MAOMBI YA KUPIGA UPOFU MAADUI ZAKO WA ROHONI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi mkuu.
Maombi ndio moyo wa Mkristo.
Maombi ndio ufunguo wa kufungulia kila jambo.
Maombi yenye majibu mazuri ni maombi yanayoambatana na utakatifu.
Utakatifu na imani na Maombi huleta majibu yako kutoka kwa MUNGU muumbaji wako.

Mtu anayekujua vizuri zaidi ndiye rahisi sana kuwa adui yako. Usiweke tumaini kwa wanadamu bali weka tumaini lako kwa MUNGU.
Mapepo Hayajali Cheo Cha Mtu Ila Yanaogopa Moyo Ulio Mkamilifu Kwa KRISTO YESU.
Maombi ya kupiga upofu macho yote ya kipepo yanayokufuatilia ni muhimu sana. Kama kuna jicho la kichawi linakufuatilia kila uendako hakikisha kwa jina la YESU piga upofu kazi hiyo ya shetani.
2 Wafalme 6:18 ''Na walipomtelemkia Elisha akamwomba Bwana, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha.'

Katika Biblia,  Kitabu hicho cha Samweli wa pili sura ya 6 kuna kisa ambacho kinawazungumzia washami waliotaka kuliangamiza taifa la MUNGU.
Elisha nabii alikuwa anaona rohoni kila mpango wa washami kwa Israeli.
Washami baadae wakagundua kwamba sio akili ya kawaida inayoweza kubaini mipango yao ya vita walioifanya sirini, wakajua kwamba Elisha Nabii ndio alikuwa anaona rohoni na kumjulisha Mfalme wa Israeli na jeshi lake. Mfalme wa  Shami na majenerali wake wakaona njia ya kushinda vita ni kumkamata Elisha, Wakatuma jeshi kubwa ili kumkamata. Elisha akaomba maombi kama ambayo tunayaomba leo yaani akamuomba MUNGU awapige upofu maadui wale.
MUNGU anajibu maombi ya watumishi wake ndio maana Biblia inasema MUNGU ''Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha. ''
Leo ni nafasi yako mteule wa KRISTO kuwapiga upofu kwa damu ya YESU kila maadui zako katika ulimwengu wa roho.
Maombi haya ni muhimu sana maana maadui watakutafuta na hawatakuona maana umewapiga upofu kwa jina la YESU.
Kama kuna roho za kuzimu zimetumwa katika ndoa yako, kazi yako, Elimu yako, uchumba wako au Biashara yako ili kuharibu, leo piga upofu hao kwa jina la YESU KRISTO na kwa damu ya YESU KRISTO.
Kama kuna  mizimu inataka kukuletea magonjwa yaliyowatesa babu zako, piga upofu kwa damu ya YESU.
Kama kuna wafanyakazi wenzako shetani amewavamia na wanapanga kukuharibia kazi, wapige upofu na watashangaa japokuwa mipango waliipanga ili ufukuzwe kazi lakini watashangaa miaka 2 hadi 4 ijayo jambo hilo wala halitokei, watashangaa maana hadi watahama kituo cha kazi huku wewe ukiendelea kupandishwa cheo maana uliwapiga upofu katika mabaya waliyokuwazia.
Biblia inakuruhusu Kuomba juu ya hilo, Bwana YESU anasema  ndani ya Biblia kwamba  '' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.-Yohana 14:13-14''
Leo kazi yetu ni kuwapiga upofu maadui waote wa rohoni.
Wakati mwingine kwa sababu umewapiga upofu maadui zako rohoni basi watajikuta wanakusaidia kuendelea na sio kuharibikiwa.
Mabaya yao MUNGU anaweza kuyageuza kuwa mema kwako, kuwa yenye faida kwako.
Leo hakika kuna ushindi mkuu katika jina la YESU KRISTO.
Maombi haya naomba yamsaidie muombaji mchanga ili aweze kuomba akiliendea hitaji lake.
Kwa waombaji wazoefu naamini kabisa kwa kulisoma tu somo basi utajua ni wapi upige upofu.
Kitabu cha ''MAOMBI YA KINA'' bado sijakikamilisha, ukipenda kunisapoti basi MUNGU wa mbinguni akubariki sana na unaweza kunitumia kutokea mtandao wowote kuja namba yangu ya tigo hapo chini ambayo hiyo namba ipo pia mwisho wa kila somo langu ambapo hili la leo ni somo la 593.

MAOMBI YA KUWAPIGA UPOFU MAADUI WOTE WA ROHONI.

BABA katika jina la YESU KRISTO ninakuabudu na kukusifu maana umenilinda na kunipa uzima wako.
Wewe ni YAHWEH MUNGU mweza yote.
Neno lako linakutambulisha katika Luka 1:37 ya kwamba wewe unaweza yote.
Neno lako pia linakutambulisha katika Yeremia 10:6 ya kwamba Hakuna aliye kama wewe MUNGU, Wewe ni mkuu na jina lako ni kuu katika uwezo.
MUNGU wangu nakuomba unisamehe na kunisafisha uovu wangu wote, nipe moyo wa toba na moyo wa kukutii wewe na Neno lako.
Nakushukuru kwa ajili ya siku ya leo ambayo umeileta mbele yangu ili niombe kwa habari ya maadui zangu kupigwa upofu na wewe kupitia damu ya YESU na jina la YESU KRISTO.
Katika jina la YESU KRISTO ninawapiga upofu wachawi wote wanaonifuatilia na kufuatilia maisha yangu.
Kila jini aliyetumwa ili kuniharibia ndoa yangu au uchumba wangu, ninampiga upofu kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai. 
majini wanaojigeuza wanaume/Wanawake wa ndotoni ili kunifanya nisiolewe/Nisioe maisha yangu yote, nawaharibu kwa damu ya YESU KRISTO, na nawapiga upofu na hawataniona tena milele. Sasa Nitaolewa/ Nitaoa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO Mfalme wa uzima.
Wachawi hawataiona ndoa yangu na wala hawataiona sehemu yangu ya Biashara, Wachawi hawatauona mwili wangu na hawataweza kuniletea magonjwa tena, Nawapiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila waganga na uganga wao, Nawapiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila washirikina na ushirikina wao,Nawapiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila wakuu wa giza na giza lao, Nawapiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila majeshi ya shetani katika ulimwengu wa roho, Nawapiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila wanadamu wanaotumika kishetani dhidi yangu, Nawapiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila anayetaka kuniharibia biashara yangu, Nampiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila anayeniendea kwa waganga, Nampiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila anayenichonganisha kazini au kwa ndugu zangu,
Nampiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila anayeninenea mabaya, Nampiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila aliyekusudia mabaya kwangu, Nampiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila roho ya shetani inayonifuatilia, kokote iliko naipiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila macho ya kishetani yanayonichunguza ili kuniharibia, napiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nakushukuru MUNGU BABA maana maadui zangu wote katika ulimwengu wa roho umewapiga upofu na sasa hawataniona tena na hawataweza kunitendea kusudi lao baya tena .
Asante Bwana YESU maana damu yako ya thamani sana sasa inanena mema katika maisha yangu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Amen Amen.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments