WEWE UNA UJANJA UPI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze.
Leo nilikuwa katika kutafakari neno ''Ujanja' na nikapata ufafanuzi kwenye kamusi ya kiswahili sanifu juu ya neno hilo.
Neno ujanja lina maana kadhaa kwa mujibu wa kamusi.
Ujanja ni hali ya kuwa na hila.
Ujanja ni hali ya kuwa na udanganyifu.
Ujanja ni hali ya kuwa na unafiki.
Ujanja ni hali ya kuwa mpunjaji.

Lakini Kamusi hiyo hiyo ya kiswahili sanifu inajulisha pia kwamba.
Ujanja ni hali ya kuwa na akili.
Ujanja ni hali ya kuwa na werevu.
Ujanja ni hali ya hali ya kuwa na fahamu.

Baada ya uchunguzi huo wa maana ya neno ujanja, ikabidi nichunguze Biblia inasemaje juu ya ujanja.
Katika Biblia nzima nimegundua kwamba Neno Ujanja linapatikana katika andiko moja tu yaani Waefeso 4:14, na andiko hilo katika hiyo Waefeso 4:14 baada ya kuangalia Tafasiri zingine za Biblia nimekuta Neno hilo lina maana ya udanganyifu.
Waefeso 4:14-15 Biblia inasema '' ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KRISTO.''

Baada ya hapo nikagundua kwamba watu wengi hujiita wajanja baada ya kufanya hila fulani.
Hata kuna baadhi ya wakristo na watumishi  hujiita wajanja au hujiona wajanja baada ya kutapeli au kufanya jambo baya mbele za MUNGU na mbele za wanadamu.
Japokuwa maana ya pili ya neno ujanja ni nzuri lakini wajanja wengi wa leo huitwa hivyo au hujiita hivyo baada ya kufanya ujanja wenye mabaya ndani yake.
Ndugu, je wanaokuita mjanja ni kwasababu wameona ujanja gani kwako?
Wagalatia 5:19-21 ''Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU. ''
 Katika maandiko haya juu yanaonyesha matendo ya mwanadamu ambayo ni machukizo kwa MUNGU.
Kuna watu husifiwa au kujiita wajanja baada ya kutenda dhambi lakini ujanja huo unaweza kuwapeleka jehanamu wasipotubu.
Binti unatoa mimba kisha unajiita mjanja?
Kweli wewe ni mjanja kwa maana ya hila zako na udanganyifu wako, lakini mimi nakuambia kwamba wewe sio  mjanja tu lakini ni mjanja mjinga, tena wewe ni mjinga kabisa.
Kijana unavuta sigara, bangi na madawa ya kulevya kisha unajiita mjanja na kujitangaza kwamba wewe ni mjanja, ndugu huo ni ujanja aina ya ujinga.
Ndugu unafanya dhambi na unajiona mjanja, ndugu huo ni ujanja aina ya ujinga.
Wengine hufanya dhambi na kuwakimbia wachungaji wao ili wasiwaone, ndugu huo ni ujanja aina ya ujinga.
Kuna watu wanawachukia wanadamu wenzao na hawataki kuwasamehe, wanajiona wajanja kwa hilo, lakini mimi nakuambia kwamba huo ni ujanja aina ya ujinga, tena ni hatari kubwa kwa mtu asiyesamehe.
1 Yohana 2:11 '' Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.''

 Kama wewe unafanya dhambi na kujiona mjanja hakika naomba nikuambie kwamba ujanja wako huo haukupeleki mbinguni hakika. 
Tubu na acha dhambi.
Unasingizia watu kisha unajiona mjanja.
Unaibia watu kisha unajiona mjanja.
Unaroga watu kisha unajiona mjanja.
Unadanganya watu kisha unajiona mjanja.
Unakwepa kutoa fungu la kumi(Zaka) kisha unajiona mjanja.
Ndugu yangu, huo ujanja wako ni ujanja wa hila, udanganyifu na ni ujanja aina ya ujinga.
Ndugu mmoja alikuwa amezoea kuchukua wake za watu, siku moja alikamatwa na kuteswa sana na kupigwa sana, hiyo ni adhabu A lakini mtu kama huyo asipotubu basi kuna adhabu nyingine inaitwa jehanamu ya moto.
Mtu mmoja alikuwa amezoea kuiba na kujiona mjanja kwa sababu hakuwahi kukamatwa, lakini alipokamatwa alipigwa kisha kuchomwa moto, ni hatari hiyo ndugu zangu.
Kuna wasaliti wa ndoa zao wamewahi kufumaniwa na kupigwa hadi wako vilema hadi leo, ni hatari hiyo ndugu zangu.
Ndugu zangu ni saa ya kuokoka na kuachana na maovu hayo.
Ni saa ya kumpokea YESU kama Mwokozi na kuanza kuishi maisha matakatifu katika yeye.

1 Kor 6:9-10 ''
Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.''

 Wewe ni mlawiti na mfiraji na kwa uovu wako huo unajiona mjanja, ndugu ujanja huo ni tiketi yako ya jehanamu, geuka leo na tubu dhambi zako na anza kuishi sasa maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani.
Ulevi na uabudu sanamu wako hata kama unauona ujanja lakini nakuambia kwamba ujanja huo unaweza kukupeleka ziwa la moto, geuka leo kwa kuokoka.
Watoto wa Nuhu wakubwa walijiona wajanja baada ya kumchungulia baba yao akiwa uchi, matokeo ya ujanja wao ni laana.
Walilaaniwa na kufanywa watumwa wa ndugu zao.
Kuna watu leo huenda kwa waganga na kujiona wajanja, kumbe ujanja huo ni wa hila na ujanja huo ni tiketi yao ya jehanamu kama hawatapata neema ya kutubu kwa Bwana YESU.
Unaweza ukajiita mjanja au ukaitwa mjanja kwa sababu ya udanganyifu wako.
Unaweza ukajiita mjanja au ukaitwa mjanja kwa sababu tu kila siku unawarubuni mabinti ili uwaambukize magonjwa ya zinaa.
Ndugu ujanja wako huo usipotubu na kuokoka hakika ujanja huo unaweza kukupeleka jehanamu.
Nimekuonya leo tangu mwanzo wa somo hili ili ugeuke na kutubu na kumpokea YESU KRISTO Mwokozi na kuanza kuishi maisha matakatifu katika yeye.
1 Yohana 2:15-17 ''
Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.'
'

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.


Comments