WEWE HUWA UNAISOMAJE BIBLIA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Je wewe huwa unaisomaje Biblia?

1. Je huwa unaisoma Biblia kidhehebu ili ikupendelee dhehebu lako?
2. Je huwa unaisoma Biblia kidini ili ikusapoti kwenye dini yako?
3. Je huwa unaisoma Biblia kielimu ya kidunia ili ikusapoti katika baadhi ya hotuba zako?
4. Je huwa unaisoma Biblia kwa mtazamo wa falsafa yako au sayansi ili ikusapoti katika baadhi ya vipengele?
5. Je huwa unaisoma Biblia kwa mtazamo wa kazi yako ili ukusapoti kwa baadhi ya kauli zako?
6. Je huwa unaisoma Biblia Vipande vipande tu uvitakavyo?
7. Je huwa unaisoma Biblia kwa jinsi ya KRISTO?

Biblia ni neno pekee hai la MUNGU aliye hai.
Copy moja original tunayo duniani na copy nyingine moja original iko mbinguni, utaonekana tu muongo na uongo wako hautakusaidia kama utaitumia Biblia vibaya au utaisoma vibaya au utaisoma kwa malengo yango na sio ya MUNGU.
Waliojaribu kuibadili Biblia waliishia kufa tu huku Biblia halisi ikiendelea mbele..
Biblia ni Neno la MUNGU lililohakikishwa na MUNGU mwenyewe aliyelileta ili litusaidie sisi wanadamu.
Mithali 30:5-6 '' Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.''


Kila Neno la MUNGU katika Biblia lina kazi nne(4)
1. Kufundisha wanadamu.
2. Kuonya watu makosa yao.
3. Kuwaongoza watu.
4. Kuwaadabisha katika haki wanadamu.

Ukitaka kujua kazi nne hizo za Neno la MUNGU soma 2 Timotheo 3:16-17 ambao Biblia inasema '' Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU , lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa MUNGU awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.''

Kila mwanadamu anayeuhitaji uzima wa milele na anahitaji kumpendeza MUNGU inampasa kuisoma Biblia kwa jinsi ya KRISTO tu na kuielewa pia kuitii.
Wakolosai 3:16 ''Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu.''

Neno la KRISTO linatakiwa likae kwa wingi ndani ya kila mwanadamu na alitendee kazi ndipo atatenda vyema sana.
Leo kuna mashindano mengi sana kati ya dini na dini, dhehebu na dhehebu na katika ya mtu na mtu kwa sababu tu ya kila kundi kuisoma Biblia katika mitazamo yao na sio mtazamo wa MUNGU wa wakati huu.
Watu hawasomi Biblia katika mtazamo wa ROHO MTAKATIFU ambaye ndiye aliyeiandika Biblia.
Mabishano hayo hayawezi kumsaidia mtu yeyote.
Wakati huu ni wakati wa kuihubiri injili ya KRISTO inayookoa, hilo ndilo Neno la KRISTO linalotakiwa kuwa ndani ya kila mtu na alifanyie kazi.


Ndio maana Biblia inawaambia watumishi wa MUNGU kuwasaidia watu ili wasiishie kubishana tu huku hawana utakatifu ndani yao na wala hawatimizi kusudi la MUNGU na la wao kuwa duniani hai leo.
Biblia inasema
2 Timotheo 2:14 '' Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa MUNGU , wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.'' 


Wengi hawatimizi kusudi la MUNGU kwa sababu wanaisoma Biblia katika mitazamo ya dini zao au madhehebu yao tu. Hao huchambua baadhi tu ya maandiko na mengine hawashughuliki nayo. Mfano kama kuna watu Hawali wanyama fulani lakini wanasahau kuwa aliyeumba hao wanyama ndiyo huyo huyo ambaye mwanzo aliwaambiwa waisraeli wasile wanyama hao lakini waisraeli walipovunja agano lake, yeye aliandaa agano jipya na akavitakasa vyakula hivyo na kuruhusu kuvila tena akisema kwamba mtu hawi najisi kwa vyakula bali mtu anakuwa najisi kwa sababu ya mawazo yake mabaya. Hilo ni jambo la Kumwelewa tu MUNGU na mpango wake kwa nyakati hii tuliyopo.

Kuna watu kwa sababu tu wanaabudu sanamu basi huyaacha kuyasoma na kuyazingatia maandiko yanayokataza sanamu na kwa njia hiyo wanakuwa wanapishana na mbingu kimya kimya.
Kuna watu kwa sababu hawampendi YESU na wokovu wake basi hao huanza kudanganya watu kwamba YESU ni malaika tu mara yeye ni mwanadamu tu, hao hujitenga na uzima wake wa milele kwa sababu ya kukosa kumtegemea ROHO MTAKATIFU.
Kuna watu hawataki kusikia kwamba YESU ni Mwana wa MUNGU na kwa njia hiyo wao hujitenga na uzima wake kwa sababu hawataweza kumtii yeye ambaye ndiye aliye na uzima wao wa milele.
Wengine wamekalia kusema tu YESU ni mtume kama mitume wengine lakini wanashindwa kujua kwamba ni yeye Pekee alitoka Mbinguni(Yohana 3:31) na wanasahu kwamba yeye ndiye aliyechagua mitume kabla mwanadamu yeyote hajaitwa mtume, maana maandiko mengine yote yalitokea baadae sana baada ya YESU kuchagua Mitume. Hivyo wale waliojiita mitume baade baada ya YESU kuchagua mitume, hao waliiba tu jina la utume ili wazitumike dini zao za kishetani.
Kuna watu hadi wamejiwekea Biblia zao zilizoondolewa baadhi ya maneno au maana za awali ili tu watimize matakwa yao, hao hujitenga na MUNGU hata kama wanamtaja sana.
Kuna watu wao ni wadhambi wakubwa sana lakini kwa sababu na nafasi zao katika serikali au jamii basi hutumia baadhi ya maandiko ya Biblia ili yawasaidie katika mikakati yao, hao hawajamjua MUNGU bado na hawajajua kusudi la MUNGU kulileta Neno lake kwa wanadamu.
Hadi wasanii wa nyimbo za kidunia leo huweka maandiko ya Biblia kwenye nyimbo zao za kishetani ili kuwadanganya watu wasio na ufahamu wa MUNGU na Neno lake.
Ni heri sana kila mwanadamu angekuwa na mtazamo huu katika Neno la MUNGU.


Zaburi 119:72 ''Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.''
Sheria ya kinywa cha MUNGU ndio Neno lake ndio Biblia takatifu. Hiyo sheria inatakiwa kuwa njema kwa kila mtu na mtu huyo amtii MUNGU kupitia sheria yake ambayo ni Neno lake.
Kila mtu anatakiwa awe analisoma Neno la MUNGU kwa jinsi ya KRISTO ili Neno limsaidie kumtii MUNGU na mpango wake wa wokovu kwa wakati huu.
Neno la MUNGU ni la MUNGU tu na limehakikisha mara saba.
Hatutakiwi kulitumia vibaya Neno la MUNGU.


'' Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.-Zaburi 12:6 ''

Tangu kitabu cha Mwanzo hadi Kitabu cha Ufunuo kuna Neno la KRISTO lililotayari kutusaidia ili tumtii MUNGU na tuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi wetu.
Ni heri sana kuliruhusu Neno la MUNGU likatutengeneza vile atakavyo MUNGU.
Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''


Ndugu yangu, naomba ujue kwamba ukiisoma Biblia kidini hakika hutaielewa, iue kwanza hiyo dini ndani yako ndipo ulisome Neno la MUNGU na utaelewa mpango wa MUNGU.
Ukiisoma Biblia kidhehebu hakika hutaielewa, ua kwanza huo udhehebu ndani yako ndipo utaielewa Biblia vile atakvyo MUNGU.
Wewe mwanasiasa acha kuitumia Biblia ili ikufanye kuaminika katika siasa wakati wewe sio mcha MUNGU.
Wewe mwimbaji wa kidunia acha kuitumia Biblia ili uwe na mashabiki wakristo wakati kazi uifanyao ni ya shetani.
Wewe mtumishi unayeitumia Biblia ili kupata fedha za aibu acha hiyo tabia leo.
Wewe kijana unayetumia maandiko ili kumdangaya binti ili umpate kimapenzi acha uovu huo.
Wewe MpingaKRISTO ambaye ingawa unajua kwamba ni Biblia pekee ndilo hasa Neno la MUNGU lakini unatumia baadhi ya maandiko ya Biblia kwa kunyofoa ili tu ikusapoti kwenye dini yako, wewe umepotea na u mtoto wa shetani.
Bwana YESU anasema '' Afadhali, heri walisikiao neno la MUNGU na kulishika.-Luka 11:28 ''


Wala usije ukajisema kwamba una MUNGU wakati unamkataa YESU KRISTO na Wokovu wake.
Unaweza ukajiona una Neno la MUNGU lakini kama unamkataa YESU hakika wewe huna Neno la MUNGU.
Biblia inakuonya.
Yohana 5:38 ''Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye.'' 


Ni muhimu sana kila mwanadamu awe na Neno la KRISTO ndani yake na alitii Neno la KRISTO maishani mwake.
Yeye YESU Mwenye Neno lake takatifu anasema.
''Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.-Mathayo 24:35''

Neno lake halitapita kamwe.
Alisema kwamba wachawi na waongo hawataurithi uzima wa milele, hakika wasipotubu na kumpokea hakika hawataurithi uzima wa milele.
Alisema kwamba wazinzi na waasherati hawataurithi uzima wa milele, hakika wasipotubu na kumpokea hawataurithi uzima wa milele.
Alisema kwamba wezi, wala rushwa, wapokea rushwa na walevi hawataurithi uzima wa milele, hakika wasipotubu na kumpokea hakika hawataurithi uzima wa milele.
Kumbuka amesema ''Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe-Mathayo 24:35'' 


Ndugu yangu mpendwa ni muhimu sana kujifunza Neno la MUNGU na kulitafakari usiku na mchana.
Tendea kazi Neno la KRISTO maana hilo ni chakula cha uzima wako.
Yohana 6:27 ''Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, MUNGU.'' 


Ndugu yangu mpendwa, kumbuka waovu watatupwa katika ziwa la moto hivyo kutubu leo ni lazima sana, kutengeneza na MUNGU ni muhimu sana leo.
Mathayo 13:49-50 ''Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.'' 


Ndugu nakuomba husika na Neno la MUNGU tu na litii Neno la KRISTO maana hilo linakutaka uokoke na uishi maisha matakatifu ya Wokovu katika yeye Bwana YESU KRISTO.
Kumbuka Neno lake litadumu milele na litatimiza kusudi la MUNGU hivyo fanyia kazi neno la MUNGU.
1 Petro 1:25 ''Bali Neno la BWANA hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.''
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments