SIO WATUMISHI WOTE WANA ROHO WA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Sio Watumishi wote wana ROHO MTAKATIFU.
Kazi ya ROHO wa MUNGU ndani ya mtu ni pamoja na kumshuhudia KRISTO YESU ndani yetu na kutukumbuka yale ya YESU KRISTO,
Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia ''

ROHO wa MUNGU atamfafanua YESU KRISTO Mwokozi wetu, atamfafanua ndani yetu na Neno lake la injili tutalielewa.
Yohana 15:26 ''Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa BABA, huyo ROHO wa kweli atokaye kwa BABA, yeye atanishuhudia.''

Tena mtu yeyote asiye na ROHO MTAKATIFU huyo sio wake KRISTO.
Warumi 8:9 '' Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake.''

Ndugu zangu,Sio Watumishi wote wana ROHO MTAKATIFU.
Mtumishi mmoja ambaye ni Mchungaji mkubwa katika Nchi moja inayopakana na Tanzania alinionya kwa kuniambia Niache kuwa naanza masomo yangu kwa kusema ''BWANA YESU ATUKUZWE au BWANA YESU ASIFIWE''
Alisema ni makosa makubwa na mimi nikamjibu kwa ukali sana na kumwambia kwamba kama hamjui YESU KRISTO ni nani basi afunge makanisa yake anayoyachunga. Nilimwambia kwamba Kumkataa YESU KRISTO ni kuukataa uzima wa milele.
Baada ya hapo aliogopa lakini akawa akiona masomo yangu baadhi anaandika tu kwenye Comment kwamba ''Sawa Mtumishi wa YESU''
Sasa kama mtu anakwazika tu kutukuzwa kwa Bwana YESU, je mtu kama huyo anategemea mbingu ipi?
Mimi simhukumu yeyote lakini ni heri kutubu na kuanza sasa kumfuata MUNGU katika KRISTO.
YESU KRISTO yuko ndani ya Neno la MUNGU akiokoa kwa wanaotii.
MUNGU yuko ndani ya Neno lake akiokoa wateule wake katika KRISTO.
Mtu kama huyo anayekwaza na Bwana YESU hakika mimi naamini kabisa huyo kanisani kwake huwa hahubiri Wokovu wala injili wala hamhubiri YESU kama Mwokozi wa wote wenye mwili.
Katika kanisa la leo tunatakiwa Neno la KRISTO tu ndilo liwe kwa wingi mioyoni mwetu, sio neno la mtume wala nabii.
Wakolosai 3:16-17 '' Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.''
Ndugu zangu,Sio Watumishi wote wana ROHO MTAKATIFU.
Wengine wana roho ya kuiga.
Wengine wana roho ya kutengeneza.
Wengine wana roho ya shetani.
Wenye roho ya kuiga wengine walianzisha madhehebu na kuwapotosha wengi hadi leo.
Wenye roho ya shetani wengine ni waanzilishi wa madhehebu na sasa wafuasi wao hawamwabudu JEHOVAH bali wanaabudu mapepo.
Wenye roho ya shetani wengine walianzisha madhehebu na kujiita kristo.
Wengine baada ya kuanzisha makanisa yao walijiita Mungu.

Ndugu nakuomba mtii YESU KRISTO na Neno lake hapo ndipo utawabaini kwamba wana Roho gani ndani yao.
1 Yohana 4:1-6 'Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia Sisi twatokana na MUNGU. Yeye amjuaye MUNGU atusikia; yeye asiyetokana na MUNGU hatusikii. Katika hili twamjua ROHO wa kweli, na roho ya upotevu.''

Shetani ni mjanja sana, akiwapata watu na kuwapa dhehebu lao la kipepo huwapa mafundisho ili madhehebu mengine yote yaonekane ni ya shetani kumbe wao ndio wako dhehebu la shetani. Watu hao hukatazwa hata kuhudhuria mikutano ya injili ya wahubiri wengine waliookolewa na Bwana YESU.
Ndugu fulani walinikaribisha katika group la Kanisa lao facebook. Nikawa napost lakini sikuona hata mmoja aki-Comment chochote kwa miezi kazaa. Mimi nilijua wale wanasumbuliwa na udhehebu lakini niligundua kabisa kwamba wanayasoma masomo yangu japokuwa hawayapendi. Baada ya muda kadhaa mmoja katika wao aliniuliza kwamba ''Na wewe ni mmoja wa waaminio ujumbe wa .........(Sitataja kwa sababu maalumu')  Nikamjibu mimi naamini Biblia na YESU KRISTO ni Neno juu ya Neno la MUNGU.
Yule ndugu alijitenga na mimi na baadae ikabidi afundishe katika Group hilo hilo kwamba huwezi kuielewa Biblia hata kidogo kama hujasoma vitabu vya Mwanzilishi wa dhehebu lao.
Niligundua kabisa kwamba hawa ndugu wametengwa na kweli ya Biblia na kweli ya MUNGU kwa sababu wamefundishwa kuwaona wengine kama wamepotea wakati ukweli wao ndio wanahitaji msaada.
Nilichogundua kuna baadhi ya madhehebu waanzilishi wao walikuwa watumishi wa kweli wa Bwana YESU lakini baada ya kufa kwao shetani alianza kutawala madhehebu yale ya kupindua pindua kusudi la Injili ya KRISTO YESU.
Wengine waanzilishi wao walikuwa ni waigizaji au wametumwa na shetani ili kujikusanyia kundi la kupeleka kuzimu.
Ndugu, ukishindwa kumwamini YESU KRISTO na Neno lake kisha unaamini askofu hakika wewe hujitambui.
Kuna watu leo badala ya kumcha MUNGU wao humcha Mwanzilishi wa dhehebu lao.

Biblia inasema kwamba mtu akileta injili nyingine na kuiacha injili ya KRISTO huyo ni mtumishi wa kuzimu.
Wagalatia 1:9 '' Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. ''

Mtu akileta habari za Yesu mwingine huyo alaaniwe.
Mtu akileta habari za MUNGU mwingine nje na JEHOVAH, huyo na alaaniwe.
Yohana 3:17-21 ''Maana MUNGU hakumtuma Mwana(YESU) ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.''
 
Leo watumishi wengi wako busy kufundisha watu kwamba ''Waaminini manabii wa MUNGU''
Biblia inatutaka tumwamini YESU KRISTO.
Kama Mtumishi halibebi Neno la KRISTO kwa usahihi hakika huyo hakuna haja ya kumwamini na hakuna dhambi ya kutokumwamini.
Wengine hujiona ni madhehebu makongwe hivyo ni lazima kuwatii.
Ndugu zangu, Dini kongwe kuliko zote ni Wokovu wa YESU KRISTO.
Dhehebu kongwe kuliko yote ni Wokovu wa YESU KRISTO.
Kuna watu leo wakihubiriwa kuokoka hudhani kwamba wanaletewa dini mpya kumbe Wokovu wa KRISTO ndio dini ya Biblia na ndio kongwe kuliko dini zote.
Mitume wote kwenye Biblia walihubiri injili ya YESU KRISTO iletayo Wokovu kwa watu wote waaminio, Hiyo ndio dini ya kweli na ya zamani kabla ya dini nyingine yeyote.
''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu.-Warumi 6:23''

Uzima wa milele ni katika KRISTO YESU na sio katika dhehebu wala tamaduni.
Uzima wa milele sio katika kumwamini askofu au mtume au nabii au Mchungaji bali ni katika kumwamini YESU KRISTO kama Mwokozi na kisha unaanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu katika yeye.
1 Petro 1;13-16 ''Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake YESU KRISTO. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. ''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments