MUNGU ANATAKA MATUNDA MEMA KWAKO HUKU UKILITIMIZA KUSUDI LAKE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Karibu nikujuze kile ambacho MUNGU anakitaka kwako.
Luka 13:6-9 ''Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.''


MUNGU anataka matunda kwako ndugu.
Umeongezewa mwaka huu kuishi ili uzae matunda mema, huu ni mwaka wako wa nyongeza kwa ajili ya kuzaa matunda mema.
Matunda anayoyataka MUNGU kwako ni wewe kuishi maisha matakatifu.
Matunda anayotaka MUNGU ni wewe ulitimize kusudi la MUNGU kwa kuifanya kazi yake.
Inawezekana umevumiliwa tu kuwepo mwaka huu.
Inawezekana ukiishi maisha matakatifu mwaka huu na ukaamua kuifanya kazi yake MUNGU hakika MUNGU anaweza kukupa miaka mingi ya nyongeza.
Mfalme Hezekia aliongozewa miaka 15 ya kuishi kwa sababu tu aliomba, alitubu na kuacha uovu.
Wewe je?
Wewe je?
Wewe je?
Maamuzi unayo moyoni mwako.
Mfalme Hezekia siku zake za kuishi duniani zilikuwa zimeisha ila maombi na toba yake ikamfanya MUNGU amuongezee Hezekia miaka 15 ya nyongeza.
Isaya 38:1-7 '' Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA, akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu. Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kuwa BWANA atalitimiza jambo hili alilolisema; ''


Kila mtu ukimuuliza kwanini yuko hai atakuambia ni kwa neema ya MUNGU.
Ni kweli tunaishi kwa neema ya MUNGU lakini neema ya MUNGU ina kusudi ndani yake.
Biblia inasema ''Basi zaeni matunda yapasayo toba;-Mathayo 3:8''
 
Ni heri kuzaa matunda mema.
Matunda mema ni kumpokea Bwana YESU kama Mwokozi kisha kuanza kuishi maisha ya kuitii injili yake ya wokovu.
Matunda mema ni kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Matunda mema ni kuishi kwa kulitii Neno la MUNGU huku ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Wakati huu ambao MUNGU ametupa tuishi yatupasa sana kuishi maisha matakatifu katika wokovu wa KRISTO Mwana wa MUNGU.
Ndugu nakuomba zaa matunda mema ayatakayo MUNGU.
Kama hujui wajibu wako kwa MUNGU hakika unaweza ukavuka mwaka hadi mwaka hadi mwaka hadi mwaka hujafanya chochote kwa MUNGU. Unadhani ni kwanini?
Ni Kwa sababu tu hujui wajibu wako kwa MUNGU.

Ezra 10:4 '' Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.''

Ndugu inuka sasa ili ulitumize kusudi la MUNGU.
Kuna karama zingine hazifanyi kazi katika makanisa leo kwa sababu tu wahusika yaani wenye karama hizo Kanisani hawajui wajibu wao kwa MUNGU.
Mimi nakuambia hivi ndugu ''Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende''

Kuna watu leo wamechaguliwa na MUNGU kufanya kazi yake kwa utukufu wake, lakini wao hawajui kusudi la MUNGU juu yao.
Wengine wameamua kufanya tofauti na jinsi ambavyo MUNGU amewaagiza.
Kuna mtu ameitwa na Bwana YESU ili aimbe nyimbo za injili zinazovuta uwepo wa MUNGU lakini yeye kaamua kuimba nyimbo za kidunia na kuuvuta uwepo wa shetani. Kwa sababu ana sauti ya kuimba basi ameamua kuimba nyimbo za kidunia.
Ni kweli karama za MUNGU hazina majuto(Warumi 11:29) Ndio maana MUNGU hajamuondolea karama ya uimbaji lakini kuna jehanamu ya moto kwa waovu.
Waebrania 9:27 ”Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu”.


Ndugu zangu ni muhimu sana kulitambua kusudi la MUNGU kutuokoa.
Ni muhimu sana utambue kusudi la MUNGU la kukuacha hai leo.
Ndugu fanya kazi ya MUNGU.
Mtumikie MUNGU kwa mali yako na kwa muda wako.
Mimi nakuambia kwamba ''Jihadhari basi; kwani BWANA amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.-1 Nyakati 28:10''
Tena nakuambia hivi ''Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.-Ezra 10:4''


Ndugu timiza kusudi la MUNGU.
Kuna watu wamechaguliwa na MUNGU ili waifanye kazi yake.
Kuna watu wanatakiwa kuwasaidia watu jinsi ya kusonga mbele katika Wokovu bila kusitasita.
Kuna watu wamepewa kazi na MUNGU ya kuiimalisha miguu ya wateule inayolegea.
Kuna watu wameitwa na MUNGU ili kutegemeza huduma na watumishi.
Ndugu yangu timiza kusudi la kuitwa kwako, wambie watu wasonge mbele na YESU kwa utakatifu na maombi.
Mimi nasema hivi '' Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya MUNGU; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi. Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.-Isaya 35:3-8'' 


Kuna mengine MUNGU anasubiri wewe mtumishi utamke ndipo MUNGU BABA atende, kama hujui kusudi la kuitwa kwako hakika tambua kwamba unawazuilia hata watu wengine kuja katika Wokovu maana wewe hujui kusudi la kuitwa kwako.
Unaweza ukalisoma sana Neno la MUNGU lakini kama hulitendei kazi haitakusaidia lolote.
MUNGU anasema '' Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao.-Zaburi 16:3''

Ni kazi yako mteule wa MUNGU kuifanya kazi ya MUNGU.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments