo Bibti yule akafunga ndoa lakini kwa sababu ya laani ile iliyozaliwa na kiapo ilipita miaka zaidi ya 5 akitafuta mwanaume wa kumuoa lakini hakumpata hata mmoja na hakumpata hata wa kumtongoza tu. Ndugu yangu Biblia inasema kwamba;
'' Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.-Mathayo 5:36-37 ''

Inawezekana wewe umezoaea kuapa bila kutimiza kiapo chako lakini leo naomba utambue kwamba kiapo ni kitu kinachomfunga mtu.
Kazi nyingi katika serikali zinaambatanishwa na viapo kwa sababu wanajua viapo vina nguvu sana na viapo huwafunga wahusika.
Kuna viapo vizuri na vibaya lakini leo nataka ufute viapo vyote vibaya ambayo umejinenea wewe au vile ulivyonenewa na wachawi au watu wabaya.
Lakini naomba pia utambue kwamba kama uliapa kufanya jambo fulani la ki MUNGU kwa kanisa au kwa watumishi wa MUNGU na ukapotezea basi nakuomba utubu kwa MUNGU na ukatimize kiapo hicho maana hicho kiapo kitafutika kwa wewe kutimiza kiapo chako.
Kuna mtu unakuta mbele ya kanisa anaahidi labda kujenga nyumba ya mchungaji, tena anaapa kabisa mbele ya kanisa kwamba atafanya jambo hilo lakini baadae anashindwa kutekeleza jambo hilo. Ndugu kama uko wa namna hiyo naomba ujue kwamba MUNGU hadhihakiwi hivyo tubu na katende kipo chako ndipo utakuwa huru.

Hata wachawi na waganga huapa ndipo wanaanza kutekeleza ushetani wao ndio maana nimesema kwamba kuna viapo vizuri na vibaya.
Kuna viapo inawezekana waliapa baba zako au babu zako zamani kwa ajili ya uzao wao ambapo uzao huo na wewe ni mhusika, hivyo kwa maombi ya jina la YESU KRISTO Mfalme wa uzima unaweza kuomba kufuta viapo hivyo kama vimekukamata hata husongi mbele.
Usiape kitu ambacho huna uhakika nacho maana kitakufunga kipao hicho hadi ukitimize.

Walawi 5:4-6 ''au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo; kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa; naye atamletea BWANA sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake.''

Maandiko haya yanatuonyesha ukubwa wa kiapo maana watu zamani walipokuwa wanajigundua kwamba wameapa kimakosa basi ili viapo vyao vifutwe iliwapasa kutoa sadaka nzuri kwa ajili ya kufuta viapo maana viapo huwafunga wahusika.
Inawezekana kwako kuna mambo yamegoma kwa sababu tu ya viapo vyako ulivyoapa zamani.
Inawezekana wewe huzai kwa sababu tu ya mtu mbaya aliapa katika madhabahu za kishetani ili kiapo hicho kikunase.
Ndugu Damu ya YESU KRISTO ipo na jina la YESU KRISTO lipo hivyo ni nafasi yako kuomba leo.
Inawezekana kabisa hali uliyonayo mbaya sasa ni kwa sababu ya viapo vyako mbele ya MUNGU ambavyo uliviapa bila kutekeleza.
Inawezekana kabisa wewe umezoea kwenda kwa waganga na hao siku zote wanajua maghara ya viapo ndioo maana wanapenda sana kukuapisha na viapo hivyo vya waganga ndivyo vimegeuka mikosi kwako na balaa, Ndugu ni zamu ya Maombi sasa ndipo utapona kutoka katika kifungo cha viapo vya kipepo.
Biblia inakataza kwenda kwa waganga.
Biblia inakataza kuapa kwa vitu ambavyo huna uhakika navyo hata kama vitu hivyo ni vyema.

Hesabu 30:2-5 ''Mtu atakapomwekea BWANA nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake. Tena mtu mke atakapomwekea BWANA nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aketi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake; babaye naye akasikia nadhiri yake, na kile kifungo chake alichofungia nafsi yake, na babaye akamnyamazia; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichofungia nafsi yake kitathibitika.Lakini kama huyo babaye akimkataza siku hiyo aliyosikia; nadhiri zake ziwazo zote, wala vifungo vyake alivyoifungia nafsi yake havitathibitika; na BWANA atamsamehe, kwa kuwa babaye alimkataza''

Ndugu usipende kuapa apa tu bila kujua maana itakugharimu baadae.
Usikubali kuapa kiapo kama ni cha kipepo.
Usikubali kuapa kiapo kibaya.
Usiape kiapo kama huna uhakika nacho.
Kuna watu waliaapa kutegemeza kazi yake au kutegemeza watumishi wake. Baada ya muda MUNGU aliwabariki pesa ili watimize viapo vyao katika kazi yake MUNGU lakini watu hao baada ya kubarikiwa waliendelea na mambo yao hivyo wamejiletea laana, mikosi na majanga kwa sababu hawakutumiza viapo vyao.
Kama uliapa kufanya jambo la ki MUNGU hakika unatimiza kipo chako. Muombe MUNGU BABA akubariki ili utimize kipaoo chako ndipo utakuwa huru.

Zakaria 8:17 '' wala mtu wa kwenu asiwaze mabaya moyoni mwake juu ya jirani yake; wala msipende kiapo cha uongo; maana hayo yote ndiyo niyachukiayo, asema BWANA.''
Inawezekana uliapa ili kuwafurahisha kanisa.
Inawezekana uliapa ili upigiwe makofi mengi.
Ndugu yakupasa utimize kiapo chako.
Leo naomba uombe mwenyewe mambo yafuatayo;
1. Omba toba kwa ajili ya viapo ulivyoapa kwa kazi ya MUNGU kisha timiza kipo chako kwa kutoa hicho ulichoapa.
2. Futa viapo vyote ambavyo waganga ana wachawi au watu wabaya wako waliapa kwa ajili yako.
3. Futa viapo vyote ulivyoapa wewe bila kujua.
4. Jifue kutoka viapo vya kishetani vyote.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments