UJUMBE WA KINABII KUHUSU KUNYAKULIWA KWA KANISA

Na Askofu Mkuu Silyvester Gamanywa.
Kufuatia changamoto za kiimani ambazo jamii ya wanafunzi wa Yesu Kristo tunazipitia; na kutokana na matishio mbali mbali yanayotishia uhusiano wetu wa kiroho na Bwana Yesu; ni dhahiri kwamba umefika wakati wa kuzingatia vipaumbele vya imani ikiwa ni pamoja na kuzingatia ujumbe wa kinabii
kuhusu kunyakuliwa kwa kanisa la Kristo.

Mada hii inaanza kwa kuchambua maana ya misamiati wa kunyakuliwa, jinsi tukio litakavyokuwa, sababu za kunyakuliwa; na mchakato wa maandalizi ya unyakuo wenyewe. Karibuni.
MAANA YA KUNYAKULIWA
"Kunyakuliwa" ni tukio maalum la kinabii ambalo linatarajiwa kutokea wakati wowote kwa ajili ya kuhitimisha huduma za Kanisa la Kristo duniani. Tukio hili linawahusu makundi mawili ya walengwa. Kundi la kwanza ni “kufufuliwa kwa wafu waliolala mauti katika Kristo”! Na kundi la pili ni “wanafunzi halisi wa Yesu Kristo tutakaokutwa hai. Na hii ni kwa mujibu wa maandiko ya Paulo alipowaandikia Wathesalonike:
"Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo." (1 THE. 4:13-18)
JINSI UNYAKUO UTAKAVYOFANYIKA
Tukio hili la kinabii litafanyika kwa kasi na kwa kushtukiza. Hakutakuwepo na taarifa ya kujiandaa kwa unyakuo. Maandiko yanasema kwamba itakuwa ni: "kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika." (1 KOR. 15:52)
Kwa sababu ya kushtukiza kwa tukio hili la ghafla imeandikwa ya kuwa kuna baadhi waliotakiwa kunyakuliwa wataachwa kwa sababu ni kwa ajili ya watakaokutwa wako tayari tu ndio watakaonyakuliwa:
"Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu." (MT. 24:37-42)
SABABU ZA KUNYAKULIWA
Baada ya kupitia tafsiri na jinsi unyakuo utakavyofanyika, napenda tupitie hoja muhimu za sababu za kunyakuliwa. Napenda kuzielezea sababu hizi kwa sababu kuna malumbano ya kitheolojia kuhusu unyakuo na mjadala ukilenga ni wakati gani unyakuo utafanyika.
Kuna kundi lenye kudai kunyakuliwa kutafanyika kabla kuanza kipindi cha miaka 7 ya dhidi kuu (Pre-tri-rapture) ; kundi la pili linaamini unyakuo utafanyika katikati ya kipindi cha miaka 7(Mid-tri-rapture); na kundi jingine linaamini kunyakuliwa kutafanyika mwishoni mwa dhiki kuu (Post-tri-rapture)
Uchunguzi wangu na imani yangu vinaangukia katika kundi la kwanza la(Pre-tri-rapture) na ndiyo maana nimeona nitoe sababu za kunyakuliwa kabla ya kuanza kipindi cha dhiki kuu.
1. Ahadi ya Yesu Kristo
Yesu mwenyewe ndiye aliyetangulia kuwajulisha wanafunzi wake kuhusu suala la kurudi tena kuwachukua ili wakae pamoja naye mbinguni: " Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo." (YN. 14:2-3)
2. Kuepushwa na ghadhabu ya Mungu
Mtume Paulo alidokeza habari za ujio wa Mpinga Kristo na atakavyotawala chini ya uvuvio wa Shetani mwenyewe. Na Kisha akataja habari za wale watakaochwa baada ya unyakuo watakavyoingia kwenye kipindi cha udanganyifu mkubwa wa Shetani kwa sababu walikataa kuamini kweli ya Injili kabla ya unyakuo:
“Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.” (2 THE. 2:8-12)
Kwa hiyo, kunyakuliwa kabla ya kipindi cha utawala wa MpingaKristo ni ili tuepushwe na hii ghadhabu ya Mungu inayotarajiwa kuupata ulimwengu katika kipindi hicho: “Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.” (1 THE. 1:9-10)
TISHIO LA KUACHWA KAMA HAKUNA MAANDALIZI
Kufuatia tukio la kunyakuliwa kufanyika ghafla, ndiyo maana maandiko yanahimiza walengwa wa unyakuo kuwa tayari wakati wote ili wasijekuachwa wakati wa unyakuo. Na hii ndiyo sababu ya kuamini kwamba unyakuo utafanyika kabla ya kipindi cha dhiki kuu ili walengwa wawe wametimiza vigezo vya unyakuo huo wasijepatwa na mabalaa ya dhiki kuu.
Ushahidi ni maandiko yanayo tahadharisha kuwa tayari, kutubu na kuishi maisha ya utakaso kamili wakati wote: "Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo." (UFU. 21:27)
No automatic alt text available. Yesu mwenyewe aliyaonya makanisa ya Karne ya kwanza yajitakase na kujiweka tayari kwa unyakuo vinginevyo yatakosa fursa hiyo. Kwa Kanisa la Efeso alilionya akisema: "Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu." (UFU. 2:5)
Maana ya "Kuondolewa kinara" ni kufutiwa haki ya urithi wa ufalme wa mbinguni na kufutwa jina kwenye kitabu cha uzima. Mtume Paulo naye anasisitiza akisema kwa kuwa siku ya unyakuo yaja kama mwivi na itawakumba wote wasiojiandaa;akasema sisi tusikubali kubaki gizani mpaka tuvamiwe ghafla:
“Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.” (1 THE. 5:2-4)
Tutaendelea na sehemu ya pili ambapo tutapitia mchakato wa maandalizi kwa ajili ya kunyakuliwa, ni mambo gani yatakayojiri baada ya unyakuo mbinguni na nini kitaendelea duniani. Tafadhali kama ujumbe huu umekugusa nijulishe kwa ku-like ukurasa huu na kisha warushie na marafiki zako wengine.

Comments