MSIYACHOCHEE MAPENZI WALA KUYAAMSHA HADI WAKATI WA NDOA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Wimbo 8:4 ''Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwani kuyachochea mapenzi, au kuyaamsha, Hata yatakapoona vema?''
Kama ambavyo Kuna vichocheo vinavyoweza kumwingiza mtu hatiani, vile vile Kuna vitu vinaweza kuchochea watu wakafanya dhambi ya uasherati na uzinzi.
Kama ambavyo kuna vitu vinaweza kumchochea mtu akatenda dhambi, vile vile kuna vichocheo vinavyoweza kumfanya mtu akaingia katika dhambi ya uzinzi.
Tukumbuke kuwa kwa MUNGU hakuna kujitetea wala hakuna kusingizia vichocheo ndivyo vilikufanya uingie dhambini.
 Ufunuo 21:8 '' Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili''. 

Watenda dhambi wasiopata Neema ya KRISTO ya kutubu  na kuacha uovu wataenda jehanamu bila kujali kama vichocheo tu ndivyo vilisababisha wakatenda dhambi, ni hatari sana.
Kuna vitu vinavyoweza kuyaamsha mapenzi hata watu wakafanya mapenzi katika dhambi yaani kabla ya ndoa na wakawa wametenda dhambi kuu.
Biblia inasema tusiyaamshe mapenzi wala kuyachochea hadi muda wake ufike. Muda wa mapenzi kuyachochea na kuyaamsha ni katika ndoa tu baada ya kufunga ndoa takatifu.
Jambo la ajabu leo kuna wanaoyaamsha mapenzi wakati ambao sio sahihi na jambo hilo kuwaletea madhara makubwa katika maisha yao.
Mimba za utotoni nyingi leo zimesababishwa na kuyaamsha mapenzi katika  wakati usio ndani ya ndoa.
Utoaji wa mimba leo umejaa kwa sababu ya kuyaamsha na kuyachochea mapenzi katika muda ambao sio ndani ya ndoa.
Watu wanajiua wakati wa uchumba  kwa sababu tu ya mapenzi lakini chanzo kikiwa ni kuyachochea mapenzi muda ambao sio ndani ya ndoa.
Kuna watu wamejeruhiana kwa silaha na maneno makali kwa sababu tu ya kuyaamsha mapenzi katika muda ambao sio ndani ya ndoa.
Kuna watu wamefukuzwa na wazazi wao kwa sababu tu ya kuyaamsha mapenzi katika muda ambao sio ndani ya ndoa.
Kuna watu wamefukuzwa kazi kwa sababu tu ya kuyaamsha mapenzi katika muda usio sahihi, MUDA SAHIHI WA KUYAAMSHA MAPENZI NI NDANI YA NDOA TU KWENU TU MKE NA MUME TU WAWILI TU MLIOFUNGA NDOA TAKATIFU.
Kuna wanafunzi wengi wamefeli masomo yao kwa sababu tu ya kuyaamsha mapenzi katika muda usio ndani ya ndoa takatifu.
Kuna watu leo ni vilema baada ya kupigwa na wazinzi wenzao kwa sababu tu ya kuyaamsha mapenzi katika muda ambao sio ndani ya ndoa.
Biblia inasema kwa Kanisa la MUNGU kwamba '' Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.-1 Kor 5:10-11''
 
Kuna watu leo hawaongei kwa sababu tu walikuwa wapenzi, wakayaamsha mapenzi katika muda usio ndani ya ndoa kisha wakaachana na kununiana na sasa hawaongei maana wamegeuka maadui kama panya na paka.
Kuna watu leo wamebaki wakisema tu ''NIMEKUSAMEHE LAKINI SITAKUSAHAU'' Kwa sababu tu ya kuyaamsha mapenzi katika muda usio ndani ya ndoa takatifu.
Kuna watu shetani amepanda maroho ya kuwatesa kwa sababu walifungua mlango kipindi kile wanayaamsha mapenzi katika muda usio sahihi.
Kuna watu mioyo yao ina makovu na wamejikuta wakijilaani na kujizuilia kuoa au kuolewa kwa sababu tu walifanya mwanzo Big mistake kwa kuyaamcha mapenzi na kuyachochea kipindi ambacho ni dhambi kwao kuyaamsha maana walikuwa hawajaoana.
Zamani wazinzi na waasherati walikuwa wanauawa.
1Kor 10:8 ''Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. ''

 Leo wazinzi na waasherati hawauawi lakini wasipotubu na kuacha wanaweza kujikuta jehanamu.
Kuna madhara mengi sana katika dhambi ya uzinzi na uasherati.
Inawezekana Kabisa wewe ungesoma ungekuja kuwa waziri au mkuu wa idara kubwa serikalini lakini uasherati wako wakati ukiwa shule unaweza kufuta hiyo baraka yako ya baadae.
Kwa wale ndugu ambao muda wao wa kuoa au kuolewa umefika ni heri ukaoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
Lakini pia tamaa unaweza kuiepuka kama utafuta Neno la MUNGU.
 Kama huna mchumba na muda wako wa kuingia ndani ya ndoa umefika basi omba MUNGU na utapata lakini kumbuka sana kuyachochea mapenzi wakati wa uchumba ni hatari kubwa na inaweza hata kuuvunja uchumba huo kabla ya ndoa.
Yakobo 4:4 '' Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU.''

MAMBO YANAYOCHOCHEA MAPENZI KABLA YA MUDA WA NDOA.

1. Uvaaji mbaya.
Mithali 11:16a '' Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;'' 
Mwanamke na hata mwanaume mwenye adabu huheshimiwa daima.
Adabu mojawapo ni pamoja na mavazi.
Ni muhimu sana kila mtu akawa na adamu katika mavazi.
Leo kuna wanawake wanavaa kikahaba kabisa, huko ni kupungukiwa adabu 100%.
Leo kuna vijana hutembea mitaani kama wanajiuza, huko ni kukosa Adabu.
Biblia inaagiza kanisa kwamba tulichukie hata vazi lililo chafu.
Yuda 1:23 '' na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.'' 

Uvaaji mbaya unaweza sana kuyachocheo mapenzi na kuyaamsha katika muda usio ndani ya ndoa, jambo hilo ni dhambi kwa MUNGU na ni kukosa adabu kwa kiwango cha juu sana.
Leo kuna watu hutembea mitaani matiti nje.
Leo kuna watu hutembea mitaani nguo za ndani zinaonekana.
Leo kuna watu hutembea barabarani makalio yakiwa nje.
Leo kuna watu hutembea mitaaani wakiwa wamevaa nguo za kubana na nyepesi sana hata mtu akiwatazama anawaona hadi ndani ya miili yao kwenye maeneo nyeti.
Leo watu wanavaa vimini hadi maofisini kwao.
Hayo yote ni kama ujanja kwa wapenda dunia lakini ukweli ni kwamba huo ni ujinga na ni machukizo kwa MUNGU, na jambo hilo ni moja ya vichocheo vya ngono, na kama ni vichocheo vya ngono basi pia hivyo tunaweza kusema ni vichocheo vya magonjwa ya zinaa.
1 Timotheo 2:9-10 '' Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa MUNGU.''

2.  Kuwa Boyfriend na Girlfriend.
Wimbo 8:4 ''Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwani kuyachochea mapenzi, au kuyaamsha, Hata yatakapoona vema?  ''
 Hakuna eneo mapenzi huchochewa na kuamshwa kama katika eneo la kuwa na boyfriend au girlfiend.
Leo hadi watoto wa miaka hadi 14 wana boyfriend au girlfriend.
Ingekuwa hiyo inawakalisha tu rafiki wa kiume au rafiki wa kike basi hakika kila Binti au kijana tungesikia ana Boyfriend/Girlfriend  30 hadi 40 lakini kile alichokificha shetani kwenye huo u-boyfriend na u-girlfriend ni uasherati na uzinzi. Ndio maana hakuna kijana mwenye girfriend 50 bali mmoja tu, kwa ajili ya nini? ni kwa ajili ya kuyaamsha mapenzi na uasherati. Huwezi kukuta Binti ana boyfriend 100 bali utakuta binti ana boyfriend mmoja tu kwaajili ya kuyaamsha mapenzi na uasherati.
Kwanza ni vyema tukatambua kwamba Kibiblia hakuna mahusiano ya Boyfriend na Girfriend.
Kama Neno la MUNGU linakataza basi hakuna haja ya Mkristo yeyote kuwa na Girfriend na Boyfriend.
Boyfriend na Girlfriend ni taasisi ya shetani kuwanasa vijana katika chungu kimoja kiitwacho uasherati.
Ndugu nakuomba vunja mahusiano yako na huyo Girlfriend au Boyfriend wako maana hayo ni mali ya shetani ili myachochee mapenzi kabla ya ndoa.
Warumi 6:12 ''Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;''
 
 3. Filamu za ngono, picha za ngono vitabu vya ngono.
Yakobo 1:21 '' Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.''
Biblia inasema tuweke mbali uchafu wote na ubaya na ni heri kupokea Neno la MUNGU linaloweza kuziokoa roho zetu.
Filamu za ngono ni uchafu ambao hauwezi kutuokoa kwa lolote.
Picha za ngono ni machukizo ambayo hayana msaada hata mmoja kwetu.
Hata baadhi ya nyimbo za mapenzi zimetumika kama chombo cha shetani cha kuchocheo mapenzi na kupelekea watu kuzini.
Hata vitabu vyenye vichocheo vya ngono havifai na ni machukizo.
Ukiuliza shuleni au hata Kanisani leo ''Ni nani anaijua filamu ya X au picha ya X'' Utakuta karibia kila mtu anaijua na hufuatilia.

Biblia inasema '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;  wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru.  Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU.-Waefeso 5:3-5 ''

4. Mazoea mabaya kati ya watu wawili wa jinsia mbili tofauti.
 Mithali 6:23-26 ''Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani ''
Kuna unatakiwa ujilinde na mwanamke/ Mwanaume mwovu.
Huyo mwovu wa jinsia tofauti na yako anaweza akaanza mazoea mabaya na wewe ili tu akunase.
Mazoea mabaya hayo kwanza ni kichocheo cha uzinzi na uasherati na pia unaweza kuwa ni mtego kwako ili uingie katika dhambi ya uzinzi na uasherati.
Biblia inasema usiutamani uzuri wa mtu ambaye anafanya mazoea mabaya na wewe, usikubali akunase kwa kope zake wakati wa ukaribu aliouanzisha kwako.
Kuna ukaribu unaweza kutengeneza jehanamu ya mtu, kuna ukaribu unaweza kutengeneza vita na migogoro mibaya.
Kazi ya malaya au kahaba ni kumwinda mtu ili amnase ndivyo maandiko yanavyosema. Sasa kwa njia ya ukaribu na wewe anaweza akawa anakunasa taratibu taratibu hadi ukajikuta uko dhambini.
Ukaribu usio na utakatifu ndani yake ni hatari sana kwako.
Jinsia mbili tofauti kuwa karibu sana wakati mwingine ni kichocheo cha uzinzi.
Warumi 13:14 ''Bali mvaeni Bwana YESU KRISTO, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments