KWANINI UNATAKA KUMUACHA YESU ILI UIPENDEZE DUNIA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna mtu anaenda kupona kupitia somo hili.
Je umezama kimya kimya?
Umezama kimya kimya kwenye ulevi?
Umezama kimya kimya kwenye uzinzi na uasherati?
Umezama kimya kwenye utapeli?
Je Umezama kimya kimya kwenye kuwategemea waganga wa kienyeji?
Je Umezama kimya kimya kwenye wizi na uongo?

je Umezama kimya kimya kwenye ukahaba?
Inawezekana Umezama katika dhambi lakini ndugu naomba kukujulisha kwamba kuna wengine kama wewe walizama kama wewe ila walipokuja kuibuka walikuwa tayari kuzimu njiapanda ya kwenda jehanamu.
Ndugu yangu, neema ya MUNGU bado ipo kwa ajili yako ili ubadilike.
1 Kor 6:9-10 ''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.''
 Kuna watu leo ukiwahubiria baadhi ya mahubiri ya kuwaonya watakuambia kwamba hawako chini ya sheria bali wako chini ya neema.
Watu hao wanasahau kwamba ingawa wanakunywa pombe na kulewa lakini Biblia inasema kwamba watu wa namna hiyo hawataingia katika ufalme wa MUNGU.
Kuna watu leo hufanya baadhi ya maovu na kuiita kwamba wako chini ya Neema na sio chini ya sheria, wanasahau kwamba Neema ya MUNGU inatufundisha kuacha uovu.
'' Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu;-Tito 2:11-13''
Tena Neno la MUNGU linaonya likisema ole wake mtu yule anayeibadili Neema ya MUNGU kuwa ufisadi.
Ufisadi maana yake uchafu, ni hatari sana kuibadili Neema ya MUNGU kuwa uchafu.
Biblia inasema 
''Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya MUNGU wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu YESU KRISTO.-Yuda 1:3-4.
Ndugu, usikubali kuichezea neema ya MUNGU.
Wokovu ni Leo ndugu, okoka  kweli kweli Leo na jitenge na dhambi, litafute kanisa ili ukampokee YESU maana dhambi hupeleka watu jehanamu.


 Kumbuka kuna wanadamu wanaokufa kwa Bwana YESU na kuna wanaokufa kwa shetani. 
Bwana YESU yuko mbinguni hivyo na wanaokufa katika yeye huenda mbinguni.
 Na shetani yuko kuzimu hivyo wanaokufa katika shetani/ dhambi huenda kuzimu. Unaweza kutazama mfano wa Lazaro na Yule tajiri, Lazaro alipokufa alienda mbinguni kuungana na akina Ibrahimu na tajiri alipokufa alienda kuungana na majini kuzimu.

Wewe unayekataa YESU asikuokoe sio tu kwamba ufahamu wako umekupotosha Bali ufahamu wako umekupoteza kabisa.
1 Yohana 2:22-25 ''Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa YESU ni KRISTO? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba(MUNGU) na Mwana(YESU). Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia. Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba. Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.''
 
 Ndugu nakuomba sana usikubali kumwacha YESU kwa sababu ya mazingira yeyote uliyonayo.
 Inawezekana sana unatamani kuingia katika ndoa lakini kuna vikwazo unapitia, ndugu waliofanikiwa kufunga ndoa hata wao walipitia vikwazo lakini walipomtegemea MUNGU walishinda.
Usikubali kubadili dini ili uipate ndoa na umkose YESU aliye Mwokozi wako.
Vumilia ndugu na maombi na MUNGU atakupa mwenzi aliye mteule wa KRISTO na sio sasa kutaka  kumwacha YESU ili uolewe na wapinga Kristo au uoe mpinga Kristo.
Ndugu nakuomba ng'ang'ania kwa YESU na utapata tu aliye mtu sahihi.

Naamini hata wewe utashinda na muujiza wako wa kufunga ndoa utafika tu.
Songa mbele na YESU kwa utakatifu na Maombi hakika kesho yako ya baraka ya ndoa itafika tu.
Ipo Siku waliokucheka watanuna huku wewe ndio ukiwacheka, lakini kwa vyovyote usikubali kuacha  Wokovu wa KRISTO katika maisha yako.

1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.''

 Binti/Kijana kulia sana baada ya uasherati haikusaidii.
Dawa ni kuacha uasherati na kutubu.
Kuna mabinti/Vijana baada ya kufanya uchafu wao hujuta na kulia na kusema kwamba ilikuwa bahati mbaya lakini baada ya siku chache anafanya uovu huo tena.
Ndugu jehanamu inawangoja waovu hivyo dawa ni kuacha na kutubu na kuanza kumtii KRISTO na neno lake.
Ni heri muda ulioutumia kwenye uzinzi ungeutumia kumwabudu MUNGU na kufanya mambo mema yanayompa MUNGU utukufu.
Nakuonya ndugu.

2 Petro 2:9-14 '' basi, BWANA ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka. Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za BWANA. Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao; Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi; wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;''

Mteule wa KRISTO nakuomba sana zingatia haya:
1. Kataa yote yanayokuondoa katika kusudi la MUNGU.
2. Kataa yote yanayokuondoa katika utakatifu.
3. Yakatae yote yanayofanya injili ya KRISTO itukanwe.
4. Kataa yote yaliyo kinyume na neno la MUNGU.
5. Kataa mambo yote ya dunia yaliyo machukizo kwa MUNGU.
6. Kataa kuwa mtumwa wa kanisa lako, Bali uwe mtumwa wa KRISTO uliye tayari kutumwa na YESU KRISTO.
7. Kataa kulichanganya neno la MUNGU na uongo.

Kumbuka Warumi 6:23 "Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu."
 MUNGU akubariki na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments