JE MKEO/MMEO ANATOKA KWA MUNGU?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Je huyo mchumba wako anatoka kwa MUNGU?
Je huyo mke wao au mume wako anatoka kwa MUNGU?
Maswali hayo yanatakiwa yapatiwe majibu kabla ya kuchumbiana na sio kutafuta majibu baada ya kufunga ndoa.
Usianze kutaka kujua kama huyo mumeo anatoka kwa MUNGU wakati mko tayari katika ndoa.
Usianze kutaka kujua kama huyo mkeo ni mke mwema wako kutoka kwa MUNGU wakati mko katika ndoa sasa.
Nimewahi kukutana na visa hivi mara nyingi.
Unakuta mama yuko katika ndoa na ndoa hiyo ina miaka zaidi ya mitatu tangu wafunge ndoa lakini kwa sababu tu ya vitu fulani kutokea mama huyo anaanza kuomba maombi ya kuhakiki kama huyo mwanaume ni kutoka kwa MUNGU.

 Ndugu hata kama ukijua kwamba hajatoka kwa MUNGU utafanyeje? wakati sasa wewe na yeye ni mwili mmoja na hakuna kuachana?
Ni kweli kabisa mke mwema au mume mwema hutoka kwa MUNGU tu.
Mithali  19:14 ''Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA.'' 

 Ni kweli kabisa mke mwema hatoki katika macho yako bali anatoka kwa MUNGU.
Ni kweli kabisa mume mwema hatoki katika wenye mali tu bali hutoka kwa MUNGU.
Biblia inasema wazi kabisa kwamba mali unaweza ukapewa na wazazi lakini sio mke au mume.
Ni kweli kabisa wazazi wako wanaweza wakakupa elimu nzuri kwa kukusomesha lakini mume mwema au mke mwema hutoka kwa MUNGU tu.
Mke mwenye busara hutoka kwa MUNGU.
Mke mwema hutoka kwa MUNGU.
Maandalizi ya kumjua mke mwema au mume mwema yafanye kabla ya kuamua kuchumbiana.
Ukitaka kujua mke wako au mume wako anatoka kwa MUNGU wakati uko tayari katika ndoa utakuwa unapoteza muda tu maana hutapata majibu.
Ndoa ni agano na agano hilo usipomhusisha MUNGU sana kwa maombi na utakatifu unaweza kujikuta unaingia agano na watoto wa shetani waliosaini kwenda jehanamu wakati wewe unataka kwenda mbinguni.
1 Kor 6:15-16 '' Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya KRISTO? Basi nivitwae viungo vya KRISTO na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.''

Wewe mteule wa KRISTO, ni mali ya KRISTO hivyo unatakiwa kuingia katika agano la ndoa na mtakatifu mwenzako ndipo mtasaidiana kwa mambo mema.
Biblia iko wazi ikisema kwamba mtakuwa mwili mmoja hivyo huo mwili mmoja unatakiwa kuwa nao makini sana ili usijichanganye na ubaya.
Muda wa kujua mkeo au mumeo anatoka kwa MUNGU basi ni wakati wa uchumba na sio wakati wa ndoa.

Ndugu mmoja siku moja akanipigia simu akiniomba nimuombee ili ajue kama mkewe ni mpango wa MUNGU kwake. Kwa mazingira aliyokuwepo huyo ndugu sikumkemea ila nikaanza kuombea amani na furaha katika ndoa hiyo.
Kumjua kama anatoka kwa MUNGU wakati mmeshaoana tayari ni jambo ambalo halina maana na halikusaidii kwa vyovyote.
Mke wako ni mke wako na usitake kujua kama katoka kwa MUNGU au katoka kwenye macho yako.


Mwanzo 2:24 ''Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.''


Mume wako ni mume wako tu hivyo usianze kutaka kujua kama anatoka kwa MUNGU au anatoka katika nafsi yako iliyompendea pesa na mali.

Kama ukitaka kujua kama anatoka kwa MUNGU basi naomba mtambue kwamba jambo hilo linawahusu tu ambao hawajaoa wala hawajaolewa, lakini ukiingia katika ndoa jambo hilo linakuwa halihitajiki kabisa.
Hata kama ndoa yako ina siku moja tu tangu ifungwe jambo la kutaka kujua kama anatoka kwa MUNGU halikuhusu.
Mpende mkeo na muombee ili awe kwenye utakatifu wa KRISTO.
Mpende mumeo ili awe na hofu ya MUNGU na ili ndoa yenu iwe safi.

Usijilaumu kwa kukosea kuchagua ila nafasi yako ya wakati huu ni kumuombea tu huyo mwenzi wako isipokuwa kama anakusaliti hiyo ni habari nyingine.
Kama anataka mfanye mapenzi kinyume cha maumbile usikubali na kwa hilo hata kutengana kubali kutengana naye.
Zaidi ya hayo unatakiwa umuombee sana na kumsaidia kiroho ili sasa atoke kwenye kundi la mume asiye mwema ana awe mume mwema, atoke kwenye kundi la mke uliyemchagua kwa tamaa zako tu na awe mke mwema. Inawezekama kwa maombi yako hata kama hiyo ni gharama kubwa lakini inakupasa uikabili gharama hiyo hata kama itakuletea gharama kubwa na maumivu mengi. Ni wako huyo maana ulimchagua mwenyewe.
Yakobo 5:16 ''Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.''

 Kila mtu duniani ni mtu mzuri ila tu mtu huyo kama akikubali kutengenezwa na Bwana YESU.
Ukizijua mbinu anazotumia adui yako shetani kushinda itakuwa rahisi kwako kumshinda adui huyo.
Kama unajua kabisa kwamba shetani humvamia mmeo au mkeo ndio maana anakuwa mkali na mnaanza kutukanana basi wewe ukigundua hivyo utahakikisha muda mwenzi wako amevamiwa basi wewe utajiepusha nae na kuomba. Huo ni mfano mmoja katika mifano mingi ya kuijua mbinu ya shetani kutaka kukutoa katika furaha na amani yako.


Pia maumivu makubwa zaidi ya wanandoa wanaotendwa ni kutokusamehe.
 Ndugu yangu jifiunze kusamahe maana hiyo itakusaidia maishani mwako mwote.


Wakolosai 3:18-19 "Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika BWANA. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao."

Yapo matatizo mengi katika baadhi ya ndoa mfano Japokuwa wanaume wengi kwenye ndoa huwa sio wepesi kuvumilia lakini hata wamama nao ni wengi sana wasiovumilia. 
Ukitoka tu mtindo mpya wa kusuka naye anataka pesa ya kwenda saloon, hata kama haimo kwenye bajeti. 
Wababa wengi kwenye ndoa zao wanakonda sana huku wake zao wakinenepa kwa sababu tu ya wamama kushindwa kuvumilia. Mama sio kila ukionacho basi lazima ununue. utaratibu katika familia ni mzuri sana lakini wakati mwingine utaratibu huo na wamama wakati mwingine huuvunja. 
Ndoa Ni kuvumiliana. Sio mtoto akosekane mwaka wa kwanza ndipo baba unaenda kutafuta mtoto nje ya ndoa, huo ni ushetani.
 Ni muhimu sana kuvumiliana kama wanandoa waliounganishwa ili muwe pamoja daima.
Wakolosai 3 12-14 "Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu"
  Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments