VIUMBE VYA KICHAWI

Na Askofu mkuu Dk Josephat Gwajima.
Mungu ameshatupa kila tunachohitaji lakini yupo anayezuia ambaye anawakala wanaofanya kazi zake, shetani ndiye anayezuia mafanikio yetu, hakuondoka mbinguni bila kupigwa kwa vita na amekuja hapa duniani akiwa mwenye hasira akatengeneza utawala wake, wanaomtumikia shetani wanaitwa “mawakala wa shetani” ambao ni mapepo, mashetani, wachawi, viumbe wa kichawi, wasoma nyota, wapiga ramli, washirikina na wengine wengi hao ndio wanaofanya matakwa ya shetani hapa duniani na kuzuia Baraka za watu. Ukitaka kushughulika na shetani lazima upambane na mawakala wake wanaomsaidia kama wakala wake. Hakuna kifo, ugonjwa, kukataliwa, umaskini, mikosi na balaa pasipo kuwa na chanzo cha kiumbe wa rohoni.
“Usimwache mwanamke mchawi kuishi.” Kutoka 22:18
Zipo sababu za kimwili nyingi ambazo chanzo chake huanzia rohoni na viumbe wa kichawi, unaweza ukaambiwa unatakufa kwasababu ya magonjwa, au kwasababu ya njaa au ajali n.k sio ukweli na uhalisia na hutakiwi ukubaliane nao fahamu wapo viumbe wa kiroho wanaosababisha hayo, lakini upo ulimwengu usioonekana unaosababisha hayo. Mungu ametupa mamlaka ya kukabiliana na viumbe hawa kwa jina la Yesu. Mungu naye yupo lakini hatuwezi kumwona kwa macho kwasababu yupo kwenye ulimwengu wa rohoni hivyo amewaweka wakala wake ambao ni wachungaji, Maaskofu, manabii, mitume nk ambao wanafanya mapenzi ya Mungu kwa mamlaka ya jina la Yesu.
Ukisalimiana na mganga wa kienyeji basi umesalimiana na shetani, ukisalimiana na Mchungaji umesalimiana na Mungu. Ukimwona kiongozi lakini ni freemasonary au mchawi au msoma nyota maana yake huyo ni mwakilishi wa shetani na chochote anachokifanya anakuwa anatimiza matakwa ya shetani, ukitaka kumpiga shetani huwezi kumwona ndio umpige lakini ukipiga wale wakala wake utakuwa umempiga yeye.
Ukiwa Shuleni, kwenye familia, kwenye wizara, kwenye ukoo kila sehemu yupo mwakilishi wa shetani anayemwakilisha shetani kutenda uovu na kuwaibia watu.
VIUMBE WA KIROHO.
Vitu visivyoonekana vimegawanyika kwenye sehemu mbili, mfano bacteria wao wadogo lakini wanaweza kukaa kwenye maziwa yakawa mtindi ukanywa bila shida, kua bacteria wengine wanakaa kwenye ngozi lakini ni wazuri wanasaidia ngozi hawa ni viumbe walioumbwa na Mungu, kuna viumbe vingine kama malaika, Roho mtakatifu n.k hao hawaonekani lakini nao wameumbwa na Mungu.
Ulimwengu tunaouendea kule mbele hautakuwa ulimwengu wa kumwambia pepo toka kwa jina la Yesu, Utakuwa ulimwengu wa kutembea kuliko kawaida ya kibinadamu kwa maarifa na nguvu za Mungu.

Hakuna ugonjwa wowote ambao nyuma yake hauna kiumbe. Mfano mzuri ukienda hospitali kama unaumwa daktari anakuambia kachukue “stool” ili kiende kikapimwe ndani ya stool kuna kiumbe gani ili itumike dawa ya kumuua na upone, wakati mwingine ukienda hospitalini unajiskia uchovu daktari anachukua damu na kwenda kuipima ili aangalie ndani yake kuna kiumbe gani ameingia ili atolewe na upone.
VIUMBE WA KICHAWI.
“Ukiona kanisa limesimama ujue kuna vita vya kiroho imepiganwa.”
Ezekieli 28:13 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.”
shetani alikuwa amefunikwa na almasi na dhahabu na madini yete yalikuwa yapo kama kifuniko juu yake, wakati ule alikuwa malaika mtakatifu alikuwa amejaa vinanda ndani yake kiasi kwamba alikuwa akinyanyuka vinanda vinalia kwa mpangilio wala hakuna haja ya kupiga mziki.
Isaya 14:12-13 “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! awe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.”
Alipoasi ule uzuri wake ukageuka akawa mbaya na akaitwa Joka (Dragon) tunaanza kuona kumbe viumbe wa rohoni wanaweza kugeuza maumbo yao na kugeuka kuwa jambo lolote. Tunajifunza kwamba shetani anaweza kujigeuza akawa chochote.
Yeremia 51:20-23 “Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke;na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng'ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida.”
Maana yake shetani akiwa mwanaume tunampigwa, akiwa mwanamke tunampiga, akiwa farasi na mpanda farasi tunampiga, akiwa mzee tunampiga akigeuka akawa chochote unaweza kumpiga kwa jina la Yesu. Tunaweza kwamamlaka ya Mungu kumfuata kwenye umbo lolote na kumpiga kwa jina la Yesu.
Mungu alipomtokea Musa alimwambia aitupe fimbo yake chini nayo ikawa nyoka na akamwambia aishike kwenye mkia, alipoishika ikawa fimbo tena. Mungu alimtuma Musa aende na fimbo ile kwa Farao amwambie awaachie watu waende wakamwabudu Bwana.
Tofauti iliyokuwepo ni Yule nyoka wa Musa na wa wale wa kichawi, Nyoka wa Musa aliwameza wale nyoka wa wachawi wa farao. Tunajifunza unaweza kuona nyoka, chawa, kunguni kumbe ni wa kichawi, mambo haya yalifanyika Afrika na hata leo wachawi wanaweza kutengeneza viumbe wa magonjwa wakamwingizia mtu akaugua na kufa.
Kwenye maisha ya kila siku ukimwona kila aliyepewa talaka ameibiwa ndoa yake, kila aliyeshindwa kusoma ameibwa Elimu yake, kila aliyefilisika ameibiwa mtaji wake,kama unaona kuna mahali fulani hapako vizuri unachotakiwa kufanya usimame uwafuate waliokuiba kama Daudi na utawapata na kurudisha vyote kwa jina la Yesu.
ASILI YETU.
“Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie?Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima” Zaburi 8:4-5
Sisi ni punde kidogo kuliko Mungu.
“Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.
Lakini mtakufa kama wanadamu, Mtaanguka kama mmoja wa wakuu.” Zaburi 82:6-7

Ukiamini Neno hili kwa imani litakuwa vilevile kwasababu hapa Duniani sisi ni miungu hapa Duniani na tunamiliki vyote viendavyo juu ya nchi.
“lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.” 1 Wakorintho 2:9-14
Mungu anasema adui lazima awekwe chini ya miguu yetu. Unaposema kwa jina la Yesu unasema kwa mamlaka nah ii ndiyo siri ya mambo ya Mungu. Ukijua kwamba wewe ni Mungu hapa duniani ukatembea kama Mungu, ukaongea kama mtu, ukahukumu kama mtu mambo ya kawaida ya kibinadamu yanakufuata.
Mathayo 16:19 “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
Katika kupigana vita kinyamaza wewe maana yake Mungu amenyamaza, ukisema wewe Mungu amesema, unatakiwa uishi kama Mungu hapa duniani.
Musa alipogeuza fimbo yake mbele ya Farao, walikuja wachawi na waganga nao wakafanya vilevile.
“Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.” Kutoka 7:11-12
Ukiwa unaomba kama unamjua mchawi au mshirikina anayekuzuia usifanikiwekwenye mtaa wako unamtaja jina na kumfyeka kwa jina la Yesu kwasababu unazo silaha za Bwana, unao upanga wa roho na wewe ni rungu la Bwana na silaha za Bwana za vita.
“Kwa jina la Yesu kwenye ulimwengu wa roho ninafanya vita na walioniwekea mikosi kwa jina la Yesu, Kwa jina la Yesu kuanzia leo viumbe wa kichawi walioharibu afya yangu na maisha yangu ninawaharibu kwa jina la Yesu”.
Waefeso 6:17-18 “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”
Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
Pepo au jini anaweza kuwa kiumbe akaja kuingia ndani yako na kuwa ugonjwa, kufunika uso au kupindisha mgongo, au kuharibu akili yako unachotakiwa kufanya kwanza ni kujua kuwa wewe ni Mungu hapa duniani unayo mamlaka ya jina la Yesu juu ya viumbe wote hapa duniani. Ukifahamu asli yako kuwa wewe ni nani na ukaamua kuishi maisha ya kupigana vita vya kiroho utapata mafanikio makubwa kwenye kila utakachofanya kwa jina la Yesu Amen.

Comments