KWA NINI MIPANGO YAKO YA MWAKA HAIKUFANIKIWA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kwanza hongera kwa kuuona mwaka wa nyongeza. Kuna sababu njema za MUNGU ili wewe uishi mwaka huu, mtii MUNGU sasa na Neno lake la wokovu kwako kupitia KRISTO YESU.
 Natambua kabisa kila mtu huwa ana mipango mingi mwanzoni mwa mwaka ambayo atataka aitekeleze kwa mwaka husika.
Sio kila mipango yako hutimia lakini wakati mwingine huwa kuna sababu za kutokufanikiwa kwako.
Nilikuwa namuomba ROHO MTAKATIFU ili anifundishe masomo ya kufundisha mwisho wa mwaka. Nikapata vitu kadhaa na jambo lakini jambo la ajabu muda wa kuandika masomo wakati huo kwangu umekuwa mdogo sana ila jifunze kupitia ujumbe huu.

Zaburi 65:11 ''
Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono.''

MUNGU anaweza kuuvika mwaka wako taji ya wema na ukawa mwaka mzuri sana kwako.
MUNGU anaweza kukupa baraka nyingi katika mwaka lakini tu wakati mwingine sisi binadamu ndio huwa tunakwamisha kutimia kwa baraka zetu. Labda kwa matumizi mabaya ya muda au kwa sababu ya kuwategemea wanadamu na sio MUNGU , au kwa sababu ya kupunguza maombi na juhudi. 
Sijui ndugu kwa upande wako kwanini mipango yako mwaka  Haikufanikiwa.
Inawezekana mipango yako kuwa mingi ndiko kulikuvurugia.
Mipango mingi sio vibaya ila iwe unaimudu, mipango mingi sio mibaya ila ni lazima ujue unaanza na upi kisha unamalizia na Upi, ukivuruga utavuruga yote.


Mwaka umeisha na Inawezekana kuna baadhi ya mipango uliyopanga uitimize mwaka huo ila hukufanikiwa.
Inawezekana kabisa ulipanga mwaka huo ufunge ndoa ila hujafanikiwa.
Inawezekana ulipanga kufungua biashara lakini haikuwezekana.
Inawezekana ulipanga Kujenga ila hukufanikiwa.
Inawezekana ulipanga jambo lako zuri lolote lakini hukufanikiwa.

Ndugu yangu nakuomba usikate tamaa wala usiache kuomba na kufunga.
Usipunguze utakatifu na usikubali kitu chochote kikutenge na Mwokozi wako YESU KRISTO.

Usikubali kitu chochote kikupunguzie mwendo wa kusonga mbele na Wokovu wa YESU KRISTO.
Katika mwaka huu mpya nakuomba katika yote mtegemee MUNGU na kuliishi kusudi lake, katika yote mche MUNGU na mtegemee yeye na sio akili zako.
 Biblia inatoa tahadhari kwa wanaojitegemea pasipo kumtegemea MUNGU.
Yakobo 4:13-15 ''Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, BWANA akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. 

Baada ya hayo naomba nikujulishe yafuatayo;

JE KWANINI HUKUPOKEA HITAJI LAKO MWAKA ULIOPITA?.

1. Inawezekana hukuomba ndio maana hukupokea.

Mathayo 7:8-11 '' kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana BABA yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? ''

Inawezekana uliomba ila hukuomba kwa imani.
Inawezekana uliomba ila hukufikia kiwango.


2. Inawezekana wakati ulioamliwa na MUNGU haujafika.
 
Mhubiri 3:1 ''
Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''

Biblia inasema  kila jambo na wakati wake, hivyo Inawezekana wakati wake hilo hitaji lako kwako haujafika japokuwa mambo mengi wakati wake ni huu ila mazingira yako yanaweza kulisogeza mbele jambo hilo.
Inawezekana huu ndio wakati ulioamriwa juu ya baraka hiyo kuja kwako ila wewe ndio hujielewi.


3. Inawezekana adui zako katika ulimwengu wa roho wamekuzidi ujanja . 

Waefeso 6:11-13 ''Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.''
 
Jambo kubwa ambalo mawakala wa shetani hufanya ili usifanikiwe ni kukufunga ufahamu, ndio maana tangu January hadi  December bado hata hujui nini kimetokea.

 unaona tu mwaka umeisha haraka sana kumbe ufahamu wako ulifungwa ili mwaka huu usifanikiwe kuipata baraka yako.
Ndugu vaa silaha za MUNGU ndipo utawashinda maadui hao katika ulimwengu wa roho.
Mwaka huu usikubali kuomba kiulegevu, omba kwa juhudi.
Maisha ya utakatifu ni silaha kuu hivyo ishi maisha matakatifu.
Neno la MUNGU ni silaha hivyo litii Neno la MUNGU na litumie katika maombi.
Jina la YESU KRISTO ni silaha isiyoweza kushindwa na chochote na yeyote.
 
4. Inawezekana hukufanya juhudi katika kuifikia baraka yako.

Mithali 20:4 ''Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu.''

Inawezekana ulikuwa mvivu na mlegevu ndio maana hukupata baraka yako.
Inawezekana ulidanganywa na Marafiki zako au ndugu zako uliowashirikisha mwanzoni mwa mwaka na ulipoufanyia kazi ushauri huo ulifanyia kazi kitu ambacho kiko nje ya kusudi la MUNGU kwako.

5. Inawezekana dhambi imekuharibia. 
 
Waefeso 6:1 ''
Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ''
Moja ya vizuizi vikuu vya wewe kupokea kutoka kwa MUNGU ni dhambi zako. 
Kazi mojawapo ya dhambi ni kukufanya kuwa mfu hivyo na vitu vyako vitakuwa vifu tu.
Biblia inasema watenda dhambi ni wafu hivyo mfu hawezi kupewa baraka.
Dhambi ina madhara mengi sana na moja wapo ya madhara hayo ni kuondoa ulinzi wa MUNGU juu ya baraka yako ndio maana baraka yako ilipeperushwa na shetani.
Dhambi inaweza kuzuia baraka yako.

''Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.-Mithali 14:34 ''

6. Inawezekana uliwategemea wanadamu na sio MUNGU.


Yeremia 17:5 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.''

Wanadamu sio wa kuwategemea, mtegemee MUNGU sana.

Ukiwawekea tegemeo wanadamu wanaweza wakahama hivyo na wewe mipango yako inakufa.
Wanadamu wanaweza wakafa hivyo na mipango yako kufa.
Wanadamu wanaweza wakakugeuka hivyo ukabaki na maumivu tu huku mipango yako imegoma kwenda.
Ndugu mtegemee MUNGU sasa mwaka huu ili ufanikiwe.
 

9. Inawezekana ulinaswa kwa maneno ya kinywa chako.


Mithali 6:2 '' Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,''


Watu wengi hupenda sana kubarikiwa na MUNGU ila vinywa vyao huwaharibia.
Kuna watu hujinenea mabaya kila mara ndio maana wakati mwingine hayo wanayojinenea huwakamata.
Kuna watu huweka nadhiri kwa MUNGU juu ya kumtolea MUNGU au kutimiza jambo fulani lakini hushindwa kutimiza na jambo hilo, hiyo ni tatizo
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza na Mwakani ni wako wa kufanikiwa.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments