ROHO WA MUNGU AKIWA JUU YAKO NA AKAKUPAKA MAFUTA UFANYEJE?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la Uzima.
ROHO MTAKATIFU akiwa juu yako ufanyeje?
Luka 4:18-19 '' Roho wa BWANA  yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa.''

Ilikuwa siku moja Jioni mimi Peter nikiwa Kanisani ROHO MTAKATIFU alinisemesha juu ya Maandiko hayo ya Luka 4:18-19.
 Maandiko hayo nilikuwa nayafahamu lakini alipoanza kunifundisha kwa sauti ndipo nilipoelewa na nilishangaa sana. Hayo niliyojulishwa ndiyo na mimi nakujulisha leo.
 ROHO wa MUNGU akiwa juu yako  na akakutia mafuta yake ni lazima uwe mtu wa tofauti.
 Kuna viwango vitatu vya nguvu za ROHO MTAKATIFU kwa mteule wa MUNGU katika KRISTO YESU.
=Kiwango cha kwanza cha nguvu za ROHO MTAKATIFU ni Kubatizwa kwa ROHO MTAKATIFU au ujazo wa ROHO MTAKATIFU kwa mara ya kwanza.
=Kiwango cha pili cha nguvu za ROHO MTAKATIFU ndani ya  Mwamini ni Kufurika ROHO au kujazwa endelevu.
=Kiwango cha tatu cha nguvu za ROHO MTAKATIFU ndani ya mwamini ni Kutiwa Mafuta ya ROHO MTAKATIFU.
Kiwango cha tatu ndicho hicho ambacho Biblia inazungumza katika Luka 4:18-19.
Ukifikia kiwango hicho  unatakiwa uwe mtu wa tofauti na mwanzo.
Kwanini uwe mtu wa tofauti?
Ona kile ambacho walikifanya wale ambao ROHO MTAKATIFU alikuwa juu yao na akawatia mafuta yake.

Isaya 61:1-2 '' Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha MUNGU wetu; kuwafariji wote waliao;''

 Kama ROHO wa MUNGU akiwa juu yetu na akatutia mafuta yake kazi yetu ni kuhubiri injili ya wokovu wa KRISTO YESU.
Kazi yetu ni kuhubiri habari njema ambazo ni injili.
Kazi yetu ni kwaombea watu ili wafunguliwe kwa jina la YESU KRISTO.
Kazi yetu ni kuwafundisha na kuwaombea vipofu wa kiroho ili wapate kuona  baaada ya kuwahubiria.
Kazi yetu ni kuihubiri injili ya KRISTO inayowaacha huru wale waliofungwa.
Kazi yetu ni kutangaza mwaka wa MUNGU uliokubalika wa wokovu na kufunguliwa.
Kutangaza saa ya watu kufunguliwa, kutangaza saa ya watu kuokolewa na Bwana YESU maana injili ina wokovu wa  uzima wa milele.
Hizo ndizo kazi zetu kama ROHO MTAKATIFU akiwa juu yetu na kutupaka mafuta.
Mafuta ya ROHO MTAKATIFU sio mafuta haya ya kawaida, sio mafuta ambayo baadhi ya watu huwapaka watu au hujipaka.
Mafuta ya ROHO MTAKATIFU ni nguvu zake kuu sana ambazo ukizipata hizo unatenda makuu sana na unakuwa mtu wa tofauti na Mwanzo.

  1 Yohana 2:20,27 '' Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.''

 Mafuta ya ROHO MTAKATIFU ni nguvu zake na nguvu hizo zitakufanya uifanye kazi ya MUNGU kwa usahihi.
Nimesema kutiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU sio yale mafuta ambayo watu wanapakwa kichwani au mikononi makanisani.
Mafuta ya ROHO MTAKATIFU ni nguvu zake kuu sana.
Kutiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU ni kiwango cha tatu cha viwango vya ROHO MTAKATIFU ndani ya mwamini.

 2 Kor 1:21-22 ''Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika KRISTO, na kututia mafuta, ni MUNGU, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya ROHO mioyoni mwetu.''

Tumetiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU ili tuifanye kazi ya MUNGU vyema.
MUNGU ametupa arabuni ya ROHO mioyoni mwetu. Neno Arabuni maana yake rehani hivyo arabuni ya ROHO maana yake MUNGU amtupa ROHO MTAKATIFU kama rehani ndani yetu ya kutusaidia kushinda mambo yote ya duniani.
Arabuni ya ROHO ni muhuri wa ROHO MTAKATIFU ndani yetu kututhibitisha kwamba hakika tu watoto wa MUNGU waliosafishwa kwa damu ya thamani sana ya YESU KRISTO Mwokozi wetu.
Sasa  ni muhimu sana kujua kwamba Waliotiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU sio waongo wala wasengenyaji.
Waliotiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU sio wazinzi wala wezi.
Waliotiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU sio wafanya maovu.
Kama kuna mtumishi anasema ametiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU kisha anafanya uovu  na dhambi, huyo hakutiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU bali anajitangaza tu bure.
Mtumishi aliyepakwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU ni lazima afanye tu maagizo ya Hiyo Luka 4:18-19  yaani aifanye kazi ya MUNGU kwa usahihi na sio kutafuta pesa ya aibu na kudanganya watu na kuendelea na dhambi za uzinzi na zinginezo.
Waliotiwa mafuta ya ROHO wa MUNGU kazi yao ni kuhubiri habari njema za ufalme wa MUNGU ambazo ni injili.
 Waliotiwa mafuta ya ROHO wa MUNGU ni kuwaombea watu na wanafunguliwa kwa maombi yao.
Waliotiwa mafuta ya ROHO wa MUNGU kazi yao ni kuwaeleza watu matendo makuu ya MUNGU ya kuwafanya watoke kwenye hali ya vipofu wa rohoni .
Waliotiwa mafuta ya ROHO wa MUNGU  kazi yao ni kuwafundisha watu kweli ya MUNGU ambapo hiyo kweli ya MUNGU itawaweka huru.
Watumishi wanaojitangaza kwamba wamepakwa mafuta  ya ROHO MTAKATIFU kisha hawafanyi hayo yawapasayo waliotiwa mafuta ya ROHO, Hao hakika hawajatiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU.
Waliotiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU Biblia inasema  '' Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;-1 Petro 2:9'

 Kila mteule wa KRISTO anatakiwa kupakwa matiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU.
Kila aliyeokolewa na Bwana YESU anatakiwa kutiwa mafuta ya ROHO wa MUNGU.
Kanisa la MUNGU ni muhimu sana likajaa ROHO MTAKATIFU.
Moja ya faida kuu za mteule wa MUNGU ni kutiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU.
Hebu ona Faida za mtumishi wa MUNGU Daudi katika kutiwa kwake mafuta ya ROHO wa MUNGU.
 ''Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu. Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu. Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa. Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia. Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.- Zaburi 89:20-24 ''
Ukitiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU hakika wewe unakuwa mshindi rohoni maana aliye upande wako ambaye ni ROHO MTAKATAIFU ni mkuu sana kuliko wote.
Baada ya Daudi kutiwa mafuta Biblia inasema Mkono wa MUNGU ulikuwa juu yake, kwanini isiwe kwako leo unayesoma ujumbe huu?
 Adui hatamuonea wala wana wa uovu hawatamtesa.
MUNGU atawapiga wanaomchukia na MUNGU atatukuzwa sana kupitia Daudi. Ndivyo ilivyo hata sasa.
Ndugu yangu ahadi ya ROHO MTAKATIFU ni ahadi ya kwako wewe uliyeokoka.
Unatakiwa tu uishi maisha matakatifu, ujifunze kuhusu ROHO MTAKATIFU utendaji kazi wake kwa mwamini, uwe na kiu ya kujazwa na kaa katika kusudi la MUNGU na ukimtii KRISTO na Neno lake hakika wewe utatiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU.
Nguvu ya ROHO MTAKATIFU katika Kigiriki inaitwa ''dunamis''  yaani ni ule uweza wa kuonesha ile mamlaka kuu ya MUNGU tuliyonayo, Ni nguvu zaidi ya nguvu za kawaida, ni uwezo wa ROHO MTAKATIFU utokao juu ambao hakuna anayeweza kushindana nao ndio maana vimvuli tu vya akina Petro viliweza kuponya wagonjwa wengi kwa sababu tu ya kutiwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU na kuwa na ROHO MTAKATIFU ndani yao.
Kwa Mkristo hakuna nguvu za rohoni pasipo kuwa na ROHO MTAKATIFU.
 Mengi sana unaweza ukayashinda kama tu ukiwa na ROHO MTAKATIFU na ukamtii na kukubali akuongoze daima.
Utamtukuza MUNGU ipasavyo kwa sababu ya kuwa na ROHO wake na kukubali kuongezeka kiroho.
 Zaburi 23:5-6 ''Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.   ''
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments