BINTI ANAYETAKA KUOLEWA NA KIJANA ANAYETAKA KUOA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ngoja niseme machache kuhusu mabinti wanaotamani kuolewa au wanahitaji kuolewa na vijana pia.

Esta 2:17 '' Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti.''
Andiko hilo linatufundisha mambo mengi sana.
Esta akapendwa kuliko mabinti wengine wote, unadhani kwanini ?
Kumbuka kwamba walikuwa wamechaguliwa mabinti wengi sana warembo sana kutoka kila mahali ili tu mmoja kati yao aolewe na mfalme. Inawezekana walizidi hata Elfu moja idadi yao, maana walikusanywa kutoka kila wilaya katika nchi ile.
Katika kundi lile la mabinti bikra Esta ndiye alipata kukubalika na kuolewa.
Esta aliyeokoka akapata kibali cha kuolewa na mfalme.
Inawezekana mabinti waliookoka walikuwa ni wengi tu kwenye kundi hilo la mabinti lakini Esta ndio aliolewa.
Mabinti warembo na wachangamfu walikuwa wengi kuliko Esta lakini Esta kuna vitu aliwazidi machoni pa Mfalme ndio maana yeye akaolewa na Mfalme.
Jamii ya Esta ilikuwa masikini tena ni watumwa hivyo inawezekana mabinti kutoka familia za kitajiri na waliosoma walijipa nafasi kubwa za kupendwa na Mfalme.
Esta alikuwa mkimbizi katika taifa lile maana yeye alikuwa Myahudi lakini sifa hiyo mbaya ya kibinadamu haikusababisha Esta asiolewe na Mfalme Ahasuero.
Kuna vitu ambavyo Esta aliwazidi warembo wote katika taifa lile waliotaka kuolewa na Mfalme.
Esta kulingana na andiko hilo la Esta 2:17 ni kwamba alipata
1. Kibali machoni pa Mfalme.
2. Neema machoni pa Mfalme.

Mambo hayo ni muhimu sana kwa kila binti kujifunza leo ili apate nafasi ya kuolewa na kijana fulani.
Kuna watu hudhani uzuri wao ndio utawafanya waolewe lakini hao hao wazuri sana ndio leo wanahaha kutaka kuolewa lakini imeshindikana.
Ndoa ni jambo la kiroho na sio kimwili, binti akijua hilo itamsaidia sana kuifikia ndoa njema.
Ukitaka kuifanya ndoa iwe suala ya kimwili itakusumbua sana.
Uzuri tu hautoshi kukufanya uolewe bali ni lazima uwe na kibali kwa huyo anayetaka kukuoa.
Uzuri tu hautoshi kumleta mume mwema kwako bali utakatifu na adabu njema na kibali.
Biblia inasema Mfalme akampenda zaidi Esta kuliko mabinti mabikra wote katika taifa.
Sasa wewe hata ubikra tu haukuhusu, utakatifu hata hauko kwako, adabu njema ndio hata hufanani nayo.
Umebakiza tu kubadili nguo fupi na kubadili mawigi.
Kuna watu wamejaribu sana hata kujichubua ili wapendwe lakini na dhambi yao hiyo wala haikuwasaidia kuolewa.
Ndugu ili uolewe kunahitajika kibali na neema machoni pa huyo anayetaka kukuoa.
Unadhani kwanini upate kibali machoni na sio moyoni? Ni kwa sababu wanadamu tunaangalia kwa macho na sio kwa moyo.
Kibali ni hali ya mtu kupata upendeleo fulani au ni neema kwa watu.
Ili upate mume mwema kutoka kwa MUNGU ni lazima kwanza uwe na kibali.
Kama huna kibali hata kama ni mzuri kiasi gani vijana waoaji watakupita bila hata kukusemesha lolote.
Biblia inakushauri kwamba
'' Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu. Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.-Mithali 3:3-7 ''

Kwa njia hiyo tunaweza kujua kwamba kibali hupatikana kwa kufanya yafuatayo;
=Maisha ya wokovu ya utakatifu kwa MUNGU.
=Uaminifu na unyenyekevu kwa MUNGU.
=Roho ya kumcha MUNGU.
=Usafi.
=Roho ya kusamehe na kuachilia.
=Kumtii MUNGU kwa njia ya KRISTO YESU.

Lakini pia ni muhimu tukajua jambo la muhimu sana ambalo nalo huwatesa wengi yaani mipango ya shetani kukuzuia.
Inawezekana shetani anakuonea tu lakini inawezekana umefungua milango ya shetani kuingia maishani mwako na kukutesa.
Leo nataka nikusaidie kwa kukuambia yafuatayo.
Unatakiwa umpokee YESU na uanze kuishi maisha matakatifu katika yeye, kisha omba maombi ya kujifungua kutoka hila za giza juu yako.
Binti kama una roho ya kukataliwa na kuchukiwa hakikisha unafuta roho hizo kwa jina la YESU maana ni vigumu kupata kibali kama una mpangaji ndani yako aitwae roho ya kukataliwa na kuchukiwa.
Binti inawezekana hujawahi kupata kibali kwa wateule wa KRISTO wanaotafuta wachumba, omba kupata kibali.
Esta alipendwa na Ahasuero kuliko mabinti wote bikra katika taifa kwa sababu ya kibali.
Kwanini Esta alipendwa na wengine na uzuri wao hawakupendwa?
Ni kwa sababu Esta alipata kibali machoni pa Mwanaume yule.
Hata wewe ukiamua hakika unaweza kupata kibali kwa mtu ambaye atakuchumbia na kukuoa kwa utakatifu kwa sababu tu ya kibali ulichonacho.
Unadhani kwanini mabinti wengine hawakupata kibali kwa Mfalme?
Ukilijua hilo naomba sasa uombee kibali chako cha kukubalika na kupendwa ndipo itatokea nafasi ya kuvikwa taji yaani kuolewa kwa kufunga ndoa takatifu.

Ni kweli inawezekana wewe ni binti ambaye umejitunza na una adabu njema na wala huvai kikahaba lakini umepungukiwa jambo moja ambalo ni kibali.
Omba juu ya kibali chako cha kuolewa.
Usipokuwa na kibali hakika watakuja vijana wa kukuchezea na sio waoaji na hilo kwa sababu ni dhambi basi utakuwa unaendelea kujiharibia maisha yako zaidi.
Kuna watu wao wana kibali cha kipepo kwa waume za watu lakini sio kibali safi cha vijana watakatifu waoaji, hilo ni roho ya kukataliwa inawatesa.

Kibali ni kitu cha muhimu sana.
Kila jambo linahitaji kibali ndipo utalipata kwa usahihi na uzuri.
Kwa MUNGU tunahitaji kibali chake ndipo tutafanikiwa katika maisha yetu ya kiroho katika wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi wetu.
Zaburi 19:14 ''Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.''

Ndugu, ombea maneno yako yapate kibali kwa MUNGU na kwa wanadamu.
Ombea mawazo ya moyo wako yapate kibali kwa MUNGU na kwa wanadamu ndipo utakapofanikiwa na kustawi sana.
Bila kibali cha MUNGU ni ngumu sana kufanikiwa.
Bila kibali cha MUNGU ni ngumu kufanikiwa na kukubaliwa na watu.
Ndugu unahitaji kibali kutoka kwa Bwana YESU ndipo utafanikiwa sana.
Bila kibali cha MUNGU huwezi kukubaliwa.
Bila kibali cha MUNGU huwezi kuheshimiwa.
Bila kibali cha MUNGU huwezi kupata mume mwema/mke mwema.
Bila kibali cha MUNGU huwezi kupata kazi nzuri.
Bila kibali cha MUNGU huwezi kupata mapokezi mazuri rohoni kwa huyo anayetaka kukuchumbia.
Bila kibali cha MUNGU huwezi kupandishwa cheo kazini.
Ndugu unahitaji kibali cha MUNGU.
Mithali 3:4 '' Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu.''

Muombe MUNGU akupe kibali maana usipokuwa na kibali cha MUNGU utaonekana unaropoka kwa watu hata kama unaongea ukweli asilimia mia.
Mwambie MUNGU akupe kibali cha akili nzuri.
Omba upate kibali kwa mchumba wako au mchumba wako ajaye kutoka kwa MUNGU.
Bila kibali cha MUNGU utakuwa unakimbiwa tu au kuachwa na wachumba.
Hata katika ndoa nakuomba wewe mwanandoa omba MUNGU akupe kibali kwa mwenzi wako wa ndoa, usipopata kibali neno lako kila ulisemalo litakuwa linapingwa tu.
Mama omba MUNGU akupe kibali kwa mume wako.
Usipopata kibali hata uogeje na uvaeje bado kwake utaonekana takataka tu maana huna kibali moyoni mwake.
Maombi katika jina la YESU yanaweza kuleta kibali chako, changamka leo ndugu.

Mithali 28:23 '' Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake. ''
Binti unaweza ukabadili nguo kila siku lakini vijana waoaji ndio wanazidi kukuchukia kwa sababu tu shetani ameiba kibali chako. Ndugu yangu omba ili kibali chako kiwe hai na uwe nacho.
Unaweza ukabadilisha mafuta na hata ukajichubua kabisa lakini hakuna hata mwanaume mmoja anayetaka kukuchumbia kwa sababu huna kibali.
Unaweza ukajinajisi kwa mawigi na nywele bandia na kila aina za vipodozi lakini hakuna kijana hata mmoja anataka kukuchumbia kwa sababu shetani alishaiba kibali chako cha kufunga ndoa.
Utawaona wanawake wa kawaida sana na mabinti wa kawaida sana wanafunga ndoa takatifu kanisani lakini wewe imeshindikana kwa sababu tu wao wana kibali lakini wewe huna kibali.

Danieli 1:9 '' Basi MUNGU alimjalia Danielii kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi.''
Danieli alipata kibali na huruma mbele za mkuu wa matowashi.
MUNGU alimpa kibali danieli kama ambavyo anaweza kukupa kibali wewe kwa maombi yako katika jina la YESU KRISTO.
Je wewe unakibali cha MUNGU kazini kwako?
Je wewe una kibali kwa mchumba wako?
Je wewe una kibali cha MUNGU katika ndoa yako?
Je wewe una kibali kwa ndugu zako?
Kama huna kibali nakuomba sana ndugu yangu omba maombi ya kupata kibali.
Kibali chako kitaonekana kupitia maombi yako na utakatifu wako kwa KRISTO.
Mambo yote yanahitaji kibali.
Hata injili kuihubiri inahitaji kibali pia.
Warumi 15:16 '' ili niwe mhudumu wa KRISTO YESU kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya MUNGU kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na ROHO MTAKATIFU.''
Ndugu omba kibali kwa MUNGU.
Hata mimi hapa nimepata kibali kwako ndio maana unasoma masomo yangu haya niletayo kila siku.
Kibali ni muhimu sana.
Jambo lingine la muhimu sana kujua ni kwamba dhambi huondoa kibali, hilo likumbuke sana na usije ukalisahau hata siku moja.
Kataa dhambi ndugu yangu maana dhambi zitaondoa kibali chako na dhambi zitamruhusu shetani kukuibia kibali chako.
Hata kwenda mataifa mbali mbali kunahitajika kibali cha MUNGU.
Unaweza kuwa na kibali kwa eneo lako tu maana huna kibali cha kwenda nje yaani zaidi ya hapo ulipo.

Naomba pia ujue kwama sadaka yako kwa MUNGU inaweza kuleta kibali chako pia.
Wafilipi 4:18 '' Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo MUNGU.''
Sadaka yenye kibali inaweza ikabeba kibali chako pia hivyo ni muhimu sana pia kumtolea MUNGU sadaka yenye kibali.
Ukipata kibali hata hutakuwa mchoyo kumtolea MUNGU.
Kibali cha MUNGU kwako ni muhimu sana.
1 Thesalonike 2:4 '' bali kama vile tulivyopata kibali kwa MUNGU tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu.''.
Kibali cha MUNGU ni cha muhimu sana.
Hakikisha unapata kibali cha MUNGU katika maisha yako.
Omba upate kibali cha MUNGU katika maeneo yote.
Isaya 61:6 '' Bali ninyi mtaitwa makuhani wa BWANA; watu watawaiteni wahudumu wa MUNGU wetu; mtakula utajiri wa mataifa, na kujisifia utukufu wao.''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments