KUVUKA NG'AMBO SALAMA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze neno la MUNGU.
Ukisikia kuna kuvuka maana yake kuna daraja au sehemu unatakiwa uvuke. Mfano hai ni kwamba tumevuka 2016 na kuingia 2017 kwa kusudi la MUNGU tu.
Tumevuka ng'ambo hii kwa kusudi la MUNGU tu, hatutakiwi kulisahau kusudi la MUNGU la kuvuka kwetu.
Kumbuka " Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.-Mhubiri 3:1"

Kila jambo lina majira yake.
Kuna majira ya kuvuka na uwezo wa kutuvusha ni wa MUNGU pekee.
Katika jambo lolote ukitaka kuvuka salama mtegemee MUNGU.
Ukitaka kufika salama mtii MUNGU na neno lake na mtegemee yeye kwa maombi.


Wafilipi 4:13" Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."


Utayaweza yote kama tu MUNGU atakuwezesha.
Katika safari moja wanafunzi wa YESU walitaharuki, Walidhani hawataweza kuvuka ng'ambo.
Neema waliyoipata walikuwa na Mfalme wa wafalme YESU KRISTO Mwokozi

Marko 4:35-41 ''Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?  ''
Wanafunzi wa YESU walikuwa pamoja na YESU anayeweza yote.
Katika magumu unayopitia mteule haina maana kwamba huna YESU.
Wanafunzi wa YESU walikuwa hawajajua ukuu wa YESU kwamba hata bahari inamtii.
Kuvuka ng'ambo kunamhitaji YESU akuwezeshe.
Hata wewe inawezekana hujajua ukuu wa YESU na uwezo wako katika maombi ndio maana unaogopa na kukosa amani.
Ndugu omba kwa YESU na atakushindia, bahari na upepo vinamtii itashindikana nini hizo nguvu za giza kukuacha?
Ndugu, kuna kuvuka salama ukiwa na YESU KRISTO.
Ni kweli inawezekana unaumwa lakini naomba ujue kwamba kuna kuvuka salama kama ukimuomba MUNGU.
Ni kweli umefeli katika mitihani, ni kweli umeondokewa na mtu muhimu sana, ni kweli umefukuzwa kazi au umesimamishwa kazi. Ndugu yangu, licha ya magumu hayo uliyonayo lakini naomba ujue kwamba kuna kuvuka ng'ambo salama ukiwa na YESU KRISTO.
Ukiwa na YESU kuna kuvuka salama ndugu.
Bwana YESU akupe kuvuka salama.


Wewe sio wa kwanza kupitia haki ngumu. Wengi walipitia magumu na kushinda baada ya kumtegemea MUNGU Baba.
Zaburi 69:1-4 " Ee MUNGU, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha. Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja MUNGU wangu. Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua."


Ndugu yangu naomba ujue kwamba kuna kuvuka salama hakika ukiwa na YESU KRISTO.
Naomba ujue kwamba mawakala wa shetani huwa hawakati tamaa. Kama shetani hakati tamaa wewe mteule wa MUNGU Fanya Mara. Mbili yake yaani usikate tamaa zaidi na omba MUNGU awaangamize mbele yako.
Wachawi huharibiwa na wakuu wa Giza huangamia, wewe songa mbele na YESU mwenye ushindi wako.

Inawezekana uko jangwani sasa.
Jangwani hakuna chakula wala mvua.
Jangwani hakuna maji, hakuna kimvuli wala chemichemi.
Ndugu hata kama uko jangwani sasa lakini naomba ujue kwamba ukiwa na YESU na unaishi maisha matakatifu na maombi hakika kuna kuvuka ng'ambo salama.


Yeremia 29:11-13 " Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote."


Nyakati yako ya kulia itaisha na utavuka ng'ambo salama na ng'ambo yako iko furaha na kushangilia.
Ni kweli sasa unachekwa na kudharauliwa, lakini kuna kuvuka salama ukiwa na YESU, ukivuka utakutana na kuheshimiwa, heshima yako ambayo muda huu haipo lakini utavuka salama na heshima yako itarudi. Ni muda wako tu ndugu wa kuomba na kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa Bwana YESU.
Inawezekana umekuwa mtu wa kuachwa tu wa wachumba lakini ukimtii MUNGU utavuka salama na kuingia katika ndoa takatifu.
Waliokuwazia mabaya yatawapata wao, mtii tu MUNGU na mtegemee yeye kwa maombi na utakatifu katika YESU KRISTO.
Naomba nikupe kanuni njema kwamba umpende sana YESU KRISTO katika maisha yako.
Kumpenda YESU sana maana yake ni unamtii sana yeye na neno la MUNGU.
Ndugu ukifanya hivyo hakika kunakuvuka ng'ambo salama.
Inawezekana sasa huna kazi, ng'ambo yako ni kupata kazi.
Inawezekana kwa sasa hata mchumba umekosa, ng'ambo yako ni ndoa takatifu.
Inawezekana kwa sasa kuna vita katika ndoa yako, ng'ambo na kuna na amani na furaha katika ndoa yako.
Kanisa la MUNGU linatimiza kusudi la MUNGU sasa, ng'ambo yetu ni uzima wa milele.
Ndugu zangu ni muhimu sana kuishi maisha matakatifu ili tuvuke ng'ambo salama.


1 Petro 5:6-11 '' Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na MUNGU wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika KRISTO, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina.''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments