YESU ANA MAJIBU YA AFYA YAKO KAMA TU UKIAMUA KUMTEGEMEA KWA MAOMBI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Shalom kanisa la MUNGU.
Nawasalimu katika jina kuu la YESU KRISTO na karibu tujifunze neno la MUNGU la uzima.
YESU ana majibu ya afya yako kama tu utaamua kumtegemea kupitia maombi yako ya imani katika yeye.


Marko 5:25-29 " Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za YESU, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule."

YESU ana majibu yako kama ukimtegemea yeye kwa imani.
Maandiko hayo tuliyosoma yanaonyesha kwamba Mwanamke huyu hakuhitaji kumgusa YESU Bali kugusa tu vazi lake.
Mwanamke huyu alikuwa anaonekana najisi mbele za watu.
Kwa miaka 12 alikuwa hajui ataponaje.
Ni kama wewe ambavyo Leo hujui utaponaje.
Watu walimdharau na kumtenga mwanamke huyu, kama ambavyo wewe watu wanakutenga kutokana na hali yako ya kuumwaumwa.
Neema ya MUNGU ilipofika alipona.
YESU KRISTO hakika ana jibu la afya yako.
YESU KRISTO ana jibu la ndoa yako.
YESU KRISTO ana jibu la maisha yako.
YESU KRISTO ana jibu la uchumi wako.
Anaweza kuponya chochote muda wowote.
Kuponya YESU wala haimsumbui kabisa maana anaweza kuponya magonjwa yote.


Je unaamini kwamba YESU anaweza kukuponya?
Kama unaamini hakika uponyaji utakuwa kwako.
Muhimu tu anza kumtii MUNGU na neno lake.
Ishi maisha matakatifu katika Wokovu wa YESU KRISTO.
Jitenge na mambo ya dunia yaliyo machukizo kwa MUNGU.
Uwe na imani ya kupona, sio imani ya kufa.
Uwe na imani ya kuwa mzima na husika sasa na kanisa hai la MUNGU.


Kuna funuo nyingi zilizoleta uponyaji kwa wateule wa MUNGU.
Mama ambaye tumesoma habari zake, yeye ufunuo wake ulikuwa ni kushika vazi la YESU Mwokozi na Angepona, hakika alipona.
Ndugu mmoja yeye alipokuwa anaumwa aliamua kutoa sadaka ya shukrani kwa MUNGU akisema MUNGU amemponya, watu walimshangaa maana alikuwa mgonjwa sana bado, lakini kwa maombi hayo akiambatanisha na sadaka ya shukrani kwa MUNGU hakika alipona.
Kuna mtu mwingine alikuwa mgonjwa sana lakini ufunuo wake ulikuwa ni kwenda ibadani kanisani kila siku, wala hakuwa mtu wa kanisa lakini Bwana YESU alimponya kupitia maombi ya kanisani.
Mama mmoja alikuwa mgonjwa miaka 20 lakini kwa kuhudhuria kwake mikutano ya injili alipona bila hata kuwekewa mikono na watumishi.
Ilikuwaje?
Siku hiyo ya uponyaji wake kulikuwa na mkutano wa injili na mtumishi aliye kuwa anahubiri akapata ufunuo kwamba wafanye meza ya BWANA kwenye mkutano ule, wakati walipofanya ibada hiyo takatifu ya meza ya BWANA yule mama alipona.
Penye uwepo wa MUNGU hakika kuna uponyaji wake.
Tatizo la watu wengi ni kutokumtegemea YESU mponyaji wao.
Ndugu yangu, ukweli ni kwamba YESU KRISTO ana majibu yako,Mkimbilie YESU ili akuondolee aibu inayokutesa.

Unataka kujua kama YESU anaponya magonjwa yote?
Mathayo 9:35 "Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na KUPONYA MAGONJWA YOTE NA UDHAIFU WA KILA NAMNA."

Wewe una ugonjwa gani hata YESU ashindwe kukuponya?
Nakuhakikishia kwamba YESU KRISTO anaponya, labda tu tatizo liwe kwako kwa sababu ya imani, kutokuishi maisha matakatifu au kutokumtii MUNGU.
Biblia imesema aliponya magonjwa yote.
Alipona madhaifu yote.
Una udhaifu gani ndugu?
Magonjwa ni udhaifu, madeni ni udhaifu, kukataliwa ni udhaifu, kuchukiwa bila sababu ni udhaifu, Kukosa kazi ni udhaifu, nakadhalika na kadhalika.
Lakini YESU anaponya udhaifu wa kila namna, yaani ukiwemo na udhaifu wako huo.
YESU anaponya magonjwa yote, ukiwemo ugonjwa wako wewe.

Biblia inasema kwa kitendo cha YESU kufa msalabani sisi tumeponya.
YESU alikufa na kufufuka na uzima wetu na uponyaji wetu wote.
Biblia inasema;
"Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu. Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai; kwa kupigwa kwake sisi tumepona.-Isaya 53:5 BHN"


Wakati fulani nikiwa Zanzibar mke wangu alisumbuliwa na maumivu ya tumbo. Alipoenda kupima akakutwa na uvimbe, akaamua kwenda kuhakikisha hospitali mbili zaidi na kuambiwa hivyo hivyo. Madaktari wakamwambia anatakiwa kufanyiwa upasuaji. Ni tukio lililonishangaza sana, ni kitu kigeni kwangu na niliduwaa kupita kawaida. Ikabidi tumuombe MUNGU mponyaji wetu na ashukuriwe MUNGU milele maana kwa jina la YESU KRISTO ule uvimbe ulifutika. Mke wangu akapona na anaendelea kumtumikia JEHOVAH MUNGU aliye hai.
Ndugu yangu ukweli mmoja ni huu, YESU KRISTO ana majibu yako ya ushindi.
Shetani anaweza hata kuyabadili matokeo yako ya mitihani uliyofanya, lakini kwa maombi kupitia jina la YESU KRISTO unafaulu sawa sawa na ulivyosoma ukimtegemea MUNGU.


Biblia inasema;

"MUNGU kwetu sisi ni MUNGU wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.-Zaburi 68:20 "

Tena Biblia ni inasema;
" Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.-Zaburi 83:18

Tena Bwana YESU anasema;
"Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu.-Yohana 14:13-15"

Kisha Biblia inasema;
"Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza.-Yeremia 10:6 

Kazi ya kuutafuta uponyaji wa MUNGU kwako kupitia YESU KRISTO uko kwenye uwezo wako, fanyia kazi itakusaidia sana.
Majibu ya mahitaji yako anayo YESU KRISTO Mfalme wa uzima wa milele.


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments