KWANINI ULIWEKE NENO LA MUNGU MOYONI MWAKO?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU muhimu sana leo.
Neno la MUNGU lina kazi nyingi sana  ndani ya mwamini.
Kama vile ambavyo tunakula chakula cha kimwili ili tuishi na ili tupate afya, hivyo hivyo tunakula chakula cha kiroho ambacho ni Neno la MUNGU ili tuishi kiroho na ili tupate afya kiroho na ili tukue Kiroho.
Neno la MUNGU ni Muhimu sana ndani ya kila mteule wa KRISTO popote aliko.
 Leo tunaangalia umuhimu wa Neno la MUNGU moyoni mwetu.

Je kwanini uliweke Neno la MUNGU moyoni mwako?

1. Ili usitende dhambi kwa kusahau maelekezo ya Neno hilo la MUNGU.
Zaburi 119:11 '' Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''

 
Kumbuka Neno la MUNGU li hai, lina nguvu na linajua.
Waebrania 4:12 '' Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. ''


2. Ili likumulikie uone na kutenda katika mapenzi ya MUNGU.
 
ZaburiI 119:105 ''Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. ''

 
Kumbuka kabla ya kulijua Neno la MUNGU wote tulikuwa wajinga, lakini Neno ndio limetuondolea ujinga na kutupa ufahamu mzuri wa kiMUNGU.
''Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.-Zaburi 119:130''


3. Ili likupe uhakika wa yajayo kama utalitii Neno hilo la MUNGU.
 
Yohana 5:24 '' Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye NENO langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. ''


4. Ili likutakase.
 
Yohana 17:17 '' Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. ''

 
Hivyo tunakuwa safi kwa sababu ya Neno la MUNGU.
''Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.'' Yohana 15:3


5. Ili likuongee Imani kwa MUNGU.
 
Warumi 10:17 '' Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. ''

 
Ukiwa na imani utafanya yote katika Bwana YESU.


Wakolosai 3:17 ''Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye. ''


6. Ili likufanye umshinde shetani kirahisi.
 
Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa NENO la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. ''

 
Kumbuka Neno la MUNGU lina uponyaji na linaponya.


''Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; MANENO hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.-Yohana 6:63''

 
Maneno ya YESU KRISTO(Neno la MUNGU) ni roho tena ni uzima.


7. Ili ulitumie kwa kazi ya MUNGU.
 
''Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali NENO la kweli.'' 2 Timotheo 2:15


8. Ili neno la MUNGU likufundishe kuukulia Wokovu vyema.
 
''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ''1 Petro 2:2

 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments