Mungu akuondolee zuio lolote linalokwamisha mafanikio yako aliyokupangia

Na Mwl Christopher Mwakasege
Bwana Yesu asifiwe katika mwaka huu wa 2017, na aendelee kusifiwa milele!
Salamu zetu za mwaka mpya kwako, ni kukujulisha ya kuwa tunakuombea wewe unayeusoma ujumbe huu,"Mungu akuondolee zuio lolote linalokwamisha mafanikio yako aliyokupangia katika mwaka huu wa 2017.
Kila mtu anayetaka kufanikiwa, huwa anakutana na vipingamiza vinavyokuwa vizuizi vinavyotumika kuzuia kufanikiwa kwake!
Tunajua mafanikio hayaji kwa maombi peke yake! Lakini biblia inatupa kufahamu kuwa, maombi yanayojibiwa na Mungu, yana sehemu kubwa katika kutengeneza mazingira ya mtu kufanikiwa!
Mzee Yohana aliwahi kumwombea Gayo akisema:"Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama roho yako ifanikiwavyo" (3Yohana 1:2)
Ndiyo maana salamu zetu kwako wewe usomae ujumbe huu, wa salamu zetu za mwaka huu mpya, tunataka ujue tumekuombea na tunakuombea "Mungu akuondolee zuio lolote linalokwamisha mafanikio yako aliyokupangia!


i)Ikiwa ni Roho wake amekuzuia kama alivyomzuia Paulo basi, tunakuombea akuonyeshe njia nyingine iliyo mapenzi yake na itayokufanikisha kama apendavyo (Matendo ya Mitume 16:6-10)


ii)Ikiwa ni shetani amekuzuia (1 Wathesalonike 2:18), Mungu ampangue na kumwondoa katika hilo analokuzuia usifanikiwe!


iii)Je, ni wanadamu?Mungu akutangulie na kuiyeyusha mioyo ya hao wanaokuzuia usifanikiwe (Kutoka 23:27,28)


iv)Je, ni mazingira? Mungu akusaidie pia ili mazingira yafanyike rafiki kwa mafanikio yako! Kama Mungu alivyoondoa "mlima" mbele ya "Zerubabeli"....aondoe vile vile mazingira yaliyo kizuizi kwa mafanikio yako (Zekaria 4:6,7)!


v)Je, ni wewe mwenyewe unajikwamisha? Mungu akupe imani itakayokuvusha ulipo, ili usikwamie hapo (Waebrania 3:18,19. Zaburi 78:40-43)!


vi)Je, ni jaribu limekusonga? Mungu akupe njia ya kutokea, ili usije ukajaribiwa kupita kiwango cha kushindwa kustahimili, (1Wakorintho 10:13)!


vii)Je, mambo yako yamekuwa kama vile milango ya mafanikio yako imefungwa kila mahali? Ni maombi yetu kwamba Mungu akufungulie milango ya mafanikio ambayo hakuna mtu atakayeifunga,(Ufunuo wa Yohana 3:7,8)


Tunatarajia kusikia shuhuda za mafanikio toka kwako, katika mwaka huu, zinazomtukuza Mungu katika Kristo Yesu. Amina!

Comments